TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA 12

Hali ilikuwa mbaya mjini Bagamoyo, baba yake Nancy alikuwa bado akishikiliwa na polisi kwa kosa la kumshambulia Danny kwa risasi, alishahojiwa tayari na hata mke wake pia na wote katika maelezo yao walikanusha kutokea kwa tukio hilo! Maelezo pekee ambayo yalikuwa bado hayajachukuliwa yalikuwa ni ya Danny aliyekuwa hospitali akiuguza mguu wake uliovunjika, aliwazungusha maaskari kwa makusudi.
Kama ilivyokuwa kwa mama yake Nancy, ndivyo ilivyokuwa kwa Danny! Wote hawakuelewa ni wapi alipokuwa Nancy kwa siku zote alizokuwa amepotea, mama alichanganyikiwa! Kuna wakati alihisi mwanae alichukua uamuzi wa kwenda kujiua, baada ya kutafuta kwa siku kadhaa bila mafanikio hatimaye aliamua kutoa taarifa polisi ambao waliendesha msako katika magofu yote mjini Bagamoyo na hata ufukweni mwa bahari ya Hindi lakini hakuna aliyefanikiwa kumwona Nancy.
Hakuna aliyeelewa binti huyo alikuwa wapi, mahojiano kati ya Danny na polisi yaliahirishwa kila siku kutokana na Danny mwenyewe kugoma kuongea, alitaka kwanza akutane na Nancy waongee na kupanga namna ya kufanya! Alielewa wazi katika hatua tatizo la baba yake lilipokuwa Nancy asingekuwa na chaguo jingine isipokuwa kukubali kuwa mpenzi wake tu! Kitendo chake cha kupotea katika mazingira ya kutatanisha kilimfanya Danny avute subira.
Wazazi wa Danny tayari walisharejea nchini kutoka Uswis ambako wote walifanya kazi Benki ya Dunia na kwenda Bagamoyo ambako waliendelea kumuuguza mtoto wao pekee wa kiume Danny! Alikuwa kipenzi chao.
Hakuweza kuwaficha wazazi wake ukweli juu ya tukio lililotokea, kila kitu alikiweka wazi, walichukia kupita kiasi na walitaka mzee Katobe apewe adhabu kubwa na ikibidi kufungwa miaka mingi afie gerezani au aonyongwe.
Kwa nguvu ya ushawishi aliyokuwa nayo baba yake Danny, mzee George Kasoma katika serikali na hata mahakama ingawa hakuna mtu aliye juu ya sheria, lazima mzee Katobe angefungwa, hicho ndicho walichotaka kitokee na kila siku walimshawishi mtoto wao atoe maelezo kwa polisi kueleza kila kitu kilichotokea mpaka kupigwa risasi.
Mara kadhaa mama yake Nancy aliwafuata wazazi wa Danny na kuwaomba msamaha ili mtoto wao asifungue mdomo na kusema ukweli lakini kila alipokwenda alifukuzwa, hawakutaka hata kumwona na walimhakikishia lazima mzee Katobe angefia jela!
Alipoona imeshindikana kwa wazazi wa Danny alirudisha matumaini yake kwa mtoto, kila siku alimbembeleza Danny asimwingize matatani mume wake kwani alikuwa na uwezo wa kumwepusha na kifungo.
“Ilikuwa ni hasira tu! Hata baba Nancy anajuta, amenituma nije kwako kukuomba umsaidie!”
“Mama siwezi kukudanganya, kama Nancy akipatikana na akakubali kuwa mke wangu nitafanya kesi hii isiwepo kwa sababu mimi ndiye mwenye kauli, wazazi wangu kila siku wananishinikiza nitoe maelezo ya kumgandamiza mzee Katobe lakini nasita kwa sababu sijaonana na Nancy na kusikia msimamo wake, nakushauri uendelee kumtafuta bila kuchoka!”
“Nimejitahidi sana! Lakini mafanikio ni kidogo, sijui mwanangu atakuwa amekwenda wapi? Nina wasiwasi atakuwa amekufa! Ina maana asipopatikana Nancy huwezi kumsaidia baba yake?”
“Kwa kweli haiwezekani! Na ninasema wazi kuwa, nitawazungusha polisi kwa wiki tatu mfululizo, baada ya hapo nitalazimika kusema ukweli kwa hiyo ongeza juhudi za kutafuta mama!” Alimaliza Danny, walikuwa wawili tu ndani ya chumba alicholazwa, wazazi wa Danny walikuwa hawajafika kutoka hoteli ya Badeco walikofikia.
Mama yake Nancy aliondoka wodini akiwa amenyong’onyea kupita kiasi, maneno yaliyosemwa na Danny siku hiyo yalitisha, aligundua hapakuwa na utani na ilikuwa ni lazima afanye kila kinachowezekana ili mtoto wake apatikane. Hilo ndio lingeweza kumwokoa mume wake na kifungo, hakuwa na chaguo lolote zaidi ya kuridhia mwanae aolewe na Danny kama kwa kufanya hivyo kungemfanya kijana huyo afiche siri yake ya risasi.
“Hata hivyo sio mbaya! Sijui kwanini Nancy hamtaki wakati wazazi wake wana uwezo na ni wasomi wazuri tu! Ni familia nzuri ambayo kama Nancy akiolewa kwayo itakuwa ni furaha tu, ni lazima apatikane kama yuko hai! Nitafanya kila kinachowezekana, nitatumia kila kilichopo katika muda wa wiki mbili atakuwa amepatikana!” Aliongea peke yake mama Nancy akitembea kutoka wodini hadi nje ambako alipanda gari lake na kwenda hadi gerezani ambako mume wake aliwekwa mahabusu.
Alimweleza kila kitu kilichoongelewa na hata mzee Katobe mwenyewe alikubali Nancy aolewe na Danny, hakuna mtu kati yao aliyeielewa siri ya Yamini aliyokula kwa mganga wa kienyeji, mzee Mwinyimkuu ndio maana walikuwa tayari hata kutumia nguvu ili mradi Nancy aolewe na Danny na hatimaye mzee Katobe kuachiwa huru.
“Sasa sijui tutampata wapi?”
“Peleka matangazo redioni na kwenye televisheni pia!”
“Nitafanya hivyo!”
“Na utangaze zawadi nzuri kwa mtu yeyote ambaye atasaidia kupatikana kwa Nancy, kama yupo hai lazima tutampata! Lakini kama amekufa basi tena!”
“Lakini mimi nina wasiwasi huyu mtoto anaweza kuwa amerudi tena China! Tatizo anampenda sana Tonny, pamoja na mabaya yote aliyofanyiwa yupo tayari kurudiana naye!”
“Basi nenda Wizara ya mambo ya nchi za nje wanaweza kukuelekeza jinsi ya kuwasiliana na ubalozi wa nchi yetu nchini China ili watusaidie kumtafuta!Kwanini umefikiria hivyo?”
“Nilikuta zile pesa ulizoziweka kabatini hazipo!”
“Basi kaondoka! Wala tusihangaike kufikiri eti amekufa! Ila sijui tutamrudishaje ili aje aongee na Danny wakubaliane na mimi nitolewe mahabusu!”
“Wazo lako la mambo ya nchi za nje nimelipenda, ninakwenda sasa hivi!”
Alipotoka mahabusu mama Nancy alinyoosha moja kwa moja kuelekea Dar es Salaam, saa moja na nusu baadaye alikuwa jijini na kwenda moja kwa moja redio one na ITV ambako alilipia matangazo ya kutafutwa kwa Nancy, kutoka hapo alinyoosha moja kwa moja wizara ya mambo ya nchi za nje na kueleza tatizo lake kwa msaidizi wa waziri aliyeamua kupiga simu kwenye ubalozi wa Tanzania nchini China na kuahidiwa kuwa Nancy angetafutwa kwa udi na uvumba, wafanyakazi wengi wa ubalozi walimkumbuka kutokana na vurugu alizozifanya nchini humo.
Matangazo yalianza kuruka hewani karibu kila siku lakini hakukuwa na mafanikio yoyote, siku zilizidi kukatika hatimaye wiki ya kwanza, ya pili na kuingia ya tatu! Danny bado aliendelea kusisitiza nia yake ya kueleza ukweli kama Nancy asingepatikana ndani ya wiki tatu, polisi bado walimtembelea wakitaka kuchukua maelezo yake.
“Wiki ijayo ndio nitakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kutoa maelezo! Kwa sasa hivi hapana!” Alizidi kuvuta muda ili wiki tatu zikamilike hatimaye ikawa imebaki siku moja bila Nancy kupatikana wala habari za yeye kuonekana mahali popote kusikika! Mama yake alizidi kuchanganyikiwa naye alikata tamaa kabisa ya kumwokoa mume wake na kifungo! Alijihesabu duniani alikuwa amebaki peke yake baada ya mume wake kufungwa maisha na mwanae kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Siku ya mwisho alidamka asubuhi na mapema na kuwahi wodini akiwa bado amekata tamaa, alitaka kuongea na Danny kwa mara nyingine na kumwomba aongeze muda zaidi, aliwakuta wazazi wake wamekwishafika hivyo akashindwa kuongea na kubana nje ya wodi hadi walipoondoka ndipo naye akaingia na kumkuta Danny amejilaza kitandani.
“Mama nafikiri imeshindikana, ulichokifanya ninakijua! Uliamua kumficha Nancy makusudi ili nisimuoe, sasa shauri yako!” Aliongea Danny kabla hata ya salamu.
“Mwanangu salamu kwanza basi!”
“Sitaki salamu, nilikupa wiki tatu umeshindwa kuzitumia sasa nawasubiri maaskari niwaeleze ukweli!”
Muda mfupi baadaye mlango ulifunguliwa wakaingia wanaume wawili, mama yake Nancy aliwaelewa mara moja kwani ndio waliochukua maelezo yake kituo cha polisi, walikuja kuchukua maelezo ya Danny ili kukamilisha upelelezi ndio kesi ya mzee Katobe ipelekwe mahakamani, maelezo ya Danny yalikuwa ni muhimu sana katika kesi hiyo, maisha ya mzee Katobe yalikuwa mikononi mwake, kama angesema hakupigwa risasi na mzee huyo basi angeachiwa huru lakini kufungua kwake mdomo na kusema ni mzee Katobe aliyempiga risasi kungemaanisha kifungo cha maisha jela.
“Karibuni wazee! Nawasubiri sana leo nimepania kueleza ukweli juu ya tukio hili, kwa muda mrefu sana mmehangaika kutaka niongee nanyi lakini sikuweza, afya yangu haikuwa nzuri! Namshukuru Mungu leo naweza kuongea”
“Vizuri sana! Na huyu mama?” Aliuliza askari akiwa amemwangalia mama Nancy.
“Ni rafiki wa familia yetu!”
“Huyu si ni mke wa mzee Katobe?”
“Ndiyo!”
“Hatuwezi kuchukua maelezo akiwa hapa! Mama toka nje”
“Sawa!” Alijibu mama Nancy akitembea na kufunga mlango nyuma yake, alishindwa kujizuia na kuanza kulia hadi alipolifikia gari na kuingia ndani kisha kuondoka kuelekea nyumbani, hakutaka kuelewa nini alichokiongea Danny! Dakika tano tu baadaye alikuwa nyumbani kwake, ambako aliingia na kujitupa kwenye kochi sebuleni akaendelea kumlilia mume wake tangu siku hiyo aliamini asingeishi naye tena milele na milele.
Akiwa katika mawazo mengi mara mlango wa chumba chake uligongwa na akanyanyuka na kuusogelea kisha kufungua na kuchungulia nje, kijana mdogo alisimama mbele ya mlango akiwa na bahasha mkononi mwake na kumkabidhi baada ya salamu.
“Zimetoka wapi?”
“Baba alikuja nazo!”
“Kutoka wapi?”
Je nini kitaendelea?
Je hizo bahasha zimetoka wapi?