TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA SABA

Dakika zilizotolewa na maaskari ili Tony na Nancy waongee zilikwisha, akaanza kuvutwa hadi kwenye gari ambako mlango ulifunguliwa akaingizwa ndani kwa nguvu huku akilia, maaskari wawili wakaingia na kukaa mmoja kila upande wa Nancy! Lilikuwa jambo la kutia huzuni sana lakini alipochungulia nje kupitia dirishani alimwona Tony akicheka, moyo wa Nancy ulizidi kuuma.
Kwa nguvu za Kitanzania kabla gari halijaondoka, akiwa amepigwa pingu mikononi, Nancy alijitahidi na kumsukuma askari aliyekuwa mkono wake wa kuume na wote wawili wakaanguka chini.
“I’m not going!”(Siendi!)
Pamoja na kukataa Nancy asingeweza kuwashinda maaskari wawili kwa pamoja, alikamatwa tena, akapakiwa ndani ya gari na likaondoka moja kwa moja hadi uwanja wa ndege.
Wakati wanawasili uwanja wa ndege ilikuwa tayari saa moja na nusu, masaa mawili baadaye Nancy alitakiwa kuondoka chini ya ulinzi wa maaskari wawili wa Kichina! Alikuwa bado akilia na kujaribu kuchukulia mambo yaliyotokea kama ndoto, akiamini labda baadaye angezinduka na kujikuta yuko Tanzania akiongea na Tony katika simu, wakicheka na kufurahi na kukumbushiana ahadi yao ya ndoa baada ya masomo.
Haikuwa hivyo, kila kitu kilichotokea kiliendelea kuwa kweli na saa tatu na nusu Nancy alikabidhiwa kwa maaskari wengine wawili tofauti na waliomtoa kituoni, akaongozwa hadi ndani ya ndege ambao alikaa katikati ya maaskari wawili akiwa chini ya ulinzi wa kutosha.
“Why do you treat me like a Terrorist?”(Kwanini mnanichukulia kama gaidi?) Aliwauliza maaskari wakati ndege ikijiandaa kuruka.
“That is what we have been told to do! You are supposed to reach Tanzania under Maximum security!”(Hivyo ndivyo tulivyoambiwa tufanye, unatakiwa kufika Tanzania chini ya uangalizi wa hali ya juu kiusalama!) Alijibu mmoja wa maaskari.
Ndege iliiacha China na saa moja na nusu baadaye ilikuwa ikitua katika uwanja wa ndege wa Hong kong, abiria wengine walipanda katika uwanja huo, wakiwemo waafrika kadhaa! Wote walimwangalia Nancy kwa macho ya huruma.
Alifika hapo akilia, hata ndege ilipoondoka bado aliendelea! Dubai hadi Nairobi hakuweza kuyazuia machozi yasitiririke, moyo wake ulikuwa umeumia kiasi ambacho binadamu yeyote asingeweza kuvumilia!Hakuna alichouambia moyo wake zaidi ya kutopenda tena, aliahidi kutomruhusu mwanaume kuuteka moyo wake tena.
“Nitaishi mwenyewe! Sitaki mpenzi tena maishani mwangu, sitapenda tena!” Alijisemea Nancy alipoikanyaga ardhi ya Kenya baada ya kushuka kutoka katika ndege ya China Airways.
Chini ya ulinzi mkali alipakiwa ndani ya ndege ya shirika la Ndege la Kenya, iliyokuwa ikisafiri kutoka Nairobi kuelekea Dar es Salaam. Alifurahi kufika karibu na nyumbani, mahali kulikokuwa na watu waliompenda ambao angewaeleza matatizo yake na pengine wakampa faraja. Kidonda kilikuwa kikubwa moyoni na hakutegemea kingepona kwa urahisi.
Nusu saa baadaye ndege iliondoka Nairobi na kutua Dar es Salaam katika muda wa saa moja, uwanja wa ndege badala ya kupokelewa na wazazi wake, Nancy alipokelewa na maaskari, makabidhiano kati ya maaskari wa China na Maaskari wa Tanzania yalifanyika mbele yake huku kamera za waandishi wa habari zikimulika kila upande, kichwani mwake alielewa habari yake ingetawala vyombo vyote vya habari nchini Tanzania siku iliyofuata.
Maaskari wa China waligeuza na ndege iliyowaleta kurudi Nairobi, Nancy akawa ameingia mikononi mwa askari wa Tanzania na kupelekwa moja kwa moja hadi kituo cha polisi cha kati ambako kwanza kabla hata ya mahojiano alinyang’anywa hati yake ya kusafiria ndipo mahojiano yakaanza, alikataa kuongea chochote mpaka wazazi wake wawepo.
Ilikuwa tayari ni saa nne asubuhi Simu, ilipigwa nyumbani kwao Nancy huko Bagamoyo! Wazazi wake walipata mshtuko wa ajabu, hawakutegemea kabisa kupata habari hiyo asubuhi. Walichofahamu ni kwamba mtoto wao alikuwa nchini China.
“Nancy! Yuko kituo cha polisi?”
“Ndiyo!”
“Nini kimetokea? Si alikuwa China?”
“Ndiyo! Lakini amerudishwa nchini!”
“Kafanya nini?”
“Mtaelezwa mkifika hapa!”
“Tunakuja!” Baba yake Nancy alisema.
Baada ya kukata simu alimsimulia mke wake kila kitu na hawakutaka kupoteza muda, haraka waliingia ndani ya gari lao na kuanza kuendesha kuelekea jijini Dar es Salaam. Masaa mawili baadaye , sababu ya ubovu wa barabara, gari lao lilikuwa likiegeshwa mbele ya kituo cha polisi.
Walishuka na kutembea kwa haraka kuelekea ndani ambako waliulizia mahali alipokuwa mtoto wao, suala la Nancy lilishapata umaarufu kituo cha polisi, waliambiwa wapande hadi ghorofa ya tatu, ofisini kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa. Walimkuta Nancy amekaa kwenye benchi akiwa na mizigo yake na akiendelea kulia, alinyanyuka na kuwakumbatia baba na mama yake.
“Vipi mwanangu?” Mzee Katobe aliuliza.
“Tony!Tony!Tony baba kani....!” Kwikwi ya kulia ilimkaba Nancy kiasi cha kushindwa kuongea, wazazi wake walishindwa kuelewa ni nini kilichokuwa kimetokea mpaka mtoto wao kuwa katika hali hiyo na hapakuwa na uwezekano wa Nancy kueleza kutokana na hali aliyokuwa nayo, ilibidi mzee Katobe aingie moja kwa moja ofisini kwa mkuu wa Upelelezi Mkoa ili aelezwe kilichotokea, ndani aliambiwa kila kitu kilichotokea nchini China na kutoka akiwa amepandwa na hasira.
“Tenda wema uende zako usingoje shukrani! Yaani Tony ndiye mtu wa kunifanyia hivi mimi? Sawa tutaona!” Aliongea kwa chuki mzee Katobe.
“Kwani kimetokea nini?” Mke wake aliuliza.
“Twendeni, tutaongea kila kitu nyumbani!” Aliongea Mzee Katobe akimnyanyua Nancy kutoka mahali alipoketi, mke wake alisaidia kubeba mizigo na wakashuka ngazi hadi kwenye gari lao.
Waliondoka mzee Katobe akiendesha kwa kasi hadi Bagamoyo, waliingia saa sita ya usiku! Hawakuwa tayari kumwacha Nancy alale peke yake kwa hali aliyokuwa nayo, kilichofanyika ni mama yake kuhamia chumbani kwa Nancy na kulala naye hadi asubuhi. hakuna kilichofanyika zaidi ya kumfariji mtoto wao na kumfanya achukulie kila kitu kilichotokea kama sehemu ya maisha, walielewa ni kiasi gani iliumizwa lakini ilikuwa ni lazima waungane na mtoto wao katika tatizo alilokuwa nalo.
Asubuhi hiyo kabla hata ya kunywa chai, gari aina ya Rangrover, muundo wa kisasa liliegesha mbele ya nyumba ya mzee Katobe, kijana mrefu mwenye sura nzuri na mwili uliojaa kama mcheza mpira wa kikapu alishuka na kufunga mlango wa gari lake na kutembea hadi kwenye mlango wa mbele ambako aligonga na kufunguliwa na mzee Katobe.
“Shikamoo mzee!”
“Marahaba hujambo mwanangu?”
“Sijambo baba! Hapa ndio nyumbani kwa mzee Katobe?”
“Ndiyo! Na mimi mwenyewe ndiye mzee Katobe!”
“Ahsante mimi naitwa Danny! Ah, ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam!”
“Ndiyo, nikusaidie nini mwanangu?” Aliuliza mzee Katobe badala ya kumkaribisha Danny ndani ya nyumba.
“Ah! Nimesoma kwenye gazeti leo asubuhi, juu ya Nancy! Nimesikitika sana na nimelazima kuja kumwona!”
“Basi karibu ndani!” Mzee Katobe alifungua mlango na Danny akiwa na boksi mikononi mwake aliingia na kuketi kwenye kochi.
“Huyu bibie anakufahamu?”
“Sana! Na ni rafiki yangu!”
“Subiri basi nimwambie!”
Mzee Katobe aliondoka sebuleni na kumwacha Danny akiwa amekaa peke yake, kichwani mwake alikuwa na mawazo mengi na alimfikiria ana Nancy! Kwake yaliyoandikwa katika gazeti kwamba Nancy alipigana baada ya kusalitiwa na mpenzi wake, yalikuwa ni habari njema! Ulikuwa ni wakati muafaka wa kumpata msichana aliyempenda kuliko mwingine yeyote lakini akamkataa. Akiwa katika fikra hizo mzee Katobe alirejea, uso wake ulionekana kutoka na furaha kama aliyokuwa nayo mwanzo.
“Kijana!”
“Naam baba!”
“Mwenzako hataki hata kukuona! Kifupi anasema hataki kukutana na mwanaume yeyote kwa hivi sasa isipokuwa mimi baba yake! Kwa hiyo naomba uondoke” Aliongea Mzee Katobe bila kumwangalia Danny usoni.
“Sawa baba lakini naomba basi upokee huu mzigo na umpelekee, mwambia tu asome barua niliyoandika humo ndani ni matumaini yangu anaelewa leo ni siku muhimu kiasi gani katika dunia!”
“Kwani leo ni tarehe ngapi?” Aliuliza Mzee Katobe akipokea boksi kutoka kwa Danny.
“Tarehe kumi na nne mwezi wa pili!”
“Kwani leo kuna sikukuu gani?”
“Nancy ataelewa baada ya kusoma kadi iliyomo humu ndani na ninaomba umweleze nasubiri majibu yangu!”
“Sawa!”Mzee Katobe alijibu na kuondoka.
Danny alibaki kimya akiendelea kusubiri majibu yake kutoka ndani, dakika tano baadaye bado mzee Katobe alikuwa hajarudi! Kwa alichokiandika ndani aliamini lazima Nancy angeungana naye sebuleni na kumwambia alikuwa amekubali kuwa mpenzi wake na ni yeye Danny angekuwa chanzo cha furaha yake tangu siku hiyo.
Ghafla mlango ulifunguliwa, mzee Katobe akatoka akifuatana na Nancy! Danny akahisi ushindi moyoni mwake, aliona ni fundi wa kuandika maneno ya kutoa nyoka pangoni! Nancy alikuwa amebaba maua mikononi, yalikuwa ni yale ambayo Danny aliyanunua kwa Mama Henjewele asubuhi kabla hajaondoka Dar es Salaam na pia kadi aliyoandika ilikuwa mikononi mwa Nancy, alimfuata mpaka alipokaa! Akaikunjua tena ile kadi na kuanza kuisoma kwa sauti.
Nancy!
Naamini upo katika wakati mgumu kupita kiasi, mwanaume uliyempa mategemeo yako yote amekusaliti! Usilie sana Nancy, geuka angalia nyuma bila shaka utaniona mimi, mimi Danny mwanaume ninayekupenda kwa dhati ambaye siku zote nimejitahidi kukufanya uwe wangu lakini haikuwezekana.
Bila shaka Mungu alipanga haya yatokee ili niweze kukupata, sitaki kusema mengi, sitaki kukuahidi mengi ila ninakuahidi furaha katika maisha yako! Hakika na Mungu anajua sitakuumiza moyo Nancy kama alivyofanya Tony.
Tafadhali kubali niwe wako, nia yangu si ngono, nia yangu ni kukufanya uwe mwanamke mwenye furaha kuliko mwanamke mwingine yeyote chini ya jua hili la Mungu! Nakubembeleza Nancy, tafadhali kubali uone kama ninayoyasema ni kweli! Hakika hutajutia uamuzi wako wa kunikubali mimi, usimwache Tony achukue furaha yako yote , kwani yeye ni nani? Maisha ni mafupi kuendelea kulia! Ni vyema kuishi kila siku kama vile hakuna kesho, utaliaje wakati yeye anaendelea kufaidi maisha na mwanamke mwingine?
Tafadhali nikubali, niko chini ya miguu yako.
Happy Valentine Nancy!
Je nini kitaendelea?