TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA 17

Danny hakusema kitu tena alichofanya ni kuingia bafuni ambako hakuchukua dakika tano akawa ametoka na kuvaa nguo zake vizuri na wote wakaondoka hadi stendi ambako walipanda basi liitwalo Bagamoyo Tours lililowafikisha jijini Dar es Salaam masaa matatu baadaye, kwa sababu ya ubovu wa barabara. Hakuna kazi nyingine waliyokuwa nayo jijini zaidi ya kutafuta tiketi za ndege, hawakufanikiwa kupata baada ya kuambiwa hapakuwa na ndege ya kwenda Kigoma kwa wiki nzima. Chaguo la pili ilikuwa ni treni hilo halikuwahangaisha sana, walipata tiketi daraja la kwanza na siku hiyohiyo kuondoka wakitegemea kuingia Kigoma siku mbili baadaye.
“Tutafika tu! Hata kama itachukua siku ngapi?” Aliongea mzee Katobe.
“Lazima tuwapate, nitafurahi sana kumwona Nancy ingawa ndoto yangu ya leo imenikatisha tamaa sana!”
“Hivi ni ndoto gani?”
Danny alieleza kila kitu juu ya ndoto yake na mzee Katobe akamwondolea wasiwasi na kumhakikishia kila kitu walichopanga kingekwenda sawa sawa, aliongea bila kuelewa nini kiliwapata Nancy na mama yake majini.
Safari kutoka Dar Es Salaam hadi Kigoma kwa treni ilikuwa ni ya kuchosha, ilikuwa safari ndefu kuliko zote ambazo Danny aliwahi kusafiri katika maisha yake ! Waliingia Kigoma siku mbili baadaye akiwa hoi bin taaban, na kuchukua vyumba katika hoteli iliyoitwa Lubumbashi, moja ya hoteli maarufu na za gharama mjini Kigoma.
Vichwani mwao hakuna kitu walichokuwa wakifikiria zaidi ya Nancy na mama yake, mioyo yao isingetulia mpaka wawapate watu hao ! Muda walioingia Kigoma ulikuwa mbaya, wasingeweza kufanya jambo lolote kwa kuwa tayari ilikuwa ni usiku, walilazimika kulala mpaka siku iliyofuata.
Kama ilivyo kwa siku nyingine zote, hapakuwa na usingizi kwa wote wawili ! Walikesha wakiongea na kuchanga mawazo juu ya tatizo lililokuwa limewapata, lilikuwa tatizo lao wote wawili na walikuwa na wajibu wa kulitatua.

“ Nitatumia kila kitu nilicho nacho mpaka mke wangu na mwanangu wapatikane!” Alisema mzee Katobe. “ Hata mimi pia nitatumia nguvu zangu zote kuhakikisha wanapatikana, hata kama ni kupamabana mipo tayari kupoteza maisha yangu kwa ajili ya Nancy na mama !”

Hayo ndiyo yalikuwa maneno yao, mwanzoni yalionekana ya kawaida lakini baadaye yalibadilika na kuwa kiapo ! Waliapa kuwapata Nancy na mama yake kwa udi na uvumba.
Asubuhi kulipokucha kila mmoja aliingia bafuni na kuoga, wakapata kifungua kinywa na kuondoka kuingia mitaaani ambako walianza msako kuwatafuta Nancy na mama yake, mzee Katobe akiwa na picha zao mkononi na kumwonyesha kila mtu aliyemsimamisha kumuuliza.
Kutwa nzima ya siku hiyo bila kupumzika waliuzunguka mji wa Kigoma na kuugeuza chini juu bila mafanikio ya kuwapata wala kusikia habari zao, waliporudi hotelini saa 3 usiku walikuwa wamechoka hawakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuoga, kula kisha kujitupa kitandani na kulala.
Huo uligeuka na kuwa utaratibu wao wa kila siku kwa wiki moja na nusu lakini bado hawakufanikiwa kuwapata Nancy na mama yake, walifika Bandarini kwenye ofisi za meli zilizofanya safari kati ya Kigoma na Zaire kuuliza kama walisafiri na vyombo hivyo, majina yao hayakuwepo ! Walichanganyikiwa na kushindwa wafanye nini, akili zao zilionekana kufikia kikomo cha kufikiri.
“ Nina wazo!”
“ Wazo gani mwanangu?” mzee Katobe aliuliza
“ Kwanini tusitumie hizo picha zao kutengeneza matangazo tuyabandike mitaani, nina uhakika lazima kuna watu waliishawahi kuwaona, kama si Nancy basi mama au wote pamoja !”
“Ni wazo zuri lakini si zitakuwa picha zisizo na rangi, watawatambuaje?”
“Siku hizi utalaamu umeongezeka sana, uwezekano upo wa kutengeneza matangazo kwa rangi ili mradi tuwe na pesa!“
“Nimekwisha sema niko tayari kutumia kiasi chochote cha pesa lakini mwanagu na mama yake wapatikane! Pesa haina tena thamani tena kwangu, maisha yangu yamekwishaharibika ! Ninachohitaji hivi sasa ni furaha na hiyo haiwezi kupatikana bila Nancy na mama yake kupatikana” Aliongea mzee Katobe kwa sauti ya kuhuzunika, ni wazi aliyoyasema yalitoka moyoni mwake. Basi niachie hiyo kazi, mimi nitaifanya ! “ Aliongea Danny.
Siku iliyofuata asubuhi Danny alikuwa wa kwanza kuondoka hotelini na kuingia mitaani ambako alifanya kazi ya kutafuta kiwanda cha uchapishaji, haikuwa kazi ngumu sana kwani saa mbili baadaye tayari alishakipata kimoja na alikuwa kwenye mazungumzo na Mkurugenzi wake, picha za Nancy na mama yake zikiwa mezani.
“ Nataka yawe na ukubwa wa karatasi moja ya A4, picha ziwe za rangi na ziwe kubwa!” “Juu yake kutakuwa na maneno gani?”
“Wanatafutwa na ndugu zao!”
“Kuna zawadi?”
Mkurugenzi wa kampuni hiyo bwana David Msanii aliuliza.
“Duh ! Nimesahau kuuliza, naweza kutumia simu yako?”
“Bila matatizo!”
Danny alinyanyua mkono wa simu na kubonyeza namba za hoteli ya Lubumbashi na kuomba aunganishiwe chumbani mwa mzee Katobe, sekunde kadhaa tu baadaye mzee Katobe alikuwa kwenye laini,
“Nani?”
“Ni mimi Danny!”
“Vipi umefanikiwa?”
“Ndiyo! ila kuna kitu kimoja nilisahau kukuuliza ! ”
“kitu gani?”
“Kuna zawadi yoyote tunayotoa?”
“Ndiyo! Utawezaje kuwatangazia watu wamtamfute mtu kusiwe na zawadi?”
“Sawa ni zawadi gani?”
“Millioni mbili kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa mwanangu na mama yake?”
“Ahsante sana!”
Baada ya maongezi hayo Danny alimgeukia bwana David Msanii, aliyekuwa ameketi kitini akisubiri kupewa jibu, alikuwa akichora kwenye karatasi nyeupe namna ambavyo tangazo hilo lingeonekana.
“Ni milioni mbili!” Alisema Danny. “Sawa ! Kwa hiyo hii ‘Milioni mbili’ itakaa chini yakiwa ni maandishi makubwa na ‘anatafutwa na ndugu zao’ itakaa juu, halafu hapa katikati nitaweka maandishi madogo yanayosema ‘zawadi ni’!” Aliongea bwana Msanii.
Kwa maelezo yaliyotolewa Danny alielewa tangazo lingekuwa la kuvutia sana hasa kama picha zingetoka jinsi zilivyoonekana. “Picha zitatoka hivyo hivyo?” “Ndiyo, kuna kitu kingine mngependa kuongeza?”
“Andika namba ya simu ya bosi wangu na uwaeleze kuwa anapatikana hoteli ya Lubumbashi! Baada ya siku ngapi nitegemee kupata matangazo haya?”
“Ninaanza kazi leo, nipe siku tatu!”
“Gharama yake itakuwa kiasi gani?”
“Bahati mbaya sijaelewa idadi ya nakala ninazohitaji”
“Ili kila mtu kati mji wa Kigoma ayaone matangazo haya tunaweza kuchapa kiasi gani?
Pesa sio tatizo kinachohitajika ni matangazo yawafikie watu!”
“Labda nakala elfu tano!”
“Zitagharimu kiasi gani?”
“Shilingi laki tano!”
“Hilo sio tatizo, nipe simu tena nimweleze mzee.”
“Hakuna shida.”
Danny alimweleza mzee Katobe kila kitu na akakubaliana na bei, mchana wa siku hiyo walimletea asilimia hamsini ya malipo kama utangulizi na kazi ikaanza! Siku tatu baadaye kazi ikakamilika, mzee Katobe akaajiri vijana wa matangazo, yakabandikwa katika kuta nyingi mjini Kigoma. Hapakuwahi kuwa na matangazo yaliyotapakaa namna hiyo katika mji wa Kigoma, habari ya Nancy na mama yake ikawa gumzo, watu wakawa wanaiita Bingo huku kila mtu akimpeleleza mwenzake ili apate angalau fununu ambazo zingemwezesha kuny’akuwa donge hilo.

Je nini kitaendelea?
Je Danny na mzee KAtobe watafanikiwa kuwapata Nancy na mama yake?