TAFUTA HAPA

HADITHI:Utamu wa Sukari Guru-13

Wiki iliyopita tuliona kizaazaa ambacho nusura kitokee wakati kibua alipokutanana mvulana waliyechangia baba na kuokolewa na mjomba wao.Kibua alidhamiria kumvaa mama yake.Je mama atajibu swali la Slivesta ni nani?Endelea.


Mama kibua alishtuka, akamtazama mwanae.
“Mama unakumbuka nilikuambia kwamba hutaki kunieleza baba yangu nikajua ndugu zangu kwa sababu tu za hasira zako, nitajikuta nakuletea aibu.Sasa leo karibu nimpe mwili mtu ambaye ni kaka yangu.”
“Unasemaje?”
“Nimesema mama kwani hukunisikia?”
“Nimefadhaika”
“Kwanini mama?”
“Unajua kwanini nimefadhaika.Umerejea na hata hujakaa kuona dunia ikoje umeanza kutafuta wanaume una tatizo gani?”
“Mimi mkubwa mama. Najua kabisa yule mvulana nilimuona nikampenda kwa sababu ni ndugu yangu sikujua nilidhani ni mapenzi, sasa wa kumlaumu nani?” alisema Kibua kwa hasira.
“Wewe”
“Nadhani ni wewe mbona hujataka kunambia baba yangu nani?”
“Kama mwanae niko kipanga hivi, kuna siku baba atakuletea posa hapa, shauri lako”
Akanyanyuka na kuingia nyumba ndogo baridi lilikuwa limeanza.
Mama yake Kibua alikaa palepale akitafakari maneno ya mwanae ambaye kila mara alikuwa akisema kwamba kuna siku kaka yake au baba yake ndiye atakayeleta posa  na yeye hatakuwa na kosa.
Aliona  muda umefika wa kumwambia ukweli kuhusu mahusiano ya yeye na baba yake.Mahusiano ambayo baadaye hayakuendelea kwa sababu ya ndugu wa koo mbili zinazohusika.
Alitafakari na kucheka.
Akaondoka na kuingia nyumba aliyoenda mtoto wake, akamkuta anasinzia pale.
“Kibua” aliita kwa upole.
“Sema mama.”
“Umechoka sana mwanangu.”
“Kawaida mama mtu umekuja safari. Umechoka unakutana na kitu ambacho kama si Mungu kukuamia basi ujuwe shida kubwa inakungoja katika mlango wa nyumba yako. Nataka kutembea na kaka yangu ambaye mama yangu hataki kumsema kama kaka yangu. Mama yangu anasema baba yangu alishakufa. Unakutana na sura nyingine kabisa katika mawazo. Ndio mama nimechoka sana.”
“Je hautakuwa tayari kusikiliza hadithi yangu?”
“Hadithi gani mama”
“Ya maisha yangu.”
“Hiyo sitaki kuisikia kama ungeliniambia hadithi ya baba yangu yupo wapi na Silvesta ni nani tungesikiliza”
“Ni sehemu tu ya maisha magumu ambayo nimeyapitia”
“Kwa hiyo unataka na mimi nipitie maisha hayo hayo mama”
“Hapana lakini ni vyema ukanisikiliza”
“Mama kesho, naona kweupee hatutasikilizana”
“Tutasikilizana mwanangu kama utakuwa mvumilivu”
“Haya  nambie”
“Labda tuanze mwanzo kabisa. Slivesta ni kaka yako kwa maana baba yenu ni mmoja. Baba yako yungali hai yupo Lubwe. Lakini ninachotaka kusema ni kwamba tuliachana na baba yako wakati wa ujauzito wako na mpaka leo nahangaika na dunia tu”
“Kwanini muachane?”
“Wazazi wangu hawakumpenda baba yako!Walisema maneno mengi, lakini mbaya zaidi, upande wa pili nao haukututaka wakamuozesha haraka sana baba yako kwa binti mwingine ambaye ni wa jirani kwao kule ndiko alikozaliwa Slivesta”
“Mimi na Slivesta nani mkubwa?”
“ Wewe ni mkubwa kwa miezi sita”
“Ahaaa”
“Nilikuwa mzuri tu kama wewe wakati tulipokutana na baba yako.Nilidhani nimempata mume, lakini baadae nikaruhusu mambo ambayo hayakustahili kuruhusiwa na ilikuwa siku yangu mbaya, siku yangu mbaya kabisa.Nikashika himila yako.Nikamwambia baba yako.”
“Enhee”
“Akamwambia mjomba wake, akasema ukoo wetu una kilema hawezi kuoa hapa.Akaja akaniambia tatizo lakini badala ya kupigana kama mwanaume akamsikiliza dada yake, akaniacha mimi.Nikakasirika akaondoka hapa hakurejea mpaka wewe una miaka mitatu.Akaja na wazo la kumrudisha mtoto kitandani.Nikamwambia akamwambie dada yake.Ikawa ndio mwisho wa kuonana na baba yako”
“Ahaaa sasa unasemaje?”
“Sijui kama atakupokea lakini kama unataka kumuona utaniambia nifanye mpango”
“Nitataka kumuona,nitataka kumuona.Unadhani sitaki kumuona? Nimetamani kumuona baba yangu tangu nikiwa mdogo wakati watu wanawaita baba zao.”
“Wanawaita baba zao?”
“Ndio shuleni kila siku wanakwenda baba zao wewe ulikuwa huji nikikuuliza baba yangu unaleta maneno mengi”
“hee!”
“unashangaa ngoja nikuulize swali jingine”
“Mhh!”
“Ndio, mama mimi ni Kibua kweli?”
“Wewe ni kibua kweli”
“Mbona na wewe ni Kibua?”
“sasa hilo shauri jingine kabisa lakini baba yako ukoo wake ni wa wamaze, wewe ni mmaze na mimi ni mtoto wa wamaze”
“Mchanganyiko mbaya kabisa.”
“Wala mwanangu, lakini lazima uishi ukizoea shida za wanaume”
“Wala usijali mama.Pole kwa mikasa nahitaji kulala, usiku mwema.”
“Hujala maboga yako?”
“Ohh unadhani nilisikia njaa. Duh afadhali nimejua kitu.Ngoja nile halafu  nifanye kitu Fulani kesho”
“Kitu gani mwanangu”
“Utanionesha kiwanja,nahitaji kujenga.”
“Kujenga?”
“Ndio”
“Wajomba zako umewaambia?”
“Hao wanaoniita majina yote?”
“Tabia yako mbaya”
“Kweli mama.Muite baba tu kama utapenda wengine haitwi mtu hapa.”
Mama alimtazama mwanawe mpaka akasinzia kwenye kiti cha uvivu pale jikoni, akamwangalia alivyokuwa anakula boga pale, alikuwa amekua na alionekana kujiamini sana.
Ni kweli Kibua alikuwa amekua, alikuwa na nidhamu zaidi kuliko alipoondoka, alidhamiria kujenga nyumba kabla ya mvua za masika,matofali ya kuchoma au ya miti atajua baba yake atakapofika.
itaendelea