TAFUTA HAPA

HADITHI:Utamu wa Sukari Guru-11

KIBUA ameshaondoka mjini ambako ndiko alikoishi kwa miaka minne akirejea nyumbani kwao kwa mapumziko. Ameondoka huku baba mwenye nyumba akiwa anatamani aendelee kuwapo  na Chioma mtoto wa mwenye nyumba akiwa amechanganyikiwa. Kibua akifika nyumbani yapi mengine yatatokea?

Pale Morogoro Kibua alishushwa mtaa wa Reli na kuchukua teksi mpaka katika Soko Kuu la Morogoro ambako magari ya kwenda nyumbani kwao Mgeta yalikuwa yanasimama.
Mwenye teksi alimshusha pale na akabaki anashangaa jinsi watu walivyojaa katika mida ile, alichachawa. Akasogeza mizigo yake na kushangaa gari iliyokuwa imeandikwa kwamba inaenda Mgeta.
“Za mitondo (za asubuhi)” alisema Kibua akimsalimia kijana mmoja ambaye alionekana kuwa msafiri kwa lengo la kuanza kuzungumza naye kujua inakuaje.
“Zinogha (nzuri)”
“Nikuulize swali”
“Pasi shaka bibie”
“Eti hii gari ndio inayoenda Mgeta”
“Ndio shangazi kwani  vipi?”
“Nashangaa lile basi kubwa lipo wapi”
“La Mzee Khan? Lipo lakini kipya kinyemi”
“Linaweza kupandisha milima kweli hili?Jina lenyewe Moris”
“Yako mawili haya dada na yana wiki lakini nasikia linapata shida kwelikweli milimani hasa Chidiwa”
“Sasa watu wanaonaje hali hiyo?”
“Mwe! Mradi linawafikisha, lakini badala ya saa tatu hutumia saa nne”
“Mhh, njaa itauma kwelikweli, sijui nitafute chai”
“Likijaza tu da linaondoka we pandisha mizigo yako”
Alibaki akiduwaa akaanza kufikiria nyumbani kwao. Haikuchukua muda gari lilijaa pomoni na wakaanza safari ya kurejea nyumbani kwao Mgeta. Baada ya kupita kituo cha ukaguzi Mzinga alisinzia na hakuwa na habari mpaka kwa Kisikio walipoambiwa washuke gari lijikongoje lenyewe hadi msikitini.
Alikasirika kwani Isuzu lao walilozoea kupanda hata kama lilionekana kuwa ngarangara lilikuwa na uwezo wa kusinzia huku linatembea lakini linapiga mwendo hadi Lolo bila tashwishi.
Akiwa njiani na abiria wenzake akawa anawasikiliza jinsi watu wanavyolalamikia vigari hivyo ambavyo pia havichuki mizigo mingi kama lile gari la Khan.Lakini walisifia uzuri mmoja kwamba havikai sana vinajaa na kuondoka.
“Yaani unachosifia wewe kujaa na kuondoka hii adha ya kutembea hata huioni”
“Kwani kwenu gari inafika, si unatembea kwa miguu wewe?”
“We unakujua kwetu wewe”
“Wewe sio Kibua wewe” alisema.
“Ndio mimi Kibua wewe nani?”
“Mimi  umeshanisahau?”
“Tunabadilika dadaangu”
“Mimi kwetu Lusungi. Tumepokea ekaristi pamoja kanisa la Bumu. Ulikuwa umenitangulia darasa”
“Sura inakuja.Wewe una uhusano gani na watoto wa Evarist” alisema baada ya sura kumjia.
“Mimi ni dada mkubwa pale”
“Ahhaaa duhh! mwenzangu umekoza maji ya kunde dah”
“Morogoro hiyo” akasema kwa mbwembwe.
Alimwangalia kwa tabasamu jinsi alivyokuwa akijishebedua katika kitenge chake cha Urafiki chenye maua na ndege.
“Morogoro unafanya wapi Mzinga au Cicol”
“Niko na jamaa mmoja hivi anaendesha magari ya Cicol wanaojenga barabara ya Dodoma –Moro”
“Dah jamaa anakupiga na kitana cha chokaa mwenzangu”
“Mbona hata wewe umetakata”
“Wapi kisonoko mie”
“Wewe uwe kisonoko si itakuwa hatari”
“Mhh nambie Mwenda ehh vile, nambie”
“Mimi sikupati kokote kule ungekuwa Moro hapa ningebadili vikao”
“Kwanini ubadili vikao?”
“Ukitaka kitu hukikosi. Duhh nakumbuka shule,ukimtaka mvulana lazima umpate utadhani umechanjia”
“Hilo ndio tatizo Mwenda, ndilo lililonikimbiza nyumbani, utadhani wameniloga.”
“Tatizo jamaa wakishakula sukari wakitaka kurudia unawatolea nje”
“Ha ha ha ha una nichekesha kwelikweli,”
“Nakuchekesha siku moja tulikuuliza vipi wewe. Ukasema hii sukari guru bwana utamu wake ukizidi unakichefuchefu, sitakaa nisahau”
“Kwanini?”
“Nimeona sasa, mwisho ni kichefuchefu kitupu hii” akacheka Mwenda kwa umbea.
Wakahimizana kuendelea mbele ambako basi lilikuwa ,linawasubiri wakaabiri na ndani ya basi Kibua akarejea kulala tena akaja kuamka wakati gari lipo langoni linashuka sasa kuingia Mgeta.
Kilichomuamsha ni kibaridi kilichoingia ghafla na kumweka sawa. Nusu saa baadaye walikuwa Lolo akashusha mzigo wake , hoi kwa njaa akaamua kuingia kwa Muhulo ili aweze kujipatia chochote.
Alifika katika hoteli  ya Muhulo na kujipweteka katika viti vya mbao pale na kuagiza chai kwa maziwa ya mbuzi na kujiketia kwa mapozi makubwa, kibaridi kikawa kinamsugua taratibu, akatwaa kitenge chake na kujifunika.
“Chai yako hii dada”
“Aksante.Nipatie na maandazi matatu”
Mhudumu alienda katika kabatini na kutoa maandazi yale matatu na kumfikishia katika meza yake na kumkaribisha.
Alipoanza kula akaingia mwanamme mmoja ambaye alimsisimua jinsi alivyokuwa amejazia, palepale kila kitu katika mwili wake kikaregea. Kibua hebu jisitiri kidogo akauambia moyo wake.
Ujisitiri nini na unaona kabisa anayeingia ni kitu cha kuheshimika. Kutongoza, watongoze wanaume akipenda mwanamke inakuwa shida huyu mimi ninaye.Alijisemea.
Mvulana yule ambaye umri wake ni kama miaka 25 hadi 30 alifika pale na kuketi mbele yake, akaagiza supu ya mbuzi na maandazi.
“Itachelewa kidogo mafuta  yaliganda”
“Hamna neno Berege, nitasubiri” alisema kisha akatulia mezani kwake pale akawa anapasha moto mikono yake.Kibua alimtazama, uzalendo ukamshinda.
Itaendelea