TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA NNE

Gari lilifika na kuegeshwa tena nyumbani kwa mzee Katobe na wote wawili wakashuka na kuanza kutembea kuelekea ndani, mzee Katobe akiwa mbele Tony akimfuata nyuma, walinyoosha moja kwa moja hadi chumbani kwa Nancy na kuingia ndani! Nancy hakuyaamini macho yake aliruka kutoka kitandani na kumkumbatia Tony huku akilia machozi, mzee Katobe hakutaka kuendelea kukaa ndani ya chumba hicho aliondoka na kuwaacha Nancy na Tony peke yao.
“Nisamehe Tony! Sikuwa mimi, bali moyo wangu! Nakupenda sana na sijui kama naweza kubadili mawazo, imekuwa ghafla mno lakini siwezi kujizuia”
“Hata mimi nakupenda Nancy! Lakini tungeweza kusubiri kidogo, ni mapema mno kwetu kuanza mapenzi na isitoshe wewe unamfahamu vizuri baba yako, akielewa mimi na wewe tuna uhusiano huo, mwisho wa maisha yangu utakuwa umefika!”
“Hawezi kuelewa!”
“Huwezi kuwa na uhakika Nancy, ni bora suala hili tukalipa muda zaidi! Sasa hivi tuzingatie masomo!”
“Sawa lakini...” Aliongea Nancy akiwa amemkumbatia Tony na katika hali ya kushangaza Tony alishtukia ulimi wa Nancy ukiingia mdomoni kwake, hakuweza kukataa aliupokea kama alivyotakiwa na dakika chache baadaye walijikuta wakielea katika anga ya mapenzi.
“.....itabidi tu tuwe wapenzi Nancy!” Tony alikiri na kumshangaza Nancy, msisimko alioupata haukuwa wa kawaida na muda mfupi baadaye waliachana Tony akanyoosha chumbani kwake kulala.
****
Maisha yaliendelea kama kawaida mpaka wakamaliza darasa la saba, mapenzi kati yao yakiwa ni siri kubwa ambayo haikushtukiwa na mzee Katobe wala mkewe na cha kushangaza zaidi mapenzi yalishabadilisha kibao, Tony alikuwa na hali mbaya zaidi kuliko Nancy! Alimpenda kupita kiasi na aligombana na vijana walioonekana kumfuatafuata Nancy wakimtaka mapenzi.
Ulikuwa ni wivu usio na kipimo, mara kwa mara walikwaruzana sababu ya wanaume! Nancy alikuwa mwaminifu kupita kiasi kwa Tony, hata siku moja hakufikiria kumvunjia heshima! Yote hayo yaliendelea wakati wazazi wao wakiwachukulia kama mtu na dada yake.
Mwaka ulioufuata walijiunga na shule ya sekondari ya Bagamoyo ambako walisoma pamoja mpaka kidato cha nne, uzuri wa Nancy uliongezeka maradufu! Usumbufu toka kwa walimu na wanafunzi nao pia uliongezeka na kuzidi kumpa wasiwasi Tony, kijana huyu hakujiamini kuna wakati aliona kama hakustahili kuwa na mpenzi kama Nancy kwa sababu ya umasikini wa familia yake kwani watoto wengi wa matajiri walimfuatafuata mpenzi wake.
“Usiwe na wasiwasi Tony! Siwezi kukusaliti, wewe ni wangu tu mpaka maisha yangu yote!” Hayo ndiyo yalikuwa maneno ya Nancy kwa Tony kila siku.
“Siamini!”
Mpaka wanamaliza kidato cha nne na kwenda kidato cha tano na sita katika shule ya Kizunguzi huko Kilosa bado wivu ulimsumbua Tony! Mapenzi yake yalikuwa mazito mno kwa Nancy, kuna wakati alihisi yeye hakupendwa kama alivyopenda.
Pamoja na wivu huo, Tony alikuwa tishio darasani, tangu darasa la kwanza mpaka anamaliza kidato cha sita hakuwahi kushika namba mbili, kila mtihani alikuwa namba moja mpaka kubandikwa na wanafunzi wenzake jina la ‘mtambo’! Mtihani wa kidato cha sita alifanya miujiza na serikali ikaamua kumpa nafasi ya kusomea udaktari katika chuo kikuu cha Beijing huko China!
Nancy pia alifaulu vizuri na kupata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya Sheria, pamoja na hizi kuwa habari njema kwao zilikuwa za kusikitisha kwani zilimaanisha kuwatenganisha, badala ya kufurahi Tony alikesha akilia kwani alikuwa akitenganishwa na mpenzi wake kwa miaka saba!
“Usiwe na wasiwasi utanikuta Tony!”
“Siwezi kuamini, wewe ni mzuri mno Nancy! Wanaume wengine watakuona na utaniacha!”
“Haiwezekani! Nitakusubiri Tony, nakupenda kwa moyo wangu! Kama ni wanaume mbona kila siku nawaona?”
“Sawa, lakini miaka saba ni mingi sana Nancy!”
“Usiwe na wasiwasi mpenzi, amini nakupenda Tony na nitakusubiri, nipo tayari kufanya lolote kukuhakikishia kuwa utanikuta!”
“Kweli unaweza kufanya lolote?”
“Ndiyo!”
“Kesho twende mlingotini!”
“Kufanya nini mpenzi?”
“Kwa mganga ukale yamini!”
“Yamini ni nini hiyo?”
“Kiapo! Ili kama ukifanya mapenzi na mtu mwingine kabla sijarudi udhurike”
“Hiyo tu mbona kitu kidogo, nakupenda sana Tony hata sasa hivi twende!” Aliongea Nancy kwa kujiamini.
“Hamna tatizo tutakwenda kesho!”
“Ok!”
Siku iliyofuata walifanya kama walivyopanga, wakaenda kwa mganga na kueleza shida yao! Kama kawaida mganga alimweleza Nancy madhara ya kitu alichokuwa anataka kukifanya.
“Binti kama huna uhakika kwamba utavumilia usifanye hiki kitu ni hatari!”
“Mbona ni kitu kidogo mzee, uamuzi wa kufanya mapenzi ni wa mtu binafsi!” Aliongea Nancy kwa kujiamini na mambo yalifanyika, wakaondoka kwa mganga Tony akiwa ameamini anakwenda China kusoma na atamkuta mpenzi wake.
“Lakini mbona wewe haukula yamini?”
“Ah! Mimi ni mwanaume bwana!”
“Nyie wanaume wajanja sana, si ajabu wewe utakuwa unafanya!”
“Siwezi!”
*****
Wiki mbili baadaye Nancy alimwaga machozi uwanja wa ndege wa Dar es Salaam akimsindikiza Tony, akawa ameondoka na kumwacha Nancy akijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam, ilikuwa huzuni kubwa sana mioyoni mwao wote wawili.
Tony alitua Beijing baada ya masaa ishirini na nne na kwenda moja kwa moja chuoni, alikuwa bado akitokwa na machozi! Kumbukumbu za Nancy zilikuwa bado zikimtawala kichwani mwake, miaka saba mbali na mpenzi wake haikuwa kidogo! Ilikuwa ni sawa na mtoto kuanza darasa la kwanza mpaka kumaliza la saba.
“Ili mradi amekula yamini nitamkuta!” Aliwaza Tony.
Chuoni alipokelewa na msichana aliyeitwa Mimi, alikuwa mchanganyiko wa Mnaigeria na Mmarekani, Tony alishangazwa na uzuri wa msichana huyo, hakutegemea kukuta msichana mzuri kama huyo katika nchi ya Wachina.
“You’re beautiful Mimi!”(Wewe ni mzuri Mimi!)
“You’re handsome as well Tony!”(Wewe ni mzuri pia Tony!)
Walisoma darasa moja na waliishi bweni moja ingawa vyumba tofauti.
****
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Nancy alipokelewa na kijana wa Kichaga aliyeitwa Daniel, wengi walimwita Danny. Alikuwa kijana mrefu, mwenye kifua kilichojaa na mikono iliyotuna! Alikuwa na macho malegevu na midomo ya duara, kifupi hakuna mwanamke angemwona Danny akaacha kusisimkwa na mwili!
“Nancy, kwanini kila siku unalia?”
“Namkumbuka rafiki yangu wa kiume!”
“Yuko wapi?”
“Beijing!”
“Asiyeko machoni na moyoni mfute! Nitakufanya umsahau”
“Danny usirudie tena kuniambia hivyo siku nyingine! Tutakosana kabisa!” Alifoka Nancy.
Nancy na Danny walisoma darasa moja na waliishi bweni moja ingawa vyumba tofauti! Danny aliapa kumpata Nancy kwa njia na kwa gharama yoyote ile.
Je nini kitaendelea?