TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA SITA

Wafanyakazi wa ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini China, waligubikwa na huzuni, habari kuwa msichana wa Kitanzania alikuwa amepigana katika chuo Kikuu cha Beijing, tena akiwa mgeni zilikuwa zimewasikitisha sana! Ilikuwa ni aibu kubwa kwa nchi ya Tanzania, ukizingatia uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya nchi hizo mbili.
“Tumwambie Balozi?”
“Hatuwezi kuficha, hili ni jambo kubwa sana na kwa sababu limeshafika polisi ni lazima Balozi ataliona katika taarifa za habari, tutaingia katika matatizo!”
“Basi nenda wewe ukamwambie!” Imelda, mmoja wa wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini China alimwambia mfanyakazi mwenzake aitwaye Kulwa, wote walikuwa ni vijana wa Kitanzania na walisikitishwa sana na kilichotokea.
“Nenda wewe, si ndiye sekretari wake?”
“Ina maana unamwogopa Balozi?”
“Sio hivyo tunafuata protoko!”
Imelda alinyanyuka kitini na kuanza kutembea kuelekea ofisini kwa Balozi, alifungua mlango na kuzama ndani wakati anaingia tayari saa ya ukutani ilikuwa ikionyesha saa kumi na moja na nusu kwa majira ya China! Balozi alikuwa nyuma ya meza kubwa, simu ilikuwa masikioni mwake alionekana kupokea maelekezo fulani kutoka nyumbani Tanzania. Imelda aliketi chini kumsubiri, dakika kumi baadaye alirudisha simu mahali pake na kumwamuru Imelda aketi kitini.
“Vipi binti?”
“Kuna tatizo mheshimiwa!”
“Tatizo gani tena?”
“Tumepigiwa simu kutoka kituo cha Polisi na kutaarifiwa kwamba kuna msichana kutoka Tanzania, aliwasili hapa jana na alikuja kumtembelea mchumba wake ambaye ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Beijing, sasa kilichotokea ni kwamba alimkuta mchumba wake ana mpenzi mwingine na kuamua kufanya vurugu kubwa iliyopelekea msichana ambaye ni mpenzi mpya wa mchumba wake kujeruhiwa vibaya, hivi ninavyoongea na wewe huyo msichana ameshonwa nyuzi kumi usoni na msichana wa Kitanzania yupo mahabusu!”
“Sasa?” Balozi aliuliza.
“Unahitajika makao makuu ya polisi Mheshimiwa na kama sio wewe,basi utume mjumbe!”
“Jamani hamuwezi kuona kuwa ni na kazi nyingi, hiyo simu uliyokuta naongea nayo imetoka Ikulu, kuna ujumbe wa chama cha wafanyabiashara na wenye viwanda nchini Tanzania, TCCIA, wanakuja hapa China kwenye maonyesho ya Februari. Sidhani kama naweza kwenda huko, hebu niitie Mwaibale!” Alisema Balozi akimaanisha msaidizi wake aitwe na Imelda alitoka ofisini haraka na aliporejea aliongozana na Kulwa.
“Ndio bosi!”
“Kuna tatizo nafikiri umeshalisikia!”
“Ndiyo!”
“Kwa hiyo naomba uniwakilishe makao makuu ya polisi, mimi siwezi kwenda najiandaa kupokea ugeni kutoka Tanzania!”
“Hakuna tatizo nitakwenda! Si ni lazima nianzie makao makuu?”
“Ndiyo! Si wito umetoka huko? Au sio Imelda?”
“Ndiyo hivyo bosi!”
***
Wakati wanaondoka ofisini kwa Balozi na Kulwa kupitiliza hadi nje ya ofisi ambako alipanda ndani ya gari, akiendeshwa na dereva wa Kichina Mr Yu kuelekea makao makuu ya polisi mtaa wa Capital.
Tayari ilikuwa saa kumi na mbili na dakika kumi na tano za jioni. Ni wakati huo ndio Tony alikuwa akiwasili kituo cha polisi na kuomba aonane na Nancy, mfuko wake wenye chakula kilichouwa ana sumu ambacho yeye aliamini kilikuwa na dawa ya kuondoa Yamini ili kumweka Nancy huru ulikuwa mkononi mwake.
Hakuelewa hata kidogo kwamba alibeba sumu, angejua asingempatia chakula hicho Nancy! Hakumchukia, alimpenda na alikumbuka wema aliomfanyia, bila yeye maisha yake yasingekuwa hapo alipokuwa!
Katu asingeweza kumuua mtu aliyemtendea mambo mema katika maisha yake, alichotaka kufanya ni kumwondolea Nancy kiapo cha hatari alichokula ili akitaka kuwa na uhusiano na mwanaume mwingine kusiwe na kizuizi chochote.
“Kula basi mama!” Tony alizidi kumbembeleza Nancy ili ale chakula, alitaka sana jambo hilo litokee ili Nancy aweze kumchukia na kumwacha ili atafute mwanaume mwingine, hakuelewa ndani ya chakula hicho kulikuwa na sumu mbaya ya kuua taratibu.
“Nafikiri umenielewa kuwa nitakula kwa sababu nina njaa vinginevyo nisingekula kabisa, umeniudhi sana Tony na sijui baba yangu utamwambia nini siku mkikuta....!” Hakuimaliza sentensi hiyo kwikwi ya kulia ikamkaba tena.
Kwa dakika kumi na tano nzima, Nancy aliendelea kulia huku Tony akizidi kumbembeleza ili ale chakula, kwikwi ilikuwa imemkaba kooni, asingeweza kufungua mdomo wake na kula chakula ndani yake, alikuwa na hasira kali isiyopimika.
“Watu wa namna yenu ndio watu huwa wanawaua!” Aliongea Nancy huku akivuta sahani ya chakula karibu yake tayari kwa kula.
“Samahani mpenzi! Najua nimekukosea lakini uwe tayari kunisamehe, naomba ule ushibe kisha tuanze kuongea!”
“Sawa Tony lakini....!”
****
Kulwa alikuwa akitoka ofisini kwa kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Beijing, jasho lilikuwa likimtoka! Alikuwa amepewa barua nyingine kwenda nayo kituo cha polisi cha kati, kilichoitwa Central Beijing Police station! Mfumo wa polisi wa China ulikuwa sawasawa kabisa na Bongo, urafiki wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa China, Mwanamapinduzi Mao Tse Tung ulifanya mambo mengi kati ya nchi hizi mbili yafanane.
“Vipi?” Dereva wake alimuuliza.
“Ilishakuwa shughuli!”
“Kwanini?”
“Yule msichana ana hatia lakini serikali ya China haitaki kumfunga kwa sababu ya uhusiano wa nchi zetu! Ukizingatia suala lenyewe ni la mapenzi na msichana mwenyewe ametendewa kitu kibaya, polisi wameamua tumchukue tumrudishe nyumbani leo usiku!”
“Afadhali, maana kwa sheria za hapa lazima angekwenda jela sio chini ya miaka mitano!”
Gari liliondoka makao makuu ya polisi kwa kasi ya ajabu, kuelekea kituo cha polisi cha kati cha Beijing, ilikuwa ni lazima Nancy asafirishwe chini ya uangalizi maalum usiku huo huo kurudi nyumbani Tanzania, kila kitu kilishaandaliwa, saa tatu na nusu ndege ilikuwa inaondoka Beijing kuelekea Hong Kong na baadaye Dubai, Nairobi ambako Nancy angepandishwa katika ndege ya shirika la ndege la Kenya, KQ na kuwasili Dar es Salaam masaa arobaini na nane baadaye.
Kulwa aliwasili kituoni akiwa na barua na kuingia nayo moja kwa moja ofisini kwa mkuu wa kituo na kumkabidhi! Alipoisoma alielewa kila kitu kwani tayari alishapewa taarifa, alimwita mmoja wa maaskari waliokuwepo mapokezi au Charge room office, CRO kama ilivyoitwa na maaskari na kumwamuru amwite Nancy kutoka mahabusu, askari huyo alinyoosha moja kwa moja mahabusu lakini hakumkuta na kurudi tena hadi mapokezi.
“Yuko kwenye kile chumba cha kuongea na wageni!” Askari mmoja aliyekuwa mapokezi alisema.
Bila kuchelewa askari aliyetumwa aliondoka akikimbia kuelekea chumba alichoelekezwa, alipofungua mlango Nancy alikuwa nyuma ya meza akisogeza sahani iliyokuwa na chakula ili ale, alimwonyesha ishara huku akiongea Kichina maneno yaliyokuwa na maana, Nancy aache kwanza kula chakula kwani alikuwa akihitajika na bosi ofisini kwake lakini Nancy hakuelewa alichokuwa akielezwa, alizidi kuvuta sahani yake! Kwa kipindi hicho alimchukia kila mtu.
“Stop eating dha food!”(Acha kula chakula!) Aliongea Mchina kwa kiingereza chenye lafudhi ya Kichina moja kwa moja.
“Why?”(Kwanini?) Tony aliuliza.
“ Dha boss is need her!”(Mkuu anamhitaji!) Mchina aliendelea kuivunjavunja lugha ya wenyewe bila huruma, huku akimvuta Nancy kutoka mahali alipokaa na kuanza kuondoka naye kuelekea ofisini kwa mkuu wa kituo.
“This is not fair! How can you keep someone without food for more than three hours? Despite being told she hasn’t had anything since moning?”(Hii sio sawa! Unawezaje kumweka mtu bila chakula zaidi ya masaa matatu? Pamoja na kuwa umeambiwa hajala kitu toka asubuhi?) Alilalamika Tony.
Lengo lake la kumwondolea Nancy kiapo alichokula Bagamoyo lisingetimia bila binti huyo kula chakula alichokuwa amemletea! Hakuelewa chakula alichokuwa ameleta kilikuwa hatari kiasi gani, laiti angejua angemshukuru Mungu kuona Nancy ameondoka bila kukila.
Ofisini kwa mkuu wa kituo hapakuwa na maongezi marefu, Nancy alitambulishwa kwa Kulwa Mwaibale na kuelezwa ni kwanini kijana huyo kutoka ubalozi wa Tanzania nchni China alikuwa kituoni pia alielezwa adhabu ya kosa alilokuwa ametenda na alitakiwa kuelewa kuwa uhusiano wa Tanzania na China ulikuwa umemsaidia.
“Siwezi kuondoka, nasema siwezi! Lazima niongee na Tony pengine tunaweza kuelewana” Aliongea Nancy kwa kiswahili akimwambia Kulwa ambaye alimtafsiria mkuu wa kituo nini kilichokuwa kikisemwa.
“Itabidi uondoke! Hii ni amri na si ombi, tunafanya hivi kukusaidia vinginevyo ungekwenda Jela miaka mitano!”
“Sitaki! Kama ni jela nipelekeni lakini nisikae mbali na Tony, ninampenda na yeye ananipenda! Amezuzuliwa tu na penzi la yule Malaya, naamini anaweza kubadilika!” aliongea Nancy akilia.
Hakuna aliyemsikiliza tena, wote walimwona amechanganyikiwa kwani kilichokuwa kikifanyika wakati huo kilikuwa ni kinyume kabisa cha sheria za China ila kilitendeka kwa ajili ya kumsaidia yeye! Mkuu wa kituo aliita askari wawili kutoka mapokezi walioingia muda mfupi baadaye na kuamriwa kumkamata Nancy haraka iwezekanavyo.
Hilo lilifanyika, akapigwa pingu mikononi na kutolewa kituoni chini ya ulinzi mkali, nje kabla hajapakiwa ndani ya gari la polisi alimwona Tony akiwa amesimama pembeni, roho yake ilimuuma sana! Bado alimpenda Tony haikuwa rahisi hata kidogo kumfuta akilini mwake pamoja na yote yaliyotokea.
“Love you Tony! And will always do! Please dont do that to me, you know I love you and will never get you out of my mind!”(Nakupenda Tony! Na nitakupenda siku zote! Tafadhali usinifanyie hivyo, unajua nakupenda na sitakutoa akilini mwangu!)
“I’m sorry Nancy! It’s not me but Mimi, she force me into a relationship that I can not simply pop out at the moment! Anything that happened between you and I is history now, I’m deeply in love with Mimi, you better look for somebody else!”(Samahani Nancy, sio mimi, lakini ni Mimi ndiye amesababisha yote haya, alinilazimisha kuingia kwenye uhusiano ambao hivi sasa si rahisi kwangu kuuacha! Chochote kilichotokea kati yangu mimi na wewe hivi sasa ni historia, ni bora ukatafute mtu mwingine!) Aliongea Tony huku akitabasamu na kumshangaza Nancy, yalikuwa mabadiliko ya ghafla mno na yaliyotendwa na mtu ambaye hakutegemewa.
“NO!NO!NO!NOOOOO! NO TONY! YOU CANT DO THIS TO ME, I LOVE YOU, I LOVE TONY, WITH ALL MY HEART! THAT MIMI IS JUST ANOTHER LAIR, SHE DOESN’T LOVE YOU, PLEASE REMAIN MY BABY! DO YOU STILL REMEMBER WHAT WE DID AT BAGAMOYO?”(Hapana! Hapana!Hapana!Hapaana Tony, huwezi kunitendea hivyo, nakupenda, nakupenda Tony tena kwa moyo wangu wote, huyo Mimi ni mwongo tu, hakupendi! Tafadhali endelea kuwa wangu, bado unakumbuka tuliyoyafanya Bagamoyo?) Aliongea Nancy huku akilia.
Je nini kitaendelea?
Je huu ndiyo mwisho wa kila kitu?
Je Penzi la Tony na Mimi litadumu?