TAFUTA HAPA

Hadithi mpya: Moyo wangu 3

YALIKUWA maajabu ya aina yake. Deo hakutegemea kabisa kumuona mwanamke huyo mbele yake. Alihisi kama haoni sawasawa...
“Huyu vipi? Amejuaje nipo hapa? Amejuaje natarajia kufunga ndoa? Amejuaje mambo yangu?...amejuaje?” akazidi kujiuliza lakini majibu hakuwa nayo.
“Nakupa pole huitiki kwa nini? Au hujapenda mimi kuja hapa?” mwanamke yule akauliza, akionekana kusononeka na mapokeo ya Deo.
Kwa ghafla sana, macho ya Deo yakaanza kupatwa na unyevunyevu, baadaye machozi yakaanza kuchuruzika machoni mwake. 
Ubongo wake ukasafiri miaka kumi nyuma. Akayatupa macho yake juu ya dari, kisha kumbukumbu zote za maisha yake yaliyopita zikaanza kumjia kama anatazama sinema ya kusisimua...
Sinema ya maisha yenye kila aina ya machafuko na mataabiko. Mateso, dhiki na kuonewa. Masimango, kutukanwa na kudhalilishwa! 
Ilikuwa sinema mbaya, lakini yenye mwisho mzuri wa kupendeza, mwisho ambao baadaye uliingia shubiri.
Ikawa chungu!
Sinema ikaanza...
***
Oktoba 22, 1999 – Dar es Salaam
Ni siku nyingine ya pilikapilika, kama ilivyokuwa kwa siku zilizotangulia, leo pia Deo ameamka saa 11:00 alfajiri kama kawaida yake. Alipoamka kitu cha kwanza kufanya ni kumwagilia maua, kufanya usafi wa mazingira na kuwapeleka watoto shule.
Aliporudi, alitoka nyumbani kwa bosi wake Mburahati, akaenda sokoni Tandale, kilometa zaidi ya kumi na tano kwa miguu. Hapo ndipo anapofanya kazi ya kuuza mchele hadi saa 11:00 jioni, anapoanza safari nyingine ya kurudi nyumbani kwa miguu. 
Siku yake humalizika kwa kufunga mifuko ya barafu hadi saa sita za usiku anapopata muda wa kupumzika, kabla ya kukurupushwa tena alfajiri inayofuata.
Hayo ndiyo maisha yake!
Deogratius Mgana, kijana mchapakazi, hajawahi kupumzika hata siku moja tangu ameanza kazi katika nyumba ya mzee Maneno miaka mitatu iliyopita. 
Alikuja Dar es Salaam, akitokea nyumbani kwao Kiomboi, Singida kwa lengo moja tu; kutafuta maisha. 
Mshahara wake ukiwa ni shingili elfu arobaini na tano tu, kwa kazi zote anazofanya.
Akiwa ametulia kwenye ubao wake sokoni, anatokea dada mmoja mrembo sana. Si mgeni machoni mwake, ni mteja wake wa kila siku, ambaye amekuwa akimhudumia mchele karibu mara mbili au tatu kwa wiki!
“Mambo kaka?” dada yule akamsalimia.
“Poa, karibu!”
“Ahsante, nipimie kilo tano!”
“Usijali!”
Deo akampimia mchele aliohitaji na kumwekea kwenye mfuko, kisha akampa. Yule msichana akalipa na kuondoka, baada ya hatua nne, akarudi tena.
“Samahani kaka, nimeshakuwa mteja wako wa kudumu sasa, nadhani ni vizuri kujua jina lako. Mimi naitwa Levina, wewe je?” 
“Deogratius, lakini wengi wanapenda kuniita Deo!”
“Nashukuru kukufahamu, sasa nimeridhika, kwaheri!”
“Poa!”
Deo alimwangalia Levina hadi alivyoishia, namna alivyokuwa akitembea, namna alivyokuwa akiozungumza vilimpa picha ya tofauti kabisa. Alianza kuhisi eti huenda Levina anampenda, lakini alijishangaa, maana lilikuwa jambo gumu kidogo!
Levina ampende yeye?
Muuza mchele? 
Mbona alikuwa anawaza mambo makubwa sana? Lakini bado hakutaka kuuhakikishia ubongo wake moja kwa moja juu ya hilo. Aliamini kwamba lazima kulikuwa na kitu kinachoendelea. Kwa nini atake kujua jina lake? Ana umuhimu gani hasa? 
“Au zali la mentali nini? Si kawaida mteja kutaka kujua jina langu bila sababu za msingi. Lazima kuna kitu kinaendelea, lazima....” akawaza Deo akiwa anamwangalia mpaka anavyoishia mbali.
Akabaki akiwa na mawazo mengi kichwani mwake, tayari hisia za mapenzi dhidi ya Levina zilianza kumwingia, lakini aliwaza sana namna ya kumwingia, hakuwa na hadhi ya kutoka na Levina.
***
“Mambo Deo?”
“Poa Levina, mzima?”
“Nipo poa!”
“Za nyumbani?”
“Salama kabisa.”
“Ngapi leo?”
“Pima kilo kumi!”
“Kwani mna sherehe?”
“Hapana ni bajeti tu!”
Deo akapima mchele alioagizwa, akamimina kwenye mfuko na kumkabidhi Levina, aliyeupokea huku akiachia tabasamu mwanana kabisa. 
“Ahsante sana Deo!”
“Nashukuru pia!”
“Samahani Deo, naweza kupata namba zako za simu?” Levina akamwuliza.
“Simu?”
“Ndiyo!”
“Mimi sina, labda nikupe namba za nyumbani!”
“Hapana, nataka namba zako mwenyewe!”
“Sina.”
“Kwa nini?”
“Maisha Levina!”
“Ok! basi chukua zangu...ukimaliza kazi zako nipigie kwenye kibanda cha simu, nahitaji kuzungumza na wewe!” Levina akasema akiandika namba na kumkabidhi Deo akiambatanisha na noti ya elfu tano.
“Ahsante sana Levina, nitakupigia!”
“Usiache tafadhali, ni muhimu sana!”
“Sawa.”
Deo alibaki na maswali mengi sana kichwani mwake bila kuwa na majibu, bado kitu kikubwa kilichokuwa kinamsumbua ni kwamba, ni kweli hisia zake zilikuwa sawa kwamba Levina alikuwa anampenda au zilikuwa hisia zake mwenyewe?
Hakujua hakika!
Lilikuwa suala gumu sana kichwani mwake kupitishwa moja kwa moja kuwa Levina alikuwa anampenda, hata hivyo ndani ya moyo wake alijua wazi kuwa kabisa yeye alimpenda sana Levina.
“Nitampataje jamani huyu msichana? Nahisi kabisa moyo wangu unaniambia kuna kitu fulani, ni kweli nampenda sana Levina,” akawaza Deo.
Siku nzima alishinda akiwa na mawazo, alitamani sana kumpigia simu Levina ili amsikilize alichokuwa akitaka kumwambia lakini kwa sababu alikuwa na wateja wengi alishindwa kufanya hivyo, lakini kubwa zaidi kelele za pale sokoni zilimfanya ashindwe kumpigia kwa kuwa alifahamu kwamba hawataweza kuelewana vizuri!
Alitamani hata kuazima simu ya mtu ili aweke vocha ampigie lakini bado alikuwa na shaka moyoni. Hakutaka mtu yeyote aijue namba ya Levina. Alihisi angeibiwa!
“Mi nafikiri mahali salama ni kwenye kibanda cha simu tu,” akawaza Deo.
Wakati huo bado huduma ya simu ilikuwa kwenye chati, ilikuwa wamiliki wa simu ni wachache sana kuliko ilivyo katika maisha ya sasa.
Jioni alifunga biashara yake na kuanza kurudi zake nyumbani, kwa kuwa alipewa pesa na Levina na pia alikuwa na haraka ya kuwahi kumpigia simu, akaona bora apande daladala.
Akachepuka kutoka sokoni Tandale hadi Manzese - Agerntina, pale akapanda daladala lililompeleka mpaka Magomeni - Mwembechai, akashuka na kutafuta kibanda cha simu.
“Habari yako dada?” Deo akamsalimia mhudumu wa kibanda cha simu.
“Salama, karibu kaka’ngu!”
“Nahitaji kupiga simu.”
“Sawa, naomba namba.”
Deo akamtajia.
Yule dada akabonyeza zile namba kwenye simu na kumpatia Deo simu.
“Haloo...” sauti laini ya kike ilisikika upande wa pili, baada ya kupokelewa.
“Haloo habari yako?”
“Nzuri, bila shaka ni Deo?”
“Umejuaje?”
“Kwanza sauti yako, lakini pia wengi wanaonipigia simu namba zao ninazo kwenye simu yangu!”
“Niambie Levina.”
“Poa!”
“Nimekupigia kama ulivyoniambia.”
“Hujakosea kitu Deo, tena umefanya vizuri sana, maana nilikuwa nawaza namna ya kukupata kama usingenipigia.”
“Sawasawa...nini kipya?” Deo akauliza.
Kimsingi hakuonekana kuwa na jambo lolote la kuzungumza zaidi ya kusubiri kumsikiliza Levina.
“Sikia Deo, kuna kitu cha muhimu sana nilitaka kuzungumza na wewe, lakini naona kama mazingira hayafanani kabisa.”
“Kivipi?”
“Nahisi upo kwenye kelele sana, kiasi kwamba hata hutakuwa na usikilizaji na uelewa mzuri wa nitakayokuambia.”
“Kwani unataka kuniambia nini?”
“Subiri Deo, usiwe na haraka kiasi hicho, huwezi kupata muda nikazungumza na wewe nje ya kazini kwako?”
“Kama lini?”
“Wewe unapumzika lini?”
“Jumapili, ingawa si mapumziko ya moja kwa moja!”
“Kivipi?”
“Huwa siendi sokoni, lakini kazi nyingine za nyumbani zinaendelea kama kawaida.”
“Sasa?”
“Naweza kujaribu kutoka mara moja, lini unataka tuonane?”
“Itakuwa Jumapili, lakini kesho nitakuja tena kuzungumza na wewe zaidi!”
“Sawa.”
“Haya usiku mwema mwaya Deo!”
“Ahsante, nawe pia ulale salama.”
Wakakata simu zao.
Deo akalipa na kuanza kutembea kwa miguu akienda Mburahati, nyumbani kwa bosi wake. Ndani ya moyo wake alijihakikishia kumpenda Levina, lakini ufukara wake ulimfanya ashindwe kuelewa namna ambavyo angeweza kumfanya Levina awe wake wa maisha!

Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia Jumapili.