TAFUTA HAPA

Hadithi:Penzi La Mpangaji Sehemu Ya #3

Sehemu ya 3
“Sasa dogo, aking’ang’ania kwenda kufanya malipo ofisini je?”.Yule jamaa muuguzi aliniuliza baada ya kumaliza kunitundikia zile diripu uchwara.
“Lile ticha siyo janja, halijui lolote. Yaani pale skuli kazi yake kusimamia makazi tunayolala na siyo kufundisha. Halafu mimi nina kadi hii ya bima ya afya, hivyo wewe usiwe na wasi. Mimi matibabu yangu ni bure”.
“Ha ha haa, hapo sawa nimekuelewa. Sasa ngoja niende kwa ticha lako”.Jamaa akawa anaondoka kwenda kumuita mwalimu yule niliyekuja naye.
Baada kama ya nusu dakika,waliingia huku mimi nikiwa kama sijielewi pale kitandani.
“Ticha, aisee dogo anaumwa sana”.Nilimsikia jamaa akianza kuongea na ticha wangu.
“Kwa hiyo ni nini kinamsumbua?”.Akauliza ticha.
“Nimecheki mapigo yake ya moyo ndiyo yanaenda kasi sana,hivyo yaonekana ni BP. Ila usiwe na shaka sana. Wewe niachie elfu hamsini za matibabu pamoja na tupesa kidogo kwa ajili ya chakula cha mgonjwa akihamka.
Siwezi kuendelea na matibabu bila kupata msaada wa kifedha ili tununue dawa zake na vitu vingine muhimu kama hizo diripu ambazo anatakiwa atundikiwe tatu”.Jamaa muuguzi alijielezea nia yake,na bila kipingamizi,yule ticha aliingiza mikono yake kwenye mfuko wa suruali na kuibuka na waleti iliyonona kiasi chake.
Wakati huo mimi nilikuwa namuangalia kwa jicho moja la kuiba, na nilishuhudia akitoa noti saba za elfu kumi na kumkabidhi yule jamaa.
“Sasa dokta, fanya harakati huyu mtoto apone. Mimi nitakuja kesho ili nijue ni nini kinaendelea, sawa dokta?Akiamka mpe salaam zangu”.Ticha alimalizana na yule jamaa muuguzi na kuanza kuondoka huku akisindikizwa na yule muuguzi ambaye kwa kumuangalia alikuwa ana ukame sana kifedha,hivyo zile hela kwake ilikuwa kama bahari kutokea jangwani.
“Dogo tumewin. Kweli ili ni bonge la boya. Sasa sikiliza, kanipa elfu sabini, wewe chukua hii thelathini halafu pitia huo mlango kafanye yako.
Huu wa kuingilia mimi naufunga, we ukirudi pitia mlango huo huo halafu njoo ile ofisi yangu kunipa taarifa,mwisho iwe saa kumi na mbili, sawa?”.Yule jamaa muuguzi alinipa maelekezo ya nini cha kufanya baada ya kuhakikisha yule ticha katokomea kabisa pale hospitali. Nilimjibu kwa kuitikia poa huku nazitoa zile diripu na kuanza kutoka nje.