TAFUTA HAPA

Hadithi mpya: Moyo wangu 2

DEOGRATIUS alikuwa amelala kimya kitandani, Cleopatra akimwangalia kwa jicho la huruma, simanzi tele ikiwa imemjaa moyoni mwake. Moyo wake unashindwa kuvumilia, macho yake yanazingirwa na unyevunyevu. 
Chozi linadondoka!
Chozi la huzuni!
Deo ametulia kitandani, mwili wake ukiwa umefunikwa kwa shuka jeupe, isipokuwa kuanzia kifuani, bandeji linaonekana mkononi mwake. Mapigo ya moyo wake yanakwenda taratibu kabisa!
“Deo wangu...Deo...Deo jamani...amka mpenzi wangu. Naomba usife kwanza mpenzi wangu jamani. Hebu amka baby, tufunge ndoa...bado nakupenda...” akasema Cleopatra akilia kwa uchungu.
Deo hakusikia kitu, alikuwa katika usingizi mzito, hajui chochote kinachoendelea. Alikuwa amepoteza fahamu na hakuwa na uwezo wa kusikia chochote. 
Wasiwasi wa Cleopatra ulikuwa mmoja tu; kwamba Deo akifa asingeweza tena kufunga naye ndoa, tendo ambalo alikuwa akilisubiria kwa muda mrefu sana. Cleopatra akazidi kulia. Alitamani sana kuliona tabasamu la Deo.
Alitaka kuona akizungumza. Akimbusu. Akimkumbatia na kumwambia maneno matamu ambayo amekuwa akimwambia kila wakati. 
Hayo tu!
Lakini Deo hakuweza kufanya chochote kati ya hayo. Alikuwa amelala kitandani kama mzigo, hana taarifa kama mpenzi wake Cleopatra aliyekuwa kitandani kwake akilia.
“Basi dada yangu, mwache apumzike, usijali, huna sababu ya kulia. Atapona tu!”
“Lakini inaniuma dokta, bado wiki tatu tufunge ndoa. Tayari ndoa imeshatangazwa mara ya kwanza kanisani, bado mara mbili ili nifunge ndoa na Deo wangu, sasa itawezekanaje tena? Si ndiyo nimeshampoteza? Si tayari nimeshapoteza ndoa?” Cleopatra akasema akionekana kuwa na uchungu sana.
“Hapana, hana hali mbaya, wiki tatu ni nyingi sana, kabla ya muda huo atakuwa amesharejea katika hali yake ya kawaida, bila shaka atapanda madhabahuni kufunga ndoa na wewe!”
Maneno ya Dk. Pallangyo kidogo yalimpa moyo Cleoptara, lakini ndani ya moyoni mwake aliendelea kuwa na uchungu mwingi, kwani Deo alikuwa kila kitu katika maisha yake. Yeye ndiye aliyekuwa wa kutimiza ndoto zake za kuingia kwenye ndoa, lakini sasa zinakaribia kuzimika!
Lazima aumie!
Lazima ateseke!
Akiwa katika mawazo ya kumuumiza moyo, simu yake ikaita. Akaangalia jina la mpigaji akakutana na jina lililoandikwa ‘My Mumy’. Alikuwa ni mama yake mzazi akimpigia. 
Kwa muda akaiangalia ile simu akijishauri kupokea, lakini alisita.
Alijua sababu ya simu ya mama yake, kwa vyovyote vile, angetaka kujua kuhusu Deo, jambo ambalo aliamini lingeweza kuamsha machozi upya, kitu ambacho hakutaka kabisa kitokee. Lakini baadaye akaamua kupokea...
“Patra uko wapi?” ndiyo neno alilokutana nalo baada ya kupokea simu ya mama yake.
“Hospitalini!”
“Upo sehemu gani, maana na mimi tayari nimeshafika hapa Muhimbili!”
“Nipo huku Kibasila, Ward 11 mama!”
“Nakuja!”
Muda mfupi baadaye, mama yake akatokea. Cleopatra alipokutanisha uso na mama yake, machozi kama maji yakaanza kumwagika machoni mwake. Akamkimbilia na kumkumbatia.
“Mama Deo wangu anakufa mama...” akasema kwa hisia za uchungu sana.
“Hapana mwanangu, hutakiwi kuwaza hayo mama...yupo wapi?”
“Wodini!”
“Twende...”
“Hawaruhusu kwenda sasa hivi, muda wa kuwaona wagonjwa umepita!”
“Tatizo ni nini hasa lakini?”
“Amepigwa risasi!”
“Na nani?”
“Hawajulikani mama.”
“Wapi?”
“Mjini. Daktari anasema aliletwa na wasamaria wema baada ya kumuokoa!”
“Masikini, ana hali mbaya sana?”
“Haongei mama, amepigwa risasi ya bega, lakini dokta anasema imekuwa vizuri maana haijatokeza upande wa pili.”
“Mungu ni mwema mwanangu.”
“Namuomba sana amponye ili tufunge ndoa yetu kwanza.”
“Sote ndiyo dua yetu!”
Kwakuwa muda ulikuwa umeshapita wakaondoka kwa ahadi ya kurudi jioni kumuona.
***
Saa 11:00 jioni, Cleopatra na mama yake walikuwa wanaingia katika wodi aliyolazwa Deo. Hawakuamini walipofika kitandani mwake na kumuona akiwa amefumbua macho yake. Cleopatra akalia kwa furaha.
“Pole sana sweetie!”
“Ahsante!” Deo akajibu kwa sauti ya taratibu sana.
“Shikamoo mama...” Deo akasalimia.
“Marhaba mwanangu, pole sana!”
“Ahsante mama!”
“Ilikuwaje?” Cleopatra akauliza akiketi kitandani kwa Deo.
“Hata sielewi, nakumbuka nilikuwa kwenye lifti, nilipofika ghorofa ya tatu lifti ikasimama, wakaingia wanaume watatu, tukaanza tena kushuka hadi ghorofa ya pili, ikasimama tena. Ghafla nikasukumwa nje, kilichofuata ilikuwa ni mlio wa risasi.
“Nikashtuka sana na kupoteza fahamu. Nilipozinduka, nikajikuta nipo hapa hospitalini.”
“Unaweza kumkumbuka kwa sura hata mmoja wao?”
“Hapana.”
“Pole sana, lakini unajisikiaje sasa?”
“Siwezi kujielezea, nahisi maumvu ya mkono na bega, lakini sielewi hali yangu hasa!”
“Pole sana, utapona usijali,” mama yake Cleopatra akasema.
“Nashukuru sana mama.”
Cleopatra akamlisha chakula huku akimwambia maneno matamu ya kumtia moyo! Kidogo Deo akaanza kujisikia vizuri baada ya kupata faraja kutoka kwa mpenzi wake. Muda wa kuwaona wagonjwa ulipoisha wakaondoka zao.
“Ugua pole dear, kesho asubuhi nitakuja kukuona.”
“Ahsante sana mpenzi wangu, nakupenda sana. Ahsante kwa kujali kwako!”
“Ni wajibu wangu...utapenda kula chakula gani asubuhi?”
“Chochote tu baby!”
“Chagua mwenyewe mpenzi wangu!”
“Nadhani mtori utanifaa zaidi.”
“Ok! lala salama, ugua pole, you will be okay!”
“Thank you baby!”
Cleopatra na mama yake wakaondoka, wakamuacha Deo akiwa ametulia kimya kitandani, akisikilizia maumivu yake ya bega. Mpaka wakati huo, hakuelewa ni kwa nini watu wale walimpiga risasi, maana hakuwa na fedha na wala hawakumwibia! Hilo liliendelea kuzunguka kichwani mwake bila kupata majibu.
***
Anahisi kama ameguswa na mkono wa mtu, anajaribu kuyafumbua macho yake kwa shida kidogo kutokana na mzigo wa usingizi aliokuwa nao! Alilala sana siku hiyo. Uchovu na usingizi ulisababishwa na mambo mawili; alikuwa hajalala usiku mzima kwa maumivu ya bega, ndiyo kwanza asubuhi hiyo alianza kuhisi usingizi.
Dawa alizokunywa, zilikuwa kali na zilimchosha sana mwili wake. Hayo yalitosha kabisa kumfanya, saa moja hii ya asubuhi, macho yake yaendelee kuwa mazito. Anajaribu kuyafumbua kwa shida na kumtazama mtu huyo!
Akashtuka sana!
Hakutegemea kukutana na sura hii hospitalini. Nani amemwambia kwamba amelazwa? Ni jana tu, alipata matatizo, leo hii amejuaje? Nani amempa taarifa za yeye kuumwa? Yalikuwa maswali yaliyofumuka mfululizo kichwani mwake, bila kupata majibu stahiki!
Anazidi kumwangalia mwanamke huyu ambaye naye amesimama kama ameganda...
“Pole Deogratius...pole sana kwa matatizo!” mwanamke huyo akatamka kwa sauti ya taratibu sana.
Deo hakuitika!
“Masikini Deo, najua ni kiasi gani unaumia, najua kwamba ni jinsi gani ndoa yako itakavyokuwa na ngumu kufungwa. Bila shaka mmebakiza wiki tatu tu, sidhani kama utaweza kupanda madhabahuni ukiwa katika hali hii...pole sana...ni majaribu tu ya shetani,” akatamka kwa yakini, akiongea kwa mpangilio mzuri sana.
Deo hakujibu neno!
Je, mwanamke huyo ni nani? Kwa nini amefika hapo hospitalini na Deo hamjibu kitu? Kuna nini kati yao? Usikose kufuatilia Jumapili ijayo.