TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA TANO

Mawasiliano kati ya Tony na Nancy yalikuwa yamekatika kabisa, hakutaka kuwasiliana naye kama njia ya kujisahaulisha, kwa wiki kadhaa alikuwa hajaongea na Nancy! Kwa kufanya hivyo aliamini labda angemwondoa kabisa akilini mwake, siku zote alikuwa karibu sana na Mimi, alishaamua kuwa mpenzi wake hapakuwa na njia yoyote ya kumtenganisha naye tena, hakujali mambo yaliyotokea nyuma wala kiapo ambacho Nancy alikula kwa mganga wa kienyeji, aliamini lazima angepata suluhisho na labda angerudi tena kwa mganga ili kiapo hicho kiondolewe.
Ni suala la kiapo hicho ndilo lililomsumbua sana Tony, aliamini ndicho kilimfunga Nancy na kumfanya awe mtumwa kwa mwanaume mmoja, lilikuwa ni kosa kubwa sana kumlisha Nancy kiapo hicho kwani asingeweza kuwa na mwanaume mwingine tofauti na yeye wakati tayari alikuwa na msichana mwingine ambaye kwa uhakika ndiye angekuwa mke wake.
“Kinachonisumbua mimi akilini mwangu si kingine ni kiapo alichokula!”
“Hilo sio tatizo! Ziko dawa Nigeria naweza nikaenda kukuletea, ukimpa akala kiapo chenu kinatoka!”
“Kweli?”
“Sina sababu ya kukudanganya, tofauti na hivyo akikutana na mwanaume mwingine bila kiapo kuondolewa atakuwa mwehu au hata kufa kabisa!”
“Sasa kwanini usiende Nigeria kuniletea hiyo dawa ili ukirudi nami nipange safari ya kwenda Tanzania kumweleza Nancy msimamo wangu baada ya kuwa nimemlisha hiyo dawa utakayoleta?”
“Inawezekana!”
“Basi fanya hivyo ili wiki ijayo mimi niende Tanzania!”
“Nitaondoka kesho!”
Hivyo ndivyo ilivyokuwa, Mimi alipanda ndege kurejea Nigeria kufuata dawa, alibeba siri kubwa kifuani mwake ambayo Tony hakuielewa, msichana huyu alifikiria mauaji ili kumwondoa mtu waliyegombania naye mwanaume, Nancy! Mpaka wakati huo alikuwa haamini kama kweli alikuwa amempata Tony moja kwa moja, hali haikuonyesha hivyo, alihisi hapakuwepo na mapenzi ya dhati bali Tony alimkubali kwa sababu ya pesa zake, kwa kumwondoa Nancy alikuwa na uhakika Tony angekuwa wake milele.
Hakwenda Nigeria kama alivyoaga, akiwa Misri alibadilisha ndege na kupanda nyingine iliyompeleka hadi Marekani ambako aliwaona wataalam wa kutengeneza sumu za kuua taratibu na kuwaomba wamuuzie sumu hiyo kwa matumizi yake binafsi! Hawakukataa baada ya kuwashawishi kwa pesa nyingi, akawa ameuziwa sumu hiyo na kuondoka nayo.
Siku nne baadaye alirejea tena nchini China ambako kabla ya kufika shuleni alinunua unga wa miti shamba na kuuchanganya na sumu aliyokuwa nayo, ilikuwa ni sumu kidogo sana yenye uwezo wa kuua mara iingiapo katika damu ya binadamu, huua chembechembe za damu kidogokidogo na hatimaye kuzimaliza kabisa, mgonjwa hupungua mwili na baadaye hugundulika ana kansa ya damu ama Ukimwi! Sumu hiyo ilitumiwa sehemu mbalimbali kufanya mauaji bila muuaji kugundulika, ilikuwa ni sumu ambayo haijagunduliwa na watu wengi.
Tony alifurahi kumwona Mimi amerejea na kumkabidhi dawa aliyokuwa amefuata, kilichofuata ni yeye kupanga safari ya kuja Tanzania, ilipangwa siku tatu baadaye! Kwa dawa aliyokuwa nayo alikuwa na uhakika Nancy angekuwa huru kuolewa na mwanaume mwingine, hivyo ndivyo Mimi alivyomweleza, hakumtajia kabisa kwamba ilikuwa ni sumu na kwa kumpa Nancy unga huo wa dawa za kienyeji angekuwa anamuua mtu asiye na hatia! Pamoja na Tony kuamua kumwacha Nancy hakumchukia, asingeweza kufikiria kumuua bali alitaka waachane kwa njia za amani.
“Hiyo itasaidia sana! Utakachofanya ni kumchanganyia katika chakula bila kumtaarifu, baada ya tu ya kula utaona amebadilika kabisa, wala hataonyesha nia ya kuwa na wewe tena, isitoshe tangu siku hiyo atakuwa na uhuru wa kuwa na mwanaume yeyote amtakaye!”
“Kweli?”
“Hakika!”
“Basi acha kesho kutwa niende Tanzania, nikamalizana naye!”
Dakika ishirini baadaye wakiwa bado katika maongezi yao tena wote wakiwa kitandani, simu chumba kwa Mimi ambako Tony alikuwa amehamia ili kuzikimbia simu za Nancy iliita, Mimi aliinyanyua na kuipokea, ilitoka idara ya mapokezi ya wageni.
“Kuna mgeni wako mapokezi!”
“Mgeni wangu kutoka wapi?”
“Aha sielewi!”
“Hajakueleza?”
“Hajasema ila ni mwanamke! Lazima twende wote, isijekuwa una mwanamke mwingine hapa China!”
“Twende basi!”
Wote wawili walinyanyuka kitandani na kuvaa nguo kisha wakaanza kushuka ngazi kuelekea Mapokezi, Hawakumwona mgeni wao mara moja walipofika ikabidi Tony amuulize msichana wa mapokezi ambaye alinyoosha mkono wake na kusonta kwenye kona iliyokuwa pembeni! Nancy alikuwa amekaa hapo na mizigo yake! Tony alishtuka na kutaka kurudi nyuma, jambo lililomshtua Mimi.
“Kwanini unataka kurudi nyuma?”
“Ni Nancy!”
“Sasa ndio umkimbie wakati ulitaka kumfuata Tanzania?”
“Naogopa!”
“Unaogopa nini?”
“Nashindwa nitamweleza nini!”
“Mbona kitu rahisi, ukishampa ile dawa niliyoleta, yeye mwenyewe atabadilika!”
“Kweli! Lakini kumbuka tulikuwa tunapendana sana na huyu msichana!”
“Bwana usiongelee historia, ongea habari zilizopo!”
“Sasa?”
“Twende!”
“Nitakutambulishaje?”
“Wewe sema mimi ni mwanafunzi mwenzako!”
Wote wawili walijitokeza na kuanza kutembea kuelekea mahali alipokuwa amekaa Nancy akiwa amejiinamia, walifika na kusimama mbele yake na Tony akamwita jina! Nancy akanyanyua kichwa chake kuangalia juu, macho yake yakapambana na sura ya Tony, hakuamini kama alichokuwa anakiona mbele ya macho yake ndicho kilichomfanya asafiri kutoka Tanzania kwenda Beijing! Aliruka na kumkumbatia Tony aliyeonyesha uso wa kutofurahishwa na ujio wake kwa furaha kubwa.
“Mbona umekuja bila kunitaarifu?”
“Nikutaarifu vipi wakati hupokei simu?”
“Sasa ndio ukaamua kuja tu?”
“Nilitaka kukupa mshangao au Suprise kwa kimombo!” Aliongea Nancy akitabasamu huku macho yake yakiwa yamemwangalia msichana aliyekuja na Tony.
“Na huyu ni nani mbona hunitambulishi?

“Ni mwanafunzi mwenzangu tunasoma naye!”
“Anaitwa nani?”
“Anaitwa Mimi!”
“Huyu ndiye Mimi?”
“Kwani unamfahamu?” Badala ya kujibu Tony aliuliza swali.
“Mbona kachoka namna hii? Au umebabaika kwa sababu ni Mmarekani?”
“Nimebabaika kitu gani?”
“Tony! Tony! Tony! Taarifa zako zote ninazo, kumbuka tulikotoka mimi na wewe na usisahau kuwa mimi nilikula yamini kwa mganga wa kienyeji, usifikirie kuniacha Tony, siwezi kuwa na mwanaume mwingine nilishakula kiapo!” Aliongea Nancy kwa ukali.
“What the shit is she talking about!”(Anaongea upuuzi gani?) Mimi aliuliza akimwangalia Nancy kuanzia juu hadi chini.
“Hey! You whore, how do you dare call what comes out of my mouth shit?”(Hey! Wee malaya unawezaje kuyaita maneno ninayoyaongea upuuzi?) Nancy aliuliza kwa ukali akimsogelea Mimi, dakika mbili baadaye walikuwa chini Nancy akiwa amekaa juu ya Mimi, ngumi mfululizo zikitua usoni kwake! Watu walifika na kusaidiana na Tony kumwondoa Nancy aliyekuwa akilia kwa hasira.
Taarifa zilishafika ofisini kwa mlezi wa wanafunzi na Tony, Nancy na Mimi waliitwa kuhojiwa, Tony alimtambua Nancy kama mgeni wake kutoka Tanzania, alipotakiwa kueleza chanzo cha ugomvi alishindwa ndipo Nancy akaeleza kila kitu waziwazi, alilaumiwa kwa kitendo chake cha kupigana mbele ya kadamnasi kilichotafsiriwa kosa kisheria nchini China.
“Kwa hali aliyonayo Mimi itabidi apelekwe hospitali na lazima taarifa itolewe polisi!” Alisema mlezi wa wanafunzi.
Simu ilipigwa kituo cha polisi cha chuo kikuu cha Beijing na polisi wakafika na kumchukua Nancy hadi kituoni ambako alihojiwa, alikiri kupigana lakini aliielezea vizuri sababu iliyopelekea yeye kutenda kosa hilo. Sababu yake haikutosha kufanya polisi wamwachie huru akatupwa mahabusu na taarifa za kuwepo kwa Mtanzania mikononi mwa polisi zikapelekwa kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini China.
Nancy alilia kupita kiasi, hakuamini kama mtu aliyempenda kupindukia angeweza kumtendea jambo hilo, ilikuwa ni kama ndoto! Aliamini baadaye labda baadaye angezinduka na kukuta mambo yakiwa kama yalivyokuwa awali lakini haikuwa hivyo, ukweli uliendelea kuwa ukweli! Alishinda mahabusu hadi jioni bila kumwona Tony, alikumbuka nyumbani, aliwakumbuka wazazi wake na alishindwa kuelewa ni nini angefanya kumsahau Tony na kukiondoa kiapo alichokula ili aweze kuwa huru tena jambo ambalo kwake halikuwa rahisi.
Alikuwa ameumia tena kupindukia, hakutegemea maishani mwake kumpenda mwanaume tena na hicho ndicho alichouahidi ubongo wake, kamwe asingempenda mwanaume kwa sababu alikuwa ameumizwa na mwanaume, aliwaona viumbe wote wenye jinsia tofauti na yake si binadamu wa kawaida, kwamba hawakuwa na huruma hata kidogo.
Wakati akiteseka mahabusu, Tony aliyesaidiwa na baba yake Nancy kusoma hadi kufika chuo kikuu, alikuwa amekumbatiwa na Mimi kitandani akimfariji na kumwomba msamaha kwa mambo yaliyotokea! Mimi alikuwa akilia kwa uchungu na kumlaumu Tony kwa kila kitu, mwisho kabisa alimsamehe na kumwomba Tony ampelekee Nancy dawa aliyoileta huko mahabusu alikokuwa ili kuepusha matatizo.
“Sawa! Ulisema ni ya kuchanganya kwenye chakula?”
“Ndiyo! Nenda kanunue chakula chochote cha majimaji na uweke ndani yake unga niliokupa, akila tu tayari mambo yatakuwa yamebadilika! Hatakuwa na hasira tena dhidi yangu au yako na baada ya hapo atakuwa huru kufanya lolote maishani mwake, vinginevyo ataendelea kutusumbua maishani mwetu, anaweza hata kuniua!”
Tony hakusema kitu tena, aliondoka chumbani kwa Mimi na kwenda chumbani kwake ambako aliuchukua unga ulioletwa na Mimi na kushuka nao hadi kwenye mgahawa wa chuo ambako alinunua viazi vilivyosagwa, akamwaga nusu ya unga wa miti aliokuwa nao ndani yake akiamini ni dawa ya kuondoa kiapo cha yamini alichokula Nancy huko Bagamoyo, alikuwa amedhamiria kuachana naye na kuwa na Mimi.
Hakutaka tena kurudi bwenini, alichofanya ni kuondoka moja kwa moja hadi kituo cha polisi na kuomba kumwona Nancy akidai alikuwa amemletea chakula na alitaka kuongea naye, polisi hawakuwa na tatizo juu ya hilo, walimruhusu akaingia ndani ya kituo na kuonyeshwa chumba maalum ambako Nancy aliungana naye muda mfupi baadaye akilia kwa uchungu.
“Nisamehe Nancy! Nitabadilika, tunahitaji kuongea juu ya jambo hilo lakini hata hivyo kula kwanza chakula, nitakueleza kila kitu juu ya msimamo wangu, nakupenda Nancy lakini.....!”
“Lakini kitu gani?”
“Kula kwanza!”
“Nitakula kwa sababu nina njaa!”
“Na mimi pia nataka ushibe kabla sijakueleza ninachotaka kusema!”
Je nini kitaendelea?