TAFUTA HAPA

Hadithi:Utamu wa sukariguru-2


Luwanda alitahayari kabisa kwa maneno ya binti yule ambaye katika vijiwe walisema ni maharage ya Bunduki  yaliyopandwa Kibaoni maji mara moja. Alishindwa kuelewa kama anapambana na sera au anapambana na mtu ambaye alishaamua kuondokana na tabia  alizokuwa nazo.
katika maisha yake alikuwa anatarajia kuwa na mtu ambaye akimuona roho inalipuka. tangu awe mtu mzima kwa maana ya kuwa kijana wa kuweza kuoa hajawahi hata mara moja kuangalia uzuri na ubaya wa mwanamke, kwani hakuna aliyemfanya akose akili, huyu kamfanya akose akili akaambiwa ni rahisi na kama urahisi wenyewe ndio huo alikuwa amekata tamaa.
alimwangalia tena, binti alikuwa anatabasamu tu.
Alimfanya moyo wake usimame kidogo kisha ukaanza kupiga kwa kasi.Tabasamu lile jamani na bila kujua akawa anajiharibikia akaamua taratibu kuondoka eneo lile, akiamua kupita kwenye siru wala bila kuaga na jinsi binti alivyomuangalia kijana anahangaika hakutaka hata kumtafadhalisha kuhusu siru  za chini ambazo zilikuwa zinachoma mno na zinaweza kumfanya awe mgonjwa.
Alipofika juu kidogo ya mahali pale walipokuwapo, aligeuka kumtazama na msichana yule alikuwa anarejea nyumbani kwao, alipigwa na butwaa.
Luwanda alifika nyumbani akiwa na mawazo tele, mawazo ya kumkosa mtoto shoo yule. Alikuwa amebakiza siku nne tu za kuishi nyumbani kwao, akadhamiria  kumfuata kanisani potelea mbali.
Kibua alirejea nyumbani taratibu, akiwa na mawazo wanaume wanamfikiriaje. Aliwaona wanaume kama watu wenye kujali maslahi yao zaidi kuliko maslahi ya watu wengine.Alidhamiria kuendelea kuwa singo kwa kipindi kirefu ili atafute maisha yake mwenyewe.
Anaingia nyumbani anakutana na mama yake katika kizingiti.
"ulikuwa wapi"
"Shikamoo mama"
"Nimekuuliza ulikuwa wapi"
"Kwa hiyo hutaki kujibu salamu yangu mpaka ujuwe nilikuwa wapi." alienda mpaka karibu naye akamnong'oneza kitu, mama akaruka vibaya.
"We mtoto mimi dada yako?"
"Si unataka kujua"
"Nitakuozesha ndoa ya mkeka"
"Wala usijali mama nitajiondoa mwenyewe manake nakuona nakuletea kero"
"Nitamwambia mjomba wako kwamba  huna maana yoyote na kazi aliyokutafutia afute"
"Ha mama!" alisema Kibua.
Akajiondoa kwenda chumbani kwake. Alienda akaanza kulia manake mama yake amekuwa sasa si mama mzazi bali kama vile ni mama wa kambo. alilia na kuishia usingizini, alikuja kuammshwa na ubaridi uliokuwa unaingia chumbani kwake jioni ilikuwa imeingia.
Alijikokota kwenda jikoni akamkuta mama yake anatafuna mahindi ya kuchoma.
"naona leo umechoshwa sana. Umelala weeeH"
"Si bure inawezekana mimi ulinipata kwa bahati mbaya, chuki za aliyekuachia mtoto unazihamisha kwa mtoto" alisema Kibua, safari hii bila hasira alikuwa ametulia zaidi.Akamtazama mama yake.
"Hamna tofauti yoyote ile"
"Mbona umekuwa ukiniambia kwamba baba yangu alishakufa zamani"
"Ulitaka aendelee kuishi"
"we ngoja hapa uletewe mahali  halafu unatambua kwamba mimi naoelewa na kaka yangu"
"Mjalaana we! unataka kuleta mkosi gani"
"ha ha ha!!! Huwezi kutambua mama si wewe mwenyewe unaniambia mimi nina ugonjwa wa wanaume?"
"Hebu nenda kale chakula huko"
Wala hakumjibu. mama yake alimzaa akiwa na miaka 15, amekua amemfunika lakini amekuwa kama vile ana husda fulani na mtoto wake na mwana alikuwa akidhani inatokana na kuanguka kwake kila mara kumbe sivyo.
Alienda mezani akakuta wali na samaki kitoga. Akachota chakula chake akaenda kukaa karibu na mama yake, alikuwa anampenda pamoja na visa anavyomfanyia.
"mama nijkuulize swali"
"sema dada"
"Itakuaje kama mimi nikiondoka hapa"
"unataka ukweli dada"
"kabisa!"
"nitakuwa mpweke lakini la maana nitaondokana na aibu ya kuambiwa kila mara kwamba mtoto wangu ni jamvi la wageni"
"Mhh@"
"kweli kabisa dada wala sitanii"