MOYO WANGU-1
HANA haraka anapotembea, ukimtazama anaonekana kujiamini sana. Tabasamu mwanana linaupamba uso wake lakini mavazi yake yanaonyesha asivyo mtu wa dhiki!
Hata kama siyo sana lakini uwezo wa kubadilisha mboga ulikuwa mikononi mwake!
Anatoka kwenye duka hili maalumu kwa kuuza kadi na zawadi mbalimbali lililopo ghorofa ya saba, katika Jengo la KPC Towers, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Anatembea taratibu kuifuata lifti iliyokuwa mita chache mbele yake.
Anatabasamu!
Ni kweli anatabasamu!
Tena basi alikuwa na kila sababu ya kutabasamu, maana zilibaki wiki tatu tu, kabla ya ndoa yake na mpenzi wake wa siku nyingi Cleopatra.
Mkononi mwake ana bahasha ya khaki ambayo ndani yake kuna zawadi kwa ajili ya Cleopatra wake. Alijua anachotakiwa kumfanyia Cleopatra!
Siku zote alikuwa akinunua apple tu, mambo yanakuwa sawa! Huo ulikuwa ugonjwa mkubwa zaidi kwa Cleopatra.
Alipoifikia lifti, alibonyeza kitufe mlangoni, mlango ukafunguka. Akaingia na kusimama, punde mlango ukajifunga, akabonyeza kwenye herufi G akimaanisha kwamba anataka kushuka chini!
Ni kijana mtanashati sana, anayevutia kwa kila mwanamke aliyekamilika. Anaitwa Deogratius Mgana. Mfanyakazi wa shirika moja lisilo la kiserikali jijini Dar es Salaam.
Ana furaha moyoni mwake, maana anakwenda kufunga ndoa na chaguo la moyo wake.
Kwa nini asitabasamu?
Hakika ana haki ya kutabasamu!
Ni kweli lazima nitabasamu, kwanza nusu ya ndoto zangu tayari zipo kwenye mstari. Lazima nijisikie vizuri, akawaza mwenyewe akiwa kwenye lifti.
Akabaki ametulia kimya akiwa amesimama kwenye lifti ile, ikaanza kushuka taratibu kwenda chini. Ghorofa ya sita, ghorofa ya tano, ghorofa ya nne...alipofika ghorofa ya tatu, lifti ikasimama. Hapo akajua kuna mtu aliyekuwa akitaka kushuka chini. Mlango ulipofunguka, wakaingia wanaume watatu, wote wamevaa miwani ya jua.
Mambo bro? mmoja akamsalimia.
Poa, akaitikia Deo.
Lifti ikaanza kushuka taratibu, walipofika ghorofa ya pili, ikasimama. Mlango ulipofunguka tu, ghafla wale vijana watatu wakamsukuma hadi nje. Mara mlango ukafunga.
Paaaaaa! mlio wa risasi ukasikika.
Deo akaanguka chini, akaanza kuvuja damu!
***
Alisikia vizuri sana mlio wa simu yake lakini aliamua kupuuzia! Si kwamba hakutaka kwenda kupokea, lakini alikuwa na kazi muhimu sana aliyokuwa akiifanya, zaidi ya kwenda kupokea simu!
Cleopatra alikuwa anapika!
Chakula kizuri ambacho mpenzi wake alikuwa anakipenda sana. Alikuwa anapika viazi vya kukausha, maarufu kama maparage, ambayo Deo alikuwa akiyapenda sana. Siku hiyo Deo alipanga kwenda nyumbani kwa kina Cleopatra, Mikocheni.
Ilikuwa zimebaki wiki tatu tu ndoa yake na Deo ifungwe. Siku ambayo alikuwa akiitamani sana na kuomba ifike haraka.
Mlio wa simu yake ukakatika ghafla. Akaendelea na mapishi yake jikoni lakini baada ya muda mfupi simu ikaita tena kwa mara nyingine...
Nani huyo aaah! Cleopatra akasema kwa hasira kidogo.
Mi nampikia Deo wangu bwana alaaah! akatamka tena, akifunika kile chakula jikoni na kufunga khanga vizuri kiunoni kwake.
Yap! Kama ungekuwepo, ungeamini kweli Cleopatra alikuwa mwanamke mrembo. Pamoja na kwamba alikuwa amevaa khanga, lakini umbo lake lenye namba nane liliweza kuonekana vyema kabisa. Cleopatra alijaaliwa umbo zuri la kuvutia.
Ona anavyotembea...
Kama anaonea huruma ardhi! Ana hips pana zinazozidisha uzuri wake, ana macho mazuri yenye uwezo wa kumchanganya mwanaume yeyote yule. Labda niseme kwamba, Cleopatra alikuwa mwanamke mrembo sana.
Alivyofika sebuleni, simu ikaacha kuita. Akachukia sana, lakini akiwa anainua ili aweze kujua aliyekuwa akimpigia ili aweze kumpigia tena, akashangaa simu yake ikianza kuita tena.
Kwenye kioo cha simu yake likaonekana jina My Deo!
Jamani, kumbe ni sweetie! akasema akipokea ili kumsikiliza.
Ilikuwa ni namba ya Deo ikionekana kwenye kioo cha simu yake...
Yes baby, najua hujasahau kuninunulia apple na napenda kukujulisha kwamba, maparage yako yanakaribia kuiva ila sijui ungependa nikuandalie juice ya nini? Machungwa, maparachichi, maembe au mananasi? Maana kila kitu kipo kwenye friji! Cleopatra akasema kwa sauti iliyojaa mahaba mazito.
Samahani dada, mimi siyo mwenye simu! sauti hii ya kiume, tulivu yenye mikwaruzo kwa mbali ilisikika kwenye simu ya Cleopatra.
Sasa kama wewe si mwenye simu, kwa nini umepiga? Kwa nini unakosa ustaarabu? Cleopatra akamwuliza yule mtu akiwa na hasira.
Samahani sana dadangu, lakini nadhani ni vyema ukawa mtulivu na kuuliza kilichotokea. Si kawaida mtu kupiga simu isiyo yake kwa watu ambao wamehifadhiwa kwenye simu hiyo. Hiyo ingetosha kabisa kukufaya ugundue kwamba kuna tatizo! mtu huyo akasema akizidi kuonesha kwamba anahitaji utulivu wa Cleopatra.
Ndiyo...enhee kuna nini? Hebu niambie, maana tayari nahisi nimeanza kuchanganyikiwa!
Sina shaka wewe ndiye Cleopatra!
Ndiyo!
Ni nani wako?
Ni mchumbangu, kwani vipi?
Usijali, tuliza moyo dada yangu. Mimi ni Dk. Palangyo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Huyu ndugu mwenye simu, ameletwa hapa na wasamaria wema, baada ya kupitishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay!
Anaumwa na nini dokta? Cleopatra akauliza akianza kulia kwa huzuni.
Amepigwa risasi na watu wasiojulikana katika Jengo la KPC Towers. Hata hivyo, hana hali mbaya sana, matibabu yanaendelea lakini nimeona ni vyema kukujulisha ili uwafahamishe ndugu wengine!
Ahsante dokta kwa taarifa, baada ya nusu saa nitakuwa hapo, Cleopatra akajibu akizidisha kilio chake.
Akatoka mbio, hadi chumbani kwake. Hakukumbuka kwenda kuipua chakula jikoni. Akavaa haraka na kutoka hadi getini! Ghafla kumbukumbu zake zikarudi!
Mama yangu, nimeacha chakula jikoni na jiko linawaka, akawaza akirudi ndani mbio.
Ilikuwa ni hatari sana, maana alikuwa anapikia jiko la umeme. Mara moja akarudi ndani na kuzima jiko, akaipua kile chakula na kutoka kwa kasi sana.
Wewe vipi mwenzetu, mbona hivyo? mama yake akamwuliza baada ya kumwona mwanaye anaonekana kuwa na haraka ambayo hakujua ni ya nini.
Nitakupigia simu mama!
Unakwenda wapi?
Mama nitakupigia!
Patra, mwenzako si anakuja au haji tena?
Mama Deo amepigwa risasi, yupo hospitalini, akasema Cleopatra akiwa tayari ameshaingia kwenye gari.
Akapiga honi kwa nguvu, mlinzi akafungua geti haraka. Cleopatra akaondoa gari kwa kasi sana. Alikuwa anakwenda Muhimbili, huku nyuma akiwa amemwacha mama yake mwenye mawazo sana.
***
Cleopatra aliendesha gari kwa kasi , hakujali ajali barabarani, alikuwa tayari kwa lolote litakalotokea! Aliendesha kwa kasi ya ajabu sana. Kutokea nyumbani kwao Mikocheni hadi Muhimbili, alitumia dakika ishirini!
Hakukubali kukaa foleni, aliendesha kama daladala, kwani alipenyeza pembeni, sehemu zilizokuwa na foleni kubwa. Alipofika hospitalini, akaegesha gari lake kisha akapiga kwenye simu ya Deo na kuzungumza na yule daktari.
Nimeshafika dokta!
Ok! Uko wapi?
Kwenye maegesho!
Tukutane Kibasila!
Sawa dokta.
Bila kupoteza muda, Cleopatra akachanganya miguu hadi liilipo Jengo la Kibasila. Akiwa kwenye lango kuu la kuingilia, akamwona mwanaume mmoja mrefu aliyevaa koti jeupe na miwani, akahisi angekuwa ndiye daktari aliyekuwa akimfuata.
Sorry, ni Dk. Pallangyo? Cleopatra akauliza akimkazia macho.
Yes, karibu!
Ahsante!
Nifuate!
Dk. Pallangyo akatangulia na Cleopatra akimfuata nyuma. Safari yao ikaishia ofisini kwa daktari yule iliyokuwa nje ya Jengo la Kibasila.
Karibu sana dada yangu!
Ahsante! Cleopatra akajibu na kuketi kwenye kiti, kwa mtindo wa kutazamana na daktari.
Ulisema mgonjwa ni nani wako?
Mchumba wangu!
Oh! pole sana...kilichotokea ni kwamba, mwenzio amepigwa risasi ya begani, lakini inaonekana kutokana na mshtuko alioupata, umesababisha apoteze fahamu. Tunashukuru kwamba risasi haijatokeza upande wa pili, kwa hiyo tumefanikiwa kuitoa, lakini bado hajazinduka!
Mungu wangu, atapona kweli?
Uwezekano huo ni mkubwa sana lakini yafaa tuombe Mungu, naamini atakuwa sawa.
Naweza kwenda kumwona tafadhali?
Bila shaka! Dokta akamjibu na kusimama.
Akaonesha ishara kwamba Cleopatra amfuate. Akasimama na kumfuata nyuma yake.
Je, Deo amepigwa risasi na nani? Kwa nini wamempiga risasi? Ili kujua kisa na mwendelezo kamili wa simulizi hii, usikose kufuatilia Jumapili ijayo.