TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA TATU

Jioni ya siku hiyo mama yake alitayarisha chakula wakala pamoja na baadae kusali kisha kulala, siku hiyo Tony wala hakushika daftari kusoma kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi kupita kiasi, akiwa kitandani majira ya saa tano za usiku alisikia gari likifunga breki nje ya nyumba yao na muda mfupi baadae mama yake akaingia mbio chumbani kwa Tony huku jasho jingi likimtoka, moyo wake ulikuwa ukidunda kwa kasi kubwa kiasi cha Tony kuusikia.
Kitendo hicho kilimfanya Tony ambaye hakushtuliwa na breki za gari hilo ashtuke na kunyanyuka kitandani akihema, alianza kufikiria majambazi lakini baadae aliyatoa mawazo hayo kichwani mwake kwani yeye na mama yake hawakuwa na kitu cha kufanya wavamiwe na majambazi.
“Mama vipi?”
“Kuna gari nje!”
“Sasa wasiwasi wa nini? Si ajabu ni gari la majirani!”
“Hakuna jirani mwenye gari! Ina maana wewe hufahamu? Mimi na wasiwasi!”
“Wa nini? Majambazi? Tuna nini sisi cha kuvamiwa mama?” Aliuliza Tony akifungua dirisha la chumbani kwake kuchungulia nje.
Hakuamini alichokiona, ni kweli mama yake alikuwa na haki ya kutetemeka! Moyo wake ulianza kwenda kwa kasi kubwa, hawakuwa majambazi kama ulivyokuwa wasiwasi wa mama yake, mzee Katobe alikuwa amesimama nje ya nyumba yao mbele ya mlango bunduki yake aina ya SMG ikiwa mkononi na akiitumia bunduki hiyo kugonga mlango. Tony alizidi kutetemeka akielewa wazi kuwa, Nancy kwa hasira zake alikuwa ameamua kumsingizia kwamba alimbaka na kilichomleta mzee Katobe nyumbani kwao usiku huo ilikuwa ni kuja kumuua kwa risasi.
“Nani?”
“Mzee Katobe, nina uhakika kaja kuniua mimi! Kuna kitu kilitokea jana ambacho nimeshindwa kukueleza kwa sababu wewe ni mzazi wangu!”
“Kitu gani?”
“Naona aibu! Ila Nancy alinilazimisha, nisingeweza kufanya kitendo hicho kwa sababu wewe kila siku unaniambia kwamba ni dhambi!”
“Nini hicho?”
“Tendo la ndoa!”
“Mama yangu! Na wewe ulikubali?”
“Nilipokataa Nancy alitishia kunishtaki kwa baba yake kwamba nimembaka! Ikabidi nikubali, nilichukia sana na ndio maana nikaamua kurudi nyumbani nilijua wazi kama ningeendelea kubaki nyumbani kwa mzee Katobe Nancy angenilazimisha tena tufanye hivyo hatimaye mzee Katobe angegundua na kuniua, naelewa uamuzi wangu wa kurudi hapa umemuudhi sana Nancy na amenisingizia kwa baba yake kwamba nilimbaka na hivyo mzee Katobe amekuja kuniua kwa risasi, sina la kufanya na siwezi kumzuia asifanye hivyo, nasikitika kwamba muda mfupi ujao nitakuwa marehemu, nitakuacha mama!”
“HODI! HODI! HODI!” Sauti ya mzee Katobe ilisikika huku akiupigapiga kwa kitako cha bunduki mlango wa nyumba yao uliotengenezwa kwa bati.
Hakuna aliyeitika, Tony na mama yake walikumbatiana huku wakilia, ulikuwa usiku wa huzuni kubwa sana kwao na kwa pamoja walianza kumuomba Mungu abadilishe hatma ya kilichokuwa kikija mbele yao, wakiwa katika maombi hayo ghafla mlango wa nyumba yao uliofungwa kwa msumali uliokunjwa ulifunguka na nyayo za mzee Katobe zikasikika sebuleni. Waliendelea kububujikwa na machozi bila kujua la kufanya.
“Siwezi kukubali akuue mbele ya macho yangu, nipo tayari kufa mimi lakini wewe ubaki hai!” Mama yake Tony aliongea kwa huzuni.
Tony na mama yake walikuwa wakitetemeka wakiwa nyuma ya mlango uliokuwa ukigongwa kwa nguvu zote na mzee Katobe, akitumia bunduki yake aina ya SMG huku akiita jina la Tony pamoja na la mama yake! Hakuna aliyeitika wakijua alikuwa amekwenda nyumbani kwao kufanya mauaji.
“Mama nasikitika nakufa, laiti ningejua nisingekubali kwenda nyumbani kwao na Nancy, najua amenisingizia kwa baba yake kwamba nilimbaka na kwa sababu hiyo mzee Katobe amekuja kuniua!”
“Hawezi kukuua mwanangu, nitapambana naye labda atuue sote wawili!”
“Lakini ana bunduki!”
“Hata kama!”
Mlango ulizidi kugongwa kwa nguvu lakini hawakudiriki kuitikia wala kuufungua, ghafla ulianza kusukumwa, bahati mbaya sana haukuwa na komeo imara, ulifungwa kwa msumari uliokunjwa! Taratibu ukaanza kuachia, Tony na mama yake hawakuwa na uwezo wa kuzuia tena, walichofanya ni kusogeleana na kukumbatiana wakisubiri lililokuwa likija mbele yao.
Mlango ulivunjwa na mzee Katobe akaingia hadi ndani bunduki yake ikiwa mkononi, miili yao ilikufa ganzi! Tony aliamini kifo chake kilikuwa kimefika na hata mama yake aliwaza vivyo hivyo, alikuwa tayari kupambana kuzuia mwanae asidhuriwe na katika kufanya hivyo alielewa na yeye angeuawa!
“Ee Mungu tusaidie!” Walijikuta wakitamka wote kwa pamoja.
***
Nancy alikuwa katika mapenzi mazito na Tony kwa kilichotokea siku moja, lilikuwa ni jambo ambalo hakulitegemea kabisa kwani lilianza kama mchezo, lakini ghafla moyo wake tayari ukawa umetekwa na kumfanya aamini maisha bila Tony yasingewezekana!
“Nampenda Tony, hilo halina ubishi!” Aliwaza Nancy akitembea kuelekea nyumbani, siku hiyo alikuwa peke yake tofauti na siku zingine zote alizoongozana na Tony.
Alirudi nyumbani kutoka shuleni akilia, kitendo cha Tony kurejea nyumbani kwao kilimuumiza sana, alielewa yeye ndiye alikuwa chanzo cha tatizo hilo kwa kumshawishi kufanya tendo la ndoa jambo ambalo Tony hakulipendelea, alikuwa na uhakika alishiriki kwa sababu tu alimtishia kumshtaki kwa baba yake kuwa alitaka kumbaka kama tu angekataa kumtimizia shida yake.
Nyumbani kwao hakutaka kuongea na mtu, baada ya kumsalimia mama yake ambaye alikuwa nyumbani wakati anawasili, Nancy alinyoosha moja kwa moja hadi chumbani kwake akajifungia na kuendelea kulia akimfikiria Tony.
Muda mfupi baadaye mlango uligongwa na aliposikiliza sauti aliyeongea nje aliitambua, alikuwa mama yake, alinyanyuka taratibu akausogelea mlango na kuufungua, mama yake alipomwangalia usoni aligundua kulikuwa na tatizo.
“Mbona macho mekundu?”
“Naumwa!”
“Unaumwa nini?”
“Kichwa!”
“Umekunywa dawa?”
“Ndiyo!”
“Dawa gani?”
“Panado na ningeomba uniache nipumzike mama!”
“Mwenzako yuko wapi?”
Badala ya kujibu swali hilo Nancy aliangua kilio mbele ya mama yake na kumhakikishia kabisa kwamba kulikuwa na tatizo lililomsumbua kichwani mwake, badala ya kuondoka mama yake aliketi pembeni mwa kitanda akitaka kufahamu nini kilichotokea kati ya Nancy na Tony.
“Nini kimetokea? Amekupiga?”
“Hapana!”
“Sasa kwanini nilipotaja jina lake ukalia?”
“Nasikitika kwa sababu Tony ameamua kurudi kwa mama yake, wakati mimi bado namhita-ta-ta-taji...!” Alisema Nancy huku kwikwi ya kulia ikiwa imemkaba.
“Kwanini ameamua kurudi?”
“Nilimkosea!”
“Kosa gani?”
“Siwezi kusema mama!”
“Kwanini?”
“Basi tu, mimi naomba mumfuate nije nimwombe msamaha!”
“Bahati mbaya nyumbani kwao sikufahamu, baba yako peke yake ndiye anapaelewa! Tumsubiri arudi! Lakini nataka kufahamu umemkosea nini?”
“Siwezi kusema hata kama kisu kiko shingoni kwangu!” Aliongea Nancy na kumtisha mama yake.
Mama yake alimfariji kwa kama nusu saa nzima, alipotulia aliondoka chumbani kuelekea jikoni ambako aliendelea na kazi za ndani akisaidiana na wafanyakazi mara kwa mara akienda chumbani kwa Nancy kuhakikisha alikuwa salama, mzee Katobe hakurejea mpaka saa tano za usiku na mkewe kumweleza wazi juu ya jambo lililotokea.
“Kwa hiyo nikimleta Tony, hutalia tena?” Mzee Katobe aliuliza akiongea na Nancy chumbani kwake.
“Ndiyo baba!”
“Ok! Wache nimfuate!” Aliongea mzee Katobe na kuondoka chumbani kwa Nancy kwenda chumbani kwake ambako alichukua bunduki yake aina ya SMG na kutoka hadi nje ambako aliingia ndani ya gari lake na kuliendesha hadi nyumbani kwa mama yake na Tony eneo la Magomeni.
Alifika na kuanza kugonga mlango lakini hakuna aliyemwitikia, hatimaye akafikia uamuzi wa kuvunja mlango wa bati uliokuwepo ili aingie ndani na hilo likawezekana tena kwa urahisi kwa sababu mlango haukuwa na ugumu wowote, akaingia hadi ndani na kuwakuta Tony na mama yake wakiwa wamekumbatiana.
“Msiogope ni mimi! Mlifikiri ni majambazi?” Aliuliza mzee Katobe lakini bado hawakumjibu kitu chochote waliendelea kukumbatiana wakisubiri risasi zipenye miilini mwao.
“Tony! Tony! Tony!” Mzee Katobe aliendelea kuita.
“Naam!” Tony alijitutumua na kuitika.
“Kwanini nawagongea hamfungui mlango mpaka nimeuvunja? Basi tutautengeneza tena mlango mwingine!” Aliongea mzee Katobe kwa sauti ya upole.
Mara moja Tony alielewa kilichomleta mzee Katobe nyumbani hapo hakikuwa kufanya mauaji, kulikuwa na kitu kingine! Hofu aliyokuwa nayo moyoni ilifutika kwa furaha na kujikuta amesimama wima huku akimwomba mama yake pia asimame.
“Shikamoo baba!”
“Marahaba hujambo Tony? Mnaogopa sana majambazi au siyo?”
“Sana! Na hatukufahamu kabisa unaweza kuwa wewe, sisi tulijua ni maharamia wametuvamia!” Aliongea Tony meno yake yakigongana.
“Hata mimi nilihisi hivyohivyo! Sasa labda nieleze shida iliyonileta na nitaanza kwa kuuliza swali ni kwanini leo hukuja nyumbani mwanangu?” Aliuliza mzee Katobe.
Tony alishindwa kulijibu swali hilo haraka, alitulia kwanza akijaribu kutafakari nini alichotakiwa kusema, asingeweza kutoboa siri ya jambo lililofanyika kati yake na Nancy, alikuwa na uhakika mzee Katobe hakuwa na taarifa juu ya ngono iliyotendeka, kama angekuwa na fahamu asingekuwa katika hali aliyokuwa nayo usiku huo.
“Kwanini umeondoka nyumbani?”
“Nilikuja kumsalimia mama!”
“Mbona mwenzako amesema kuna matatizo na anataka akuombe msamaha?”
“Amesema ni matatizo gani baba?”
“Hakutaja lakini anakuhitaji na ndio maana nimekufuata!”
“Lakini mimi nataka kubaki na mama!”
“Nancy analia sana, anakuhitaji nyumbani upesi tafadhali twende!”
Moyo wa Tony ghafla ulishikwa na huruma aliposikia Nancy alikuwa akilia mfululizo na alipomwangalia mama yake usoni alipokea ishara ya kumtaka akubali kuondoka, hakutaka kukataa tena ili mradi mama yake alikuwa ameridhia.
“Sawa twende baba! Mama kwaheri!”
“Haya nenda mwanangu, ukaishi huko huko na usome shule, unaniona mimi hali yangu ilivyo! Sina uwezo wa kukusaidia lolote, mshukuru Mungu amekupa mzee Katobe akusomeshe!” Aliitikia mama yake wakati Tony na mzee Katobe wakitembea kuelekea nje, hali ilishabadilika hapakuwa na hofu tena na hawakutaka kumwonyesha mzee Katobe jambo walilokuwa wakifikiria kabla hajaingia ndani.
“Usiwe na wasiwasi mama, nitamsomesha mtoto wako mpaka mwisho ili mradi tu waendelee kuelewana na mwanangu Nancy!”
Je nini kitaendelea?