TAFUTA HAPA

HADITHI:Utamu wa Sukari Guru -5

HA ha ha Shemeji, mbona utateseka. Angalia usijiapize unaweza kufa lazima nije na kuna siku nitakuja bila kualikwa, na ukiona nimefika na mkeo hayupo jua nini nitakachofuata, itakuwa kama leo. Kwaheri. Hayo ndiyo maneno ambayo alisema Kibua wakati akijilamba kwa utamu aliouonja wa shemeji yake kwa Semie, Je nini kinaendelea?...

Semei akiwa amechukia kabisa na huku uso umemuiva kwa kushindwa kujua amfanye nini Kibua, huku akijenga taswira ya hasara katika uchumba wake kwani alitambua kwamba mara zote Kibua hutekeleza tishio lake, alianza taratibu kushuka milima kwa njia ile ile aliyokuwa ameijia.
Kibua kwa upande wake alimtazama kwa nyodo jinsi alivyokuwa akishuka akifurahi jinsi alivyomuweza. Alitabasamu.
Kibua kwa namna fulani alikuwa binti ambaye anapenda kuudhi watu hasa wale ambao wamemfanyia visa vinavyomnyima raha na kwa Semei alikuwa amekamilisha alichotaka, lakini kumuumiza zaidi ni alitaka lazima amfumanie na mchumba wake katika kitanda chake, kukomesha ngebe zake.
Alimfuatilia mpaka alipoingia Dawilo, akiwa mdogo katika macho, aligeuka na kuelekea katika chumba chake. Alikitazama chumba kile kisha akaamua kuanza kupanga nguo zake katika sanduku lake la mbao kwani alijua ima faima safari ya kwenda mjini ilikuwa imeiva.
Hakujua anatakiwa kufanyakazi ya aina gani, lakini alijua kitu kimoja tu kwamba mama yake alikuwa anataka aondoke pale ili aweze kupata raha, manake, hakuwa na raha kutokana na jinsi yeye alivyokuwa akiendesha maisha yake.
Alimfikiria huyo mjomba wake ambaye mara zote hajui kama ni mjomba wake kweli au baba yake. Alikuwa ni mtu ambaye akimwangalia hawezi kumtazama moja kwa moja hadi  siku alipogombezwa na mama yake kwamba si vyema kumwangalia mtu mzima kwa macho ya juu juu.
Alipomaliza kukunja nguo na kuziweka katika sanduku alichukua maji akayainjika na baada ya kuchochea kuni na kupata moto aliipua na kuingia nayo chooni , muda wa kujisafi ulikuwa umefika hakutaka kulala na janaba la mtu.
Mwaka ni 1975, Kibua alikuwa amebadilika kidogo na alikuwa ni mtu ambaye  huwezi kumtambua. Alikuwa amekwenda juu kidogo, lakini hakuwa mrefu ki hivyo. Alikuwa na umbile ambalo sasa imekuwa taabu hata  pale alipokuwa anasoma.
Ahh nilisahau kukusimulia kwamba Kibua aliondoka nyumbani kwao siku ile ile aliyogombana na  Semei. Kulikuwa na gari la kahawa lililotoka Kibuko ambalo lilipitia  karibu na kwao na kumsubiri Masarawe. Kama si mama yake asingeliondoka pale kwani yeye kama walivyokuwa Waluguru wengine wa huko mlimani gari la kahawa kwao lilikuwa ni mauaji, lilikuwa ni la mumiani.
Baada ya kupata lifti ile hadi Morogoro alichukua gari la Bin Klebu mpaka Dar es Salaam ambapo alisubiriwa na mjomba wake ambaye alikuwa amefanana naye sana. Aliishi pale kwa muda kabla ya kupata kazi za ndani katika nyumba moja ya  mfanyakazi wa Serikali iliyopo Kijitonyama.
Ni katika nyumba hii ndipo alipopata nafasi ya kuanza kusoma, hakuwa na kichwa kibaya, alikuwa na kichwa kizuri. Kisa cha kuanza kusoma hakikuwa kizuri sana kama unavyofikiria kwamba eti alimpata msamaria na kumwingiza shule la hasha, ilikuwa ni sehemu ya makubaliano kati ya baba mwenye nyumba na yeye.
***
"Hapa sisi tunaishi wawili tu, mtoto wetu  yupo masomoni Chuo Kikuu Makerere na hatumtarajii kurejea hapa mpaka miaka miwili ipite, lakini la maana ni kuwa nyumba hii inahitaji msaidizi," alisema baba mwenye nyumba huku mkewe akiwa anaangalia.
Baada ya kupewa maelezo hayo na kukabidhiwa chumba chake cha kulala nje ya jengo hilo, sehemu ya kota za wafanyakazi, Kibua alianza kazi zake na hakuwa mvivu.
Kwanza akiwa na mke wa mwenye nyumba alijifunza utamaduni wao hasa katika kula na mambo yao mengine. Alikuwa na muda mfupi sana wa kujifunza hasa chakula anachokipenda baba mwenye nyumba, chakula ambacho kilimpa dhiki kwelikweli kukitengeneza. Mama mwenye nyumba alikuwa na muda mwingi wa kumwelekeza mpaka akakijua kwani alikuwa likizo.
Muda haukupita, Kibua alikuwa anajua kujibu simu, japo kwa Kiswahili, akajua ratiba ya nyumba ile, akawa msaada mkubwa kwa mke wa mwenye nyumba, aliyekuwa na utu uzima fulani hivi.
Baba mwenye nyumba ambaye alikuwa na urefu wa futi sita na inchi mbili hivi aliyejengeka katika umbile la uanariadha akiwa hana tumbo linalosababishwa na ukosefu wa mazoezi, sura ya duara, maji ya kunde hakuwa bazazi vile lakini baada ya miezi mitatu wakati akiwa nyumbani wiki moja bila mkewe kuna kichaa kilimpata.
Aliondoka pale na kwenda ofisini kwake na baada ya kumaliza kazi, alikwenda klabu  Msasani na kujipatia kilevi. Baada ya muda wakati akiwa katika bia yake ya Tusker ya  pili, akafika binti mmoja anayemfahamu.
"Ahh Richard upo hapa."
"Si unaniona"
"Toka umeoa Richard ndio basi tena."
"Duhh! unakumbuka sasa miaka 24 na mtoto anamaliza chuo kikuu, Mariana lazima uwe na wazimu."
"Nina wazimu kidogo nimekuona hapa, nimekumbuka kila kitu. Dahh mwanamke mwenzangu lazima awe anajidai."
"Kwani wewe ulikatazwa?"
"Ilikuwa lazima nisome, na wewe ulikuwa unanichanganya ningebaki dakika zaidi ya mia pale siku ya mwisho nilikuwa siendi kusoma."
"Mhh. "
"Kwanini ulikimbilia kuoa?"
"Nilihitaji mtu wa kunisaidia katika matatizo yangu."
"Matatizo yako, wewe ulikumbwa na matatizo gani?"
"Yale uliyokuwa umeyasaidia kuyatengeneza. Kulala wawili haikuwa rahisi na hasa ulipoamua kuondoka, tena bila kuaga nakuja kwenu haupo."
"Ulinichanganya wewe nikawa sina la kufanya. Narudi hapa nakutafuta haupo naenda mahali nasikia jina lako, natafuta habari zako naambiwa umeshaoa na una mtoto wa miaka 10 nikakimbilia Msumbiji."
"Ndio umerejea nini?"
"Wapi nikampata mtu akanipeleka Namibia, tumerejea hapa ninachofanya sikijui hii siku ya tatu nakuja hapa."
"Hukijui unachokitaka ? Hii ajabu sana haiwezi kutoka kwa Mariana."
"Mariana wako amebadilika. Amekua lakini bado nakumbuka ulivyokuwa mtundu. Je nina nafasi?"
"Nafasi kwa mke wa mtu, tena mwambata wa kijeshi. Haa milio ya risasi bado naikumbuka."
"Unapendeza Richard. Sijakusahau. Ulinifanya niwe na amani sasa sina, niliondoka kwa kukuogopa kwani ninapokuwa karibu nawe nahangaika sana, lakini sasa najua woga wangu umenikosesha amani na furaha."
"Wewe unayesema au mwingine."
"Ulijua kuunga wali kwa tui la nazi. Ulijua hili la tatu , hili la pili na hili la kwanza. Ulijua muda Richard, ulijua kuivisha. Ulijua mpaka aina ya ukoko unaoutaka ukajua utandu unakaa muda gani. Na kila ninapokuwa na baba wa mtoto wangu wewe ndiwe umejaa. Niondolee laana uliyoniwekea,"
"Nikuwekee laana? Mimi au?"
"Haiwezekani umenipa nini wewe. Mpaka miaka inapita lakini nakuona katika fasheni ile ile tu. Hapa nilipo nishaharibikiwa. Nikuongeze bia."
"Hapana. Nataka kuwa na akili zangu."
"Kwani huwa zinachomoka?"
"Hii pombe wewe si chai wala maji ya kunywa."
"Bado man of Principle," alitabasamu, tabasamu lililomkera sana Richard ambaye bila kujijua alikuwa nyuma miaka 20, mara tu baada ya kumaliza Tambaza. Mwanamke wake wa kwanza kumpenda kikwelikweli.
"Tuache hayo mbona unakuja ulevini?"
Itaendelea