TAFUTA HAPA

hadithi:Utamu wa Sukari Guru-1

ILIKUWA jioni sana  kwa maana kuku walikuwa wameanza kuingia katika mabanda yao huku, jua likitengeneza rangi ya hudhurungi likionesha wazi kwamba usiku unaingia.
Kila kiumbe kinachotumia mchana kwa ajili ya kazi zake za maendeleo kilikuwa kinajiandaa kurejea kwenye kiota. Katika kundi hilo alikuwapo msichana mmoja mwenye umri wa miaka 18 mwenye urembo wa haja.
Kibua mwenye urefu unaomuondoa katika maumbile ya mabinti wa Kiluguru kwa  mbali, alikuwa kiasi anakimbia kutokana na kulazimika kushuka kwa kasi katika miambao ya milima ambamo barabara imechongwa.
Kibua ambaye alikuwa  ni binti wa pekee nyumbani kwao alikuwa ameshika chupa ya mafuta ya kula ambayo wenyeji wa huku wanayaita uto, akiharakisha kurejea nyumbani.
“kibua” alisikia mtu akimuita, hakutaka kugeuka kwani maeneo aliyokuwa akiyapita ya masarawe kipindi cha jioni huwa na vituko sana.Akakazana tu akasikia tena sauti hiyo, akakazana akasikia tena, sasa akafanikiwa

kuigundua akageuka . Mvulana mmoja katika miaka yake ya 20 hivi au zaidi alikuwa anakimbia kumfuatilia.
Akasimama ajue kulikoni.
Akamfikia hima.
“Mimi naitwa Luwanda, kwetu ni Nyandira naweza kuzungumza nawe kidogo” alisema kwa Kiluguru cha kujiumauma.
Kibua hakumjibu alimkazia macho yake makubwa na kumwangalia.
“Mbona unanitazama hivyo”
Hakumjibu, akageuka na  kuelekea nyumbani kwake sasa akiwa anakimbia kidogo kidogo manake, ilikuwa lazima ale kona ya milima kabla jua halijazama kabisa. Mvulana akaona atalazimika nay eye kuvuta hatua angalau

apate miadi
“Kibua mbona unafanya shida katika hili”
“Unanichelewesha nikusaidie nini”
“Kama hutajali,napenda kuzungumza nawe”
“Kuna shida? Haya zungumza”
“Punguza mwendo basi”
“Siwezi nimechelewa na mama yangu atanipa shida bure”
“Mkubwa wewe. Nitakusindikiza”
“Mimi?Wewe unanijua mimi?”
“Sikujui ndio maana nataka kukujua.Nitakupeleka. Nizungumze nawe kidogo”
“Kunipeleka huwezi. Lakini kama una shida fika kesho saa za mchana katika jabali la Mikongowe nitakuwa nachota maji”
“Kwani hatuwezi kuzungumza hapa”
“Unaelewa au?”
“Basi Kibua mimi si mwenyeji huku kwenu”
“Kama hu mwenyeji umenijuaje?”
“Nimeelekezwa tu.”
“Kama umeelekezwa, rejea ukaelekezwe tena”
Alikuwa anakaribia kona,akaikata kisha akasema:”usipende kufuata watu usiowajua wewe”
Akasimama akaduwaa.
Alifika nyumbani na  kumkuta mama yake akimsubiri.
“Mhh Kibua ushaota mapembe. Yaani hapa na Msewe ni safari ya kwenda Morogoro au Yule mwanaharamu wako amerudi”
“Mamah nini tena unazungumza?”
“Nasema hivi kwanini umechelewa”
“Mafuta nimeyapata mbele zaidi mama sio Msewe!”
“Mwanangu taratibu!” alisema mama.
Kibua alienda zake jikoni na kuanza kuandaa chakula cha jioni akamshangaa mama yake na kelele za mwanaharamu wake. Mwanaharamu wake! Akaguna.
Alipomaliza kupika, akatenga chakula akamuita mama yake wakaenda kula. Hawakuwa na cha kuzungumza siku ile kwani Kibua alimuogopa mama yake,kwani mama yake akishaanza salamu za huyo anayemuita mwanaharamu

wake, huwa akijibu hakuchi, maneno mpaka anakasirika.
Mama yake alikuwa anamzungumzia mvulana aliyemtoa ushamba wakati akiwa darasa la saba ambaye ameenda mjini na wala hajaleta barua tena ingawa alisema kwamba atarejea kumuoa.
Amekataa wachumba wengi, kiasi cha mama yake kukereka na kumwambia wazi kwamba moyo wake ulikuwa umekufa kwa mtoto wa Peter aliyekuwa anakaa Midolowela. Miaka imepita na kwa kuwa hakupata nafasi ya

kwenda sekondari alibaki nyumbani akimsubiri mchumba aliyeondoka.
Baada ya kuona kwamba mchumba mwenyewe harudi alijaribu hapa na pale akaona kila mahali pachungu, pana mwiba na zaidi wavulana waliopatikana walikuwa na haraka sana.
Haraka zao zikawa haja zao na kila anapobaini kwamba wana haraka aliwaacha, akaenda kujilalia
Agosti ya mwaka 1970 saa nne asubuhi, akiwa nyumbani kwake anaota jua  alifika msichana mmoja jirani.
"Dada kuna mtu yupo  kule kisimani kwenye jabali anasema anaitwa Luwanda ana ujumbe wako"
"Luwanda? Unasemaje Chilua"
"Anasema anaitwa Luwanda anatoka huko sokoni" akakumbuka
"Asante mdogo wangu"
Alitoka pale na kuelekea kwenye lile jabali.
Alizunguka  kibonde na kumuona mvulana mmoja aliyempa mgongo, akadhani ndiye aliyemsimamisha jana.
Luwanda alionekana kujiketia kiuvivu kabisa katika jabali hilo kubwa.
Katika eneo lile lenye upweke mkubwa, alionekana kuigeukia mimea inayochoma ambayo kwao walikuwa wakiita siru.
hakujua kufika kwa Kibua pale, kwani mawazo yake yalikuwa yanamtazama mjusi mmoja wa rangirangi akipita kivivu katika mimea ile ambayo ukifanya masikhara ikakuchoma, basi mguu wako ukipona nenda katambike.
Yule mjusi wa rangi alimrukia mdudu mmoja na kummeza, akamshutumu kwa kummeza mdudu yule, mjusi alitoa ulimi wake nje akajilamba, kama anayemcheka.
Ahh! mjusi yule alimtibua na mimacho yake na kujilamba kwake baada ya kumuua mdudu. Aliamua kunyanyuka kuona kama mtu wake anakuja au angoje zaidi.
Alinyanyuka kivivu kabisa huku akiangalia chini ya milima akatazama mji wa Kilima kutoka pale Mikongowe, alipogeuka macho yake yakakutana moja kwa moja na ya Kibua ambaye alikuwa amejaza uso wenye bashasha.
"Nimekuja. Habari za asubuhi Luwanda"
"Nzuri.Umenishtua sikukusikia ukija"
"Mimi si mchawi Luwanda  wewe mwenyewe ulikuwa umejizamia wapi sijui. mjusi alikuwa anakuchanganya, marangirangi yake hayo.Ninapokuwa nimechoka kabisa huja hapa jioni kuona mijusi inavyoota jua la jioni.karibu

nimefika nina muda mfupi sana mama yangu atarudi"
"Nimefika hapa tuzungumze" aliingiza mkono mfukoni akatoa ua la mbaazi.
"Ua la mange? una lako jambo"
 “Una mwili mzuri!”
“Hauwezi kuushindana wa kwako”
“Hapana una uzuri ambao mimi siwezi kuwa nao.”
“Nambie Luwanda umekuja hapa kunambia hilo?”
“Nimekutunuku”
“ Luwanda hii si habari mpya na mimi si mtu mpya kuambiwa hivyo nawe”
“ Kweli kabisa ila ni hadithi ndefu,waweza nisikiliza .”
“Sawa.”
 “Mimi nafikiri tuketi ndio tuzungumze”
“Hapana. Nina kazi nyingi pale na nina muda mfupi sana wa kukusikiliza”
“ sawa”
“Tunazungumzia kitu gani hasa”
“Labda nijitambulishe.Mimi naitwa Luwanda, mtoto wa John Nyau”  alipomtamkia jina akataka kukimbia,mzee anayeogopwa sana maeneo ya Nyandira.
“Naona umeshtuka.Sikuja kwa mabaya.Nimekuja kwa heri kutaka mkono wa heri”
“Nambie wewe ndiwe mtoto wake wa Dar wanayejivunia?”
“Unataka kujua ukweli?”
“Ndio” macho yakiwa yamemtoka.
“Hapana.”
“hapana nini?Duhh, haya nambie”
“Nasikia watu wanasema mzee mchawi halafu ananiringia mimi.Najua wanavyosema lakini nataka nikuthibitishie ni upuuzi. Halafu mimi sikai dar”
 “Kwanini”
Hakumjibu akamwangalia.
“Nisaidie kitu hiki.Uliniona wapi?”
“Nilikuona jana ukiulizia mafuta pale. Nikasema dahh bonge la mtoto”
“Kisha”
“Sikia kibua sikuja hapa kupoteza wakati.Nataka kujua kama nina nafasi”
“Nafasi.Sisi hatupangishi bwana”
“ Mbona nimeambiwa, huna shida”
“Mhh nimekuwa jamvi la wageni”
“unasemaje?”
“Nimekuwa jamvi la wageni”
Hakusema na kweli ndicho alichoambiwa.
 “Unanijua mimi kikwelikweli”
“Labda sikujui”
“mimi sukari guru, unaijua sukari guru wewe”
“kama nikijua?”
“Huwezi kuila. Sikia umekuja hapa kunitongoza.Nikuambie kwamba mimi ni sukari guru huwezi kuipikia chai lakini unaweza kuila kwa saladi.Wewe unataka chai au saladi.?”
“Asubuhi sana kula saladi”
“Kwa hiyo unataka chai.Sijawahi kuambiwa hata na mwanaume mmoja duniani hasa, za dizaini zenu kuhusu sukari guru na saladi.Chai ina masharti yake. Nenda sikufai kwa kula wala kulumwagia.”
Akamtazama macho makavu kabisa.
“nakutaka kwelikweli”
“Wewe mtoto mzuri usitake kulala na majamvi huwezi kuyajua kama yanachawa au kunguni”
“nikuambie neon”
“Sema”
“ Sijaguswa nitakuwa zawadi kwako. “
Akacheka.
“Hili nalo linaongeza sababu nyingi zaidi za kukukataa.Sitaki washamba , sitaki kufundisha mtu”
 “Nataka nikuoe ili unifundishe”
“Nenda kafundishwe kwanza ukishakuwa mwalimu nitakuangalia”
 “Kwanini?”
“Sitaki kutoa wanafunzi wanaopita walimu halafu wende kufundisha wengine”
 “Kibua masikhara hayo”
 “Mimi sihitaji mume,kama wewe ndiwe unataka kuwa mume poa sana kwanza unapendeza pili unaonekana kichwani wamo,yaani naomba ufikirie tu kwenda kuoa kwingine usitafute maradhi usioweza kuyatibu”
 Itaendelea