“Sikia baba wewe ndiwe unayenianzishia matanga katika maisha yangu ningali hai” alisema Kibua kwa hasira baada ya baba yake kusema kwamba hawezi kuwa na mtoto kahaba, bazazi kama yeye.
Maneno ya baba yake yalimchoma kama mkuki moyoni hasa baada ya m zee huyo akiwa na mkewe, kumzodoa Kibua ambaye alifika hapo baada ya mama yake kumweleza ukweli kuwa juhudi za kumpeleka baba yake pale nyumbani zimeshindikana na hataki hata kusikia kwamba ana mtoto kwa jinsi anavyotia kinyaa.
Baada ya mama yake kusema hayo Kibua hakutaka hata kumjibu, alichofanya aliingia ndani akavaa nguo za ushauri akajitanda mtandio na kuelekea kwa baba yake ambaye hajawahi kumuona wala kumsikia kwa miaka yote.
Alipofika pale alimkuta Silvesta ambaye alikuwa akifunga mbuzi kisha kumwamkua alimkaribisha nyumbani pale na kwenda kuwaita wazazi wake ambaow alikuwa katika nyumba ya jiko.
Alipomuona,mama yake Silvesta aliiona sura ya mtoto wake pale akashindwa kuelewa.
“karibu ndani”
Kauli ya karibu ilimuingiza Kibua ndani ambaye aliwasalimia wazazi wake wale kwa adabu kubwa.
“Mimi naitwa Kibua, nimefika hapa kuzungumza na baba ambaye hanitambui tangu kuzaliwa kwangu hadi leo”
“Taratibu mwali, umesema unaitwa Kibua”
“Ona mai (ndio mama) “ alisema kwa kikwao akiachana na kiswahili tena kwa adabu kubwa.
“Mtoto wa nani?” aliuliza tena.
Hakumjibu na badala yake akamtazama baba yake na kunyanyua mdomo.
“Baba unaweza kujibu?”
Hapo ndipo maneno ya hovyo yalipoanza kumtoka Baba Slivesta, maneno ambayo yalimkera sana binti huyo ambaye alishakuwa kama mwehu kutokana na kusimangwa.
“Sikia baba umesema maneno mengi sana. Naweza kuwa mtovu wa adabu kukukaripia kwa kushindwa kunirejesha kitandani wewe na mwenzako, kukataa kabisa kumuona mama yangu pamoja na kumtafadhalisha kwamba utaendelea kumpenda. Umenikana kiasi ya mama kutokusema kitu bali baba yangu amekufa”
“Ndio baba yako amekufa”
“We mzee we usilete majanga hapa duniani.Usinifanyie matanga katika maisha, mimi bado nipo hai , usibane maisha yangu kwa starehe zako.”
“Starehe zangu, hebu ondoka hapa” alisema kwa ghadhabu na kutaka kuinuka akashikwa na mkewe pale.
“Mama wala usimshike.Mwache aje anipige kama kuna tusi nimemfanyia kuliko yeye. Sikuja hapa kumdai kitu chochote. Nimekuja hapa aniambie mimi ni mwanae au si mwanae na kama mimi si mwanae nijue nitampata wapi baba yangu, kwani lazima nitambike na lazima watu waje kula mahali.”
Baba akawa anatetemeka.
Akaketi chini na kumwangalia. Hakujibu.
“Sikia baba kama mimi si mwanao, mruhusu Silvesta aje atoe mahali. Alisema mwenyewe amependa bodi hili”
Akasema kwa maringo.
“Unasemaje?” alimaka.
“Silvesta juzi ulisema nini pale mgahawani?”
“Lakini sista si tulimaliza pale pale?”
“Hatujamaliza, baba anasema mimi si mwanae.Lete posa nitaikubali” alinyanyuka na kuanza kuondoka.
“Sista haiwezekani.Nimepewa taarifa zote. Baba anaweza kusema hakujui. Mimi nimefurahi kwamba nina dada nilidhani nipo peke yangu.”
Akamtazama, akatabasamu.
“Msikilize baba yako, mimi nakuachia huru kuamua kuja kunioa kama ulivyotaka au kwa vyovyote vile. Karibu kwetu.Lakini ukija ujuwe umemsikia baba yako”
Akajitupia khanga yake na kwa maringo akaondoka katika eneo lile taratibu akijua kuwa ameshinda vita, kwa kuangalia sura ya baba yake na mama yake na hasa ya kaka yake.
Jinsi alivyokuwa amejawa na hasira alienda moja kwa moja nyumbani akabadilisha nguo na kuamua kwenda kimbinyiko alikuwa na kazi ya kufanya kabla hajafanya kitu chochote, kulipiza kisasi.
Alipofika nyumbani, mama yake alikuwa na kila sababu ya kuzungumza lakini yeye alimwambia kwamba hawatazungumza kwa kuwa anakitu cha muhimu sana anataka kukifanya, aliondoka.
“Mama naenda zangu kwenye mambo yangu naomba tu usiniulize” akaondoka bila kusubiri jibu.
Wakati anafika Dawilo, kaka yake Silvesta alikuwa anaingia katika makazi yake lughongo akiwa na kondoo alikuwa kondoo wa tambiko.
Silvesta alifika pale na kuangalia zizi lililipokuwepo akamfunga kondoo yule bila kumsalimia mtu akaondoka zake taratibu, alijua wanajua nini kinatakiwa itakuwa kazi yao kuwaita wajomba.
Wakati anaondoka pale Kibua, mzozo mkubwa ulizuka kati ya Silvesta na baba yake, mzozo ambao uliamualiwa na mama yake.
“Mama nimesikia mlivyomtukana dada, lakini amefanana sana na baba pengine kuliko mimi, baba hawezi kunikatalia dada yangu. Mbaya zaidi nusura nifanye faulo kama tusingeambiwa na mtu anayetufahamu sote.Nilikuwa naleta aibu kubwa katika ukoo baba hata kama mlikuwa na hitilafu zenu na mama mkubwa”
Maneno yaliyomtoka Silvesta yalikuwa makali na mama yake alimshauri kutogombana na baba yake kwani wakati huo haukuwa sawa.Alitulia, lakini kilichomtuliza sana, ni kule kuambiwa akamate kondoo na kwenda kumfunga nyumbani kwa akina Kibua.
Itaendelea