TAFUTA HAPA

SIMULIZI YA MAMA MDOGO SEHEMU YA ...1.

Jamali ni kijana ambaye amezaliwa katika familia ya watoto wawili akiwa ni mtoto wa kwanza. Ana mdogo wake ambaye ni msichana.  Katika maisha yao wameishi katika mazingira mazuri kwani mama yao alikuwa na uwezo mkubwa sana kifedha na aliwapa kila walichokihitaji.

Baada ya mama yao mzazi kufariki na kuwaacha na baba yao Mzee Said ambaye alikuwa akimiliki mali zote baada ya kifo cha mke wake. Mzee said baada ya muda kupita aliamua kuoa mwanamke mwingine ambaye alikuwa na rika moja na mwanawe Jamali.

Mkoa wa Dar es salaam ni mkoa ambao umejaa wakazi wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania na pia kumesheheni wafanyabiashara mbalimbali wakubwa kwa wadogo. Maeneo ya Masaki katika Mkoa wa Dar es salaam ni sehemu ambayo wanaishi watu ambao wana uwezo sana kifedha na kuna utulivu pamoja na ulinzi mkali sana maeneo hayo.


Familia ya Mzee Said ni moja kati ya wakazi waliokuwa wakiishi katika maeneo hayo akiwa pamoja na mke pamoja na watoto wake Jamal na Aisha. Mama Jamal alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa sana akiwa anajishughulisha na kampuni zake binafsi katika uuzaji wa vifaa vya ujenzi na pembejeo akisaidiana na mume wake Mzee Said.

Mzee Said alikuwa akifanya kazi katika Wizara ya Kilimo, na watoto wao walikuwa wakisoma katika shule nzuri sana.  Jamal alikuwa Kidato cha Kwanza na alikuwa akisoma shule ya kutwa, wakati Aisha alikuwa akisoma Darasa la Pili. Jamal na Aisha waliishi kwa kupendana na mara nyingi walikuwa wakicheza pamoja. Kwa ujumla maisha katika familia ya Mzee Jamal yalikuwa mazuri yenye amani na upendo siku zote.

Jamal alipofika Kidato cha Tatu mama yake alitaka akasome Mkoa wa Kilimanjaro katika shule za bweni ili apate muda mwingi wa kujisomea. Aliamua kumwambia Mzee Said juu ya wazo lake, kabla ya kumwambia Jamal. Ilikuwa ni jioni  wakati Mzee Said na mkewe wakiwa  wamekaa katika uwanja wa nyumbani kwao. Jamal na Aisha walikuwa wakibembea huku wazazi wao  wakiwaangalia.

"Baba Jamal hivi unaonaje tungempeleka Jamal katika shule ya bweni ili apate muda wa kutosha wa kujisomea.” Alishauri mama Jamal.
 “Hapana naona hujawaza vizuri. huoni kama Aisha atakuwa mpweke kwani amemzoea sana kaka yake. Mimi sijaona  tatizo hata akisoma tu hapahapa hata hivyo mbona shule anayosoma ni nzuri sana!” Mzee Jamal alichangia mada ingawa alikwenda kinyume na wazo la mkewe.
“Sawa mume wangu ila hata kama ni hapahapa Dar es salaam akalale hukohuko shuleni ili aweze kupata muda wa kujichanganya na wenzake katika kujisomea kuliko kwenda na kurudi.”  Alisisitiza mama Jamal.
“Haya mama watoto hilo halina shida ngoja nimwite Jamal tumwambie.” Alisema baba Jamal.

“Jamal!” Aliita Mzee Said.
”Naam baba!” Aliita Jamal.
“Hebu njoo!” Aliita Mzee Said.
“Nakuja baba!” Alisema Jamal huku akimshika mkono mdogo wake na kuelekea waliko kaa wazazi wao.
 “Na nyie mnavyofuatana kama kumbikumbi.” Alitamka mama Jamal huku akitabasamu.
“Kaeni chini basi”. Alitamka baba Jamal huku akimshika Aisha mkono.
“Tumejadiliana na kukubaliana na baba yako kwamba kuanzia wiki ijayo Jamal utakuwa unalala shuleni ili usome zaidi, kwani tumegundua kwamba huku nyumbani hupati muda mzuri wa kujisomea.” Alimaliza kuongea mama Jamal.
“Hapana mama mimi nitabaki na nani? Sitaki kama ni hivyo bora na mimi nikalale shule” Alijibu Aisha huku akimwangalia mama yake kwa hasira. Nini kitaendelea usikose sura ya 2