TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA

SEHEMU YA 16
Uchungu mkubwa ulimkamata moyoni, alitamani mambo yawe tofauti lakini hakuwa na jinsi ya kufanya ili kuubadilisha ukweli wa hali iliyokuwepo! Kifo cha mama yake kilikuwa kimefika na sasa chake kilikuwa kinafuata, mawazo hayo yalimfanya Nancy apoteza matumaini kabisa na hapo hapo akaona giza nene likiyafunika macho yake, mbingu zikafunguka na kuwa wazi, hakuwa na fahamu tena juu ya ulimwengu wa kawaida.
Kwa mbali alimuona mnyama mkubwa mwenye mbawa na manyoya mengi akija kwa kasi kutoka mbinguni, mikono yake ilikuwa mikubwa mithili ya shina la mti wa mbuyu, kulikuwa na kucha ndefu na nene mwisho wa mikono ya mnyama huyo.
Cha kushangaza zaidi alikuwa na jicho moja tu, alipofungua mdomo wake meno makubwa zaidi ya mamba yalionekana mnyama huyo alitisha kabisa, kadri alivyodi kumkaribia ndivyo mdomo wake ulivyozidi kufunguka ikiwa ni ishara kwamba alitaka kumla. Nancy hakuhitaji kuelezwa na mtu kuwa mnyama huyo mwenye mkia mrefu alikuwa nani, alielewa mara moja alikuwa shetani akija kuichukua roho yake!
Hakuwa tayari kwa jambo hilo bado alitaka kuishi duniani alikuwa mtoto mdogo mno kufa kabla hajapata digrii yake ya chuo kikuu, alihitaji nafasi zaidi aendelee kumtafuta mganga wa kienyeji mzee Mwinyimkuu ili amwondolee kiapo alichokiweka moyoni mwake kwamba hatafanya ngono na mwanaume mwingine yoyote yule maishani mwake isipokuwa Tonny ambaye kwa wakati huo hakuwa mpenzi wake tena alishamwacha na kumchukua mwanamke mwingine! Ni kiapo tu alichokula ndicho kiliharibu maisha yake, alitaka kiondolewe, kisha amsahau Tonny na asimpende mwanaume mwingine tena baada ya hapo maisha yake yangekuwa safi.
“Ee Mungu nisaidie nipe nafasi nyingine! Bado nataka kuishi, niongezee siku utakazo wewe!” Alipiga kelele Nancy mnyama yule alipozidi kumkaribia.
***
Polisi waliridhishwa na maelezo ya Danny juu ya mtu aliyempiga risasi ingawa walihisi kulikuwa na jambo aliloficha juu ya mzee Katobe bado walishindwa kumlazimisha akubali walichokitaka na kwa maelezo hayo walijikuta wakikosa kesi na kumwachia huru! Shukrani ya mzee Katobe kwa kijana huyo hazikuwa na maneno ya kutosha kuieleza, alipotoka tu mahabusu alinyoosha moja kwa moja hadi hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na kuingia hadi chumba alicholazwa Danny.
“Nakushukuru sana, najua umeamua kunisaidia ili kuniepusha na kufungo, hakuna wema unaoweza kulingana na ulionifanyia niko tayari kufanya lolote kama shukrani, ni mimi niliokukosea!”
“Hujanikosea kitu baba!”
“Nilikupiga risasi lakini umeamua kuficha siri!”
“Nafahamu lakini usijali, nimefanya hivyo kwa sababu nampenda Nancy!’
“Sema chochote unachotaka kutoka kwa Nancy nani nitakusaidia!”
“Nampenda nataka awe mke wangu!”
“Umekwisha kumpat! Sema kingine!”
“Sina zaidi!”
“Mama amemfuatilia, hivi sasa yuko Kigoma na ninafikiri katika muda wa wiki moja atakuwa amekwisharejea!”Aliongea mzee katobe bila kuelewa mambo yaliyokuwa yakitokea upande wa pili, katika ziwa Tanganyika ambako Nancy na mama yake walikuwa wakihangaikia roho zao, angejua wala asingetamka maneno yaliyokuwa yakimtoka mdomoni.
“Kwa hiyo akirudi na mimi nikiruhusiwa kutoka hospitali tutaoana?”
“Mimi ni baba yake, nikisema neno hakuna mtu wa kupinga! Hesabu wewe na Nancy ni mtu na mkewe, unasikia Danny? Hiyo ndiyo shukrani yangu kwako!”
“Ahsante baba!”
Mzee Katobe alishinda hospitali hadi usiku ulipoingia akimsaidia Danny katika mahitaji yote, hakuwa na mtu wa kumpa msaada tangu wazazi wake wasuse na kuondoka baada ya yeye kushindwa kueleza ukweli juu ya mtu aliyempiga risasi, walikerwa na kitendo cha Danny kuuficha ukweli, waliona mtoto wao amewavunjia heshima, kwa sababu hiyo mzee Katobe aliona wajibu wa maisha yote ya Danny ulikuwa juu yake, alikuwa na kila sababu ya kumsadia na kwa sababu alikuwa ametoka mahabusu aliahidi kufanya bila kilichohitajika kwa gharama yake.
Danny aliendelea kupata matibabu hospitali, mfupa wake ukiendelea kuunga taratibu, mawazo yake yote yalikuwa kwa Nancy alitamani arudi, wafunge ndoa na baada ya hapo warejee chuoni na kuendelea na masomo hadi mwisho, wamaliza na kupata digrii zao za sheria! Mambo yake yasingekuwa sawa wala furaha yake maishani isingekuwa kamili bila Nancy! Hivyo ndivyo alivyoelewa, ndiyo maana alikuwa tayari kuwasaliti wazazi wake kwa sababu ya mwanamke aliyempenda, penzi alilokuwa nalo kwa Nancy halikuwa la kawaida.Ilikuwa rahisi mtu kuhisi labda alinyweshwa mti dawa ya mapenzi ya kuwapumbaza wanaume jambo ambalo kwa hakika halikuwa kweli.
Siku zilizidi kukatika hatimaye wiki ikaisha tangu mzee Katobe aachiwe kutoka mahabusu, bila Nancy pamoja na mama yake kurejea! Wasiwasi ulianza kuingia moyoni mwa Danny na mzee Katobe, hisia kwamba kulikuwa na tatizo lililowapata huko Kigoma zilitawala mawazo yao, hata hivyo hawakutaka tamaa kabisa walizidi kuongeza siku lakini bado hakurejea mpaka wiki ya pili ikakatika na wasiwasi ukazidi kuongezeka.
“Labda hawajaonana, anaendelea kumtafuta!” Danny alisema.
“Inawezekana kabisa! Bahati mbaya hata namba ya simu sina na huko alikokwenda sina mwenyeji ambaye ningemwomba anisaidie kumtafuta, nafikiri hakuna tatizo, tuchukulie bado anamtafuta!”Mzee Katobe aliongea.
“Ikipita wiki itabidi kuwafuatilia, lazima watakuwa kwenye matatizo!”Danny alishauri.
“Itabidi iwe hivyo!”
“Kama nitakuwa nimeruhusiwa itabidi tuongozane kama tu pesa itakuwepo, nisingependa kuona unahangaika peke yako!”
“Unategemea kuruhusiwa hivi karibuni!”
“Daktari alikuja juzi akasema hali yangu siyo mbaya naweza kuondoka mfupa wangu umeunga vizuri! Kama sikosei kesho naweza kupewa ruhusa!”
Kama alivyosema Danny kweli siku iliyofuata, aliruhusiwa kutoka hospitali baada ya X-ray yake kuonyesha mfupa ulishaunga vizuri, ilikuwa furaha kubwa mno kwake kutoka hospitali na hakuwa na mahali pengine pa kwenda isipokuwa nyumbani kwa mzee Katobe ambako wote wawili waliendelea kusubiri nancy na mama yake warejee ili mipango ya ndoa ifanyike, Danny ajipatie mke! Mpaka wakati huo hakuwa mtu aliyekuwa ameelewa kitu chochote juu ya matatizo ya upande wa pili wa shilingi.
“Hatuna njia lililopo ni kusafiri hadi Kigoma kuwafuatilia, nafikiri watakuwa kwenye matatizo!”Mzee Katobe alimwambia Danny wote wawili wakiwa mezani, chakula kilikuwepo lakini hakuna mtu aliyetamani kula! Fikra juu ya Nancy na mama yake zilichukua hamu yao ya chakula.
“niko tayari wakati wowote ukitaka tusafiri!”
“Kesho unaonaje? Mguu wako hauwezi kukusumbua?”
“Mimi ni mzima kabisa! Lolote utakalotaka hivi sasa naweza nikifanya!”
“Basi kesho tunaondoka!”
“Sawa!”
Waliagana na kila mmoja kuingia chumbani kwake kulala, kilikuwa chumba kizuri chenye kila kitu kuanzia sofa, televisheni, kiyoyozi, choo na bafu ya ndani, kilitosha kumpa binadamu yoyote raha na usingizi mara moja aingiapo chumbani, lakini ilikuwa tofauti kwa Danny, mawazo juu ya Nancy yaliendelea kumsumbua kichwani mwake mpaka saa tisa usiku alikuwa bado hajapata hata lepe la usingizi.
Masaa kumi, kumi na moja ya alfajiri hakuyaona, yalipita bila taarifa! Danny alikuwa kanisani ambako padri na kitabu chake cheusi kiitwacho Biblia alisimama mbele yake! Pembeni mwake akiwepo Nancy ndani ya shela nyeupe iliyompendeza vizuri kwa hakika wote wawili walivutia, watu wengi walijaa kanisani, mama yake Nancy alikuwepo, watu pekee ambao hakuwaona walikuwa ni wazazi na ndugu zake lakini pamoja na kutokuwepo kwao bado alikuwa na furaha kwa sababu alikuwa amemuoa Nancy, mwanamke aliyemhangaisha kwa muda mrefu.
“Danny uko tayari kumuoa Nancy?” Padri aliuliza.
“Ndiyo!”
“Unakubali kuwa naye katika shida na raha mpaka Mungu atakapowatenganisha?”
“Ndiyo padri!”
“Unaweza kuwe sahihi kwenye fomu iliyoko mbele yako!”
Danny aliinama mbele ya meza ambayo juu yake kulikuwa na fomu nyeupe pamoja na kalamu, akaichukua kalamu na kuweka saini yake, baadaye padri alimgeukia Nancy na kumuuliza maswali hayo hayo lakini badala ya kujibu alibaki kimya machozi yakimbubujika! Padri alimuuliza zaidi ya mara mbili, hakufungua mdomo wake kuseme kitu chochote, watu wote kanisani walishindwa kuelewa ni nini kilikuwa kinatokea, kanisa lilibaki kimya, furaha ilianza kuyeyuka.
“Siwezi!Siwezi!Padri siko tayari kuolewa, simpende Danny badi nampenda yule pale!” Nancy aliongea akisonta kidole chake kwenye kona katikati ya watu waliohudhuria kanisani kushuhudia ndoa ikifungwa, watu wote walielekeza macho yao mahali kidole cha Nancy kilikoelekezwa na kumwona kijana mrefu akinyanyuka na kusimama wima. ALIKUWA NI TONNY! Na alianza kutembea kuelekea altareni na kwenda kumkumbatia Nancy mbele ya Danny , wazazi pamoja na padri.
Danny alishindwa kuvimilia na kumsogelea Tonny hasira kali ilikuwa imempanda, alikunja ngumi yake ya mkono wa kushoto na kuitupa kuelekea usoni kwa Tonny, ilikuwa nzito iliyompelekea Tonny sakafuni, huku damu nyingi zikimtoka puani, kanisa lilianza kupiga kelele watu wakikimbia kwenda nje na wengine kwenda mbele kushuhudia kilichotokea.
“harusi imevunjika! Harusi imevunjika!”Maneno hayo yalisikika kila sehemu kanisani.
Padri wazazi pamoja na wazee waliokuwepo kanisani walimzunguka Tonny aliyekuwa amelala cini akiwa ametulia kabisa, baadhi walikuwa wakimshika kifuani upande wa moyo kuona kama ulikuwa unapiga na wengine wakimshika mishipa ya mikononi lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyekutana na pigo la moyo wala mshipa.
“Amekufa!”
“Kweli? Haiwezekani, mbona nimempiga kidogo tu!”Danny aliongea akijilaumu, alijutia tendo alilofanya! Hapo hapo alikalishwa chini na kuzungukwa na baadhi ya waumini kanisani, hawakutaka aondoke sababu alishafanya mauaji! simi ilipigwa polisi na muda mfupi baadaye maaskari waliingia na kumpiga pingu, wakaanza kumsukuma kwenda nje huku akilia machozi, hakuna mtu aliyemwonea huruma.
“Nancy!Nancy! Kwanini umenifanyia ukatili huu nikukosea.....!:Hakuimalizia sentensi yake alikuwa akitingishwa kwa nguvu!
“Danny!Danny!Danny! Amka tuondoke tayari saa kumi na mbili na nusu, tuwahi mabasi ya kwanza kwenda Dar ili jioni tuondoke na treni!” Ilikuwa sauti ya mzee Katobe, alimkatisha Danny ndoto yake, alinyanyuka huku akilia machozi na kumshangaza mzee Katobe.
“Vipi mbona unalia?”
“Ndoto! Nimeota ndoto mbaya sana!”
“Ndoto gani?”
“Ndoto tu, ila ni ya kutisha! Nashukuru ni ndoto vinginevyo nilikuwa na kwenda jela!”
“Achana na ndoto mwanangu, mara nyingi ni matokeo ya fikra unazokuwa nazo, tafadhali oga, kisha vaa tuondoke!”

Je nini kitaendelea?