TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA 18

Watu wengi walifurika nje ya hoteli ya Lubumbashi asubuhi ya siku iliyofuata, kila mtu akizihitaji milioni mbili zilizotangazwa, kwa kuwaangalia tu watu waliofika bila hata kuuliza ungejua walikuwa ni wavuvi na walizidi kuongezeka kadri saa zilivyozidi kusogea.
“Mnataka kumwona nani?” Mtu wa mapokezi aliwauliza.
“Yule aliyetangaza kutafutiwa ndugu zake!”
“Subirini” Aliwajibu kisha kunyenyua simu na kupiga namba ya chumbani kwa mzee Katobe, dakika mbili tu baadaye mzee Katobe alikuwa mapokezi na kuomba chumba kimoja afanye maongezi na watu waliojitokeza, alipewa chumba kimoja na Danny aliungana naye dakika chache baadaye.
Katika muda wa masaa mawili alishawasikiliza watu wote lakini ni wawili tu kati yao walioonekana kuwa na maelezo ya kusaidia, yote yalikuwa ya kusikitisha yaliyomfanya Danny alie machozi.
“Kwanza alikuja huyu msichana!” Aliongea kijana mmoja akionyesha kidole chake kwenye picha.
“Endelea!”
“Alikuwa amekonda sana na alionekana kuwa na mawazo mengi. Alinikuta mimi na wenzangu ufukweni tukitengeneza nyavu zetu akatuuliza habari za usafiri kwenda Zaire, bahati mbaya hapakuwa na meli likapatikana jahazi akapanda na kuondoka zake! Siku iliyofuata akaja huyu mama akimuulizia naye alinikuta mimi ilikuwa kama bahati nikamwambia kila kitu, akataka kusafiri kumfuatilia!”
“Alikueleza ni kwa nini?”
“Hakuniambia”
“Alisafiri kwa usafiri gani”
“Nilimpeleka kwa wale Waarabu wenye boti za kukodi!”
“Akakodisha moja na kuondoka”
“Unaweza kutupeleka kwa hao Waarabu?”
“Hakika, labda tu wagome kusema ukweli”
Hawakutaka kupoteza muda maelezo waliopewa yalitosheleza kabisa. Ni kweli kijana huyo aliwaona Nancy na mama yake, walichofanya ni kuondoka pamoja na kijana huyo kwenda ofisini kwa wakodishaji wa vyombo vya majini, huko walikutana na nahodha aliyemsafirisha mama Nancy hadi katikati ya ziwa Tanganyika.
“Ziwa lilikuwa chafu mno wakati nawaacha ilikuwa mara ya kwanza mimi kukutana na hali ya namna hiyo katika ziwa Tanganyika ! Sikutegemea kurudi hapa salama, nilipofika tu nchi kavu nilisikia katika vyombo vya habari kuwa jahazi alilopanda lilizama na watu wote wakafa maji !”
Mzee Katobe na Danny waliangua kilio. Watu waliokuwepo wakaanza kuwabembeleza na kuwafariji, haikusaidia ilibidi wakodishe gari hadi hotelini ambako waliendelea kulia. Pamoja na kushindwa kuwapata watu waliokuwa wakiwatafuta wakiwa hai, mzee Katobe aliwalipa kijana aliyewapa habari mara ya kwanza pamoja na nahodha shilingi milioni moja kila mmoja wao.
“Sikubali, lazima walizikwa mahali fulani, nitazitafuta maiti zao mpaka nizipate nikawazike Bagamoyo kwa heshima zote!” Alisema mzee Katobe akilia, yeye na Danny walikuwa wamekumbatiana! Pigo walilopata lilikuwa kubwa mno kuvumilia.
“Itabidi tukodishe boti kwenye ile kampuni tuzunguke fukwe zote lazima tutafika mahali ambapo maiti zilionekana na zikazikwa!”
“Sawa!” Danny aliitikia. Walikesha wakilia na hicho ndicho kilifanyika siku iliyofuata, walirudi kwenye kampuni ya boti na kukodisha boti kubwa yenye uwezo wa kwenda kwa kasi kubwa zaidi na kuanza kuzunguka fukwe za ziwa Tanganyika wakianzia upande wa Kigoma kisha kwenda upande wa pili wa Zaire lakini hawakufanikiwa kupata taarifa za miili hiyo.
“Tutafanyaje sasa!” Aliuliza mzee Katobe baada ya wiki tatu za kutafuta, pesa nyingi zilitumika katika operasheni hiyo.
“Labda tujaribu katika visiwa!” Nahodha aliyejulikana kwa jina la Costa aliwashauri. “Sawa niko tayari kwa lolote, zoezi hili halitakoma mpaka nifanikiwe kupata miili ya mke na mtoto wangu hata kama itachukua mwaka mzima” Aliongea mzee Katobe, walikuwa na uhakika asilimia mia moja Nancy na mama yake walishafariki dunia.
****
Kelele alizozipiga Nancy baada ya kumwona mnyama wa kutisha aliyeamini ni shetani aliyekuja kuchukua roho yake ndizo zilikuwa za mwisho, alipoteza fahamu kabisa baada ya hapo! Hakuelewa kitu chochote kilichoendelea.
Alizinduka baadaye akiwa amelala ndani ya kibanda kidogo cha nyasi, kilichokuwa na giza nene.
Hakuelewa alikuwa wapi na alikuwa akifanya nini, mahali alipolala palikuwa pa baridi na hapakuwa na godoro wala shuka, alipofumbua macho yake taratibu na kuangalia ingawa kwa pembeni alimwona mzee mwenye mwili mkubwa na ndevu nyingi akiwa amepiga magoti pembeni mwake akitikisa kitu kama kibuyu.
Alishindwa kuelewa mzee huyo aliyetisha alikuwa nani, hakuwa na kumbukumbu zozote kichwani juu ya kilichotokea. Wakati akihangaika kuvuta kumbukumbu zake alisikia kipande kirefu cha mti kikipenya mdomoni na sekunde chache baadaye alistukia kitu kichungu kikimwingia mdomoni kupitia katika kipande hicho cha mti.
“Meza! Meza dawa, imekusaidia, bila hii ungekufa !” Aliongea mzee huyo kwa sauti ya kukwaruza.
Nancy alitii sauti na kumeza majimaji yaliokuwa mdomoni mwake, yalikuwa kama shubiri, yalipomwingia tumboni michango iliunguruma akasikia nguvu kidogo zikirejea na kumbukumbu zake zikamiminika kama filamu, alijiona yu katikati ya maji akihangaika kisha akashuhudia mama yake akiachia mkungu wa ndizi na kuzama.
“Mamaaaa ! Mama yanguuuu !” Nancy alilia.
“Usilie mama yako yupo.”
Alinyanyuka na kuketi kitako katika hali ya kutoamini, mzee huyo aliendelea kumhakikishia kuwa mama yake alikuwa hai! Nancy hakuamini alitaka kumwona mama yake kwa macho, halikuwa jambo rahisi kukubali.
“Subiri kwanza !”
“Wewe ni nani?”
“Naitwa babu Ayubu!”
“Ilikuwaje nikafika hapa?”
“Siku mlipotaka kuzama, mimi na mwenzangu tulikuwa jirani na eneo hilo, tukawawahi na kuwaokoa tukaja nanyi hapa kisiwani leo ni siku ya tano!”
“Unasema ukweli? mama yangu yuko hai?”
“Hakika!tena yeye amewahi kupata nguvu mapema kuliko wewe! ndiye aliyetupikia chakula leo mchana”
“Babu Ayubu unanitania!”
“Sina sababu ya kukueleza uongo”
“Yuko wapi ?”
“Kwenye kibanda cha mwenzangu! Tulipowaokoa tulifurahi sana, kwani leo ni miaka kumi na tano tangu tufike hapa kisiwani, hatujawahi kukutana na mwanamke kimwili!” Ndiyo maana tumejitahidi sana kuwaokoa maisha yenu kwa sababu mtakuwa wake zetu! mwenzangu amekwisha kumuoa mama yako, mimi nilikuwa nakusubiri !”
“Unasema nini? nahisi umechanganyikiwa, ni heri ungeniacha nikafa majini kuliko kuniokoa halafu unifanyie unachotaka kukifanya!”
“Utakubali tu! mbona hata mama yako alikataa, mateso aliyoyapata hatayasahau, kwa mdomo wake mwenyewe alijikuta akisema ndiyo!” Aliongea babu Ayubu, hasira ilisikika katika sauti yake.
“Ninasema haiwezekani, niliishakula kiapo cha kutofanya map....!”
“Weweee! kiapo chako huko huko hapa ni serikali nyingine na hakuna kituo cha polisi, ulishawahi kuona kisiwa kikubwa kama Zanzibar wanaishi watu wawili? basi ndiyo hapa!”

Je nini kitaendelea?