TAFUTA HAPA

SIMULIZI YA MAMA MDOGO SURA YA ......2

ILIPOISHIA “Tumejadiliana na kukubaliana na baba yako kwamba kuanzia wiki ijayo
Jamal utakuwa unalala shuleni ili usome zaidi, kwani tumegundua kwamba huku nyumbani hupati muda mzuri wa kujisomea.” Alimaliza kuongea mama Jamal.
“Hapana mama mimi nitabaki na nani? Sitaki kama ni hivyo bora na mimi
nikalale shule” Alijibu Aisha huku akimwangalia mama yake kwa hasira.

INAPOENDELEA“Haya mama na wewe tutakupeleka ukalale shule ukiwa mkubwa kama
kaka yako.” Alijibu Mzee Said huku akicheka na kumnyanyua Aisha.
“Sawa mama mimi nitakwenda hakuna tatizo na Aisha si atakuwa anakuja
kunitembelea?” Alijibu na kuuliza Jamal.
“Ndiyo atakuwa anakuja, ila nataka ukasome kwa bidii ukifaulu vizuri
nitakupa zawadi nzuri sana, sawa mwanangu.” Alisisitiza mama Jamal.
“Sawa mama bila shaka nitasoma sana kwanza nataka kuwa Waziri wa
fedha nikiwa mkubwa.” Aliongeza Jamal.

Baada ya wiki moja Jamal alihamia shuleni na kumwacha mdogo wake
akiwa na wazazi wake pamoja na msichana wa kazi. Wazazi wake walikuwa
wakienda kumtembelea mara mojamoja. Jamal akiwa anaendelea na shule
aliwazoea wanafunzi na mazingira ya kuishi bweni.

Jamal alipofika Kidato cha Tatu alikuwa kijana mkubwa mwenye busara
na mwenye kupenda sana kusoma. Mama yake aliongeza bidii katika
shughuli zake za kutafuta kipato ili kuhakikisha Jamal anapata mahitaji
yote ya shule na mengineyo. Mara kwa mara alimtembelea Jamal shuleni
na kumuasa asome kwa bidii ili kujiandalia maisha yake na ya mdogo wake.
Jamal alikuwa mtiifu katika kila aliloshauriwa na mama yake.
 ***************Baada ya miezi sita**********************

Siku moja mama Jamal aliugua ghafla na kupelekwa hospitali kwa ajili ya
matibabu. Kutokana na hali yake kuwa mbaya sana mama Jamal ilibidi
alazwe. Mzee Said alihangaika sana kuhakikisha mama Jamal anapata tiba
bora naya haraka ili kunusuru uhai wake. Mzee Said aliamua kumfuata
dokta ofisini ili kutaka kujua kinachomsumbua mke wake.

“Habari yako Mzee. Karibu sana,karibu uketi”Alisema Daktari baada tu
ya Mzee Saidi kuingia ofisi.
“Asante Daktari vipi hali ya mke wangu anaendeleaje.” Alijibu na kuuliza
Mzee Said.
“Hali ya mkeo inaendelea vizuri ila kuna tatizo ambalo tumeligundua
baada ya kumpima.” Alijibu Daktari.
“Tatizo gani hilo Daktari?” Aliuliza Mzee Said.

“Mke wako ana kansa ya kizazi ambayo inamsumbua kwa muda mrefu
lakini hakuwahi kwenda hospitali na hili ni tatizo kubwa. Ningependa
kuwa muwazi kwako, ni kwamba maisha yake yapo hatarini kwani ugonjwa
alionao umefikia katika hatua mbaya sana.” Alisema Daktari huku Mzee
Said akiwa anamsikiliza kwa makini.
“Mungu wangu! Unamaanisha nini maisha ya mke wangu yapo hatarini?
Inamaana hatopona kabisa?” Aliuliza Mzee Said kwa sauti ya
kuchanganyikiwa.
Daktari naomba unisaidie mke wangu apone kwa gharama yoyote ile
fanya uwezalo.” Alisihi Mzee Said.
“Kwa kweli kwa hatua aliyofikia itamchukua muda mfupi kuishi ila
nitampa dawa za kutuliza maumivu ili angalau kumwongezea siku za
kuishi.” Alisema Daktari.

Mzee Said alikaa kimya kwa muda kidogo huku akiwa hajui atafanya nini,
kisha alijikaza na kuomba akamwone mke wake. Daktari alimpeleka kwa
mkewe na kumruhusu kuzungumza naye. Mama Jamal alipomwona tu
mume wake alianza kububujikwa na machozi huku akimwangalia
mumewe kwa uso wa kuonewa huruma.
“Mume wangu naomba unisamehe kwani huu ugonjwa nilikuwa najua
kuwa ninao, lakini sikukufahamisha nikawa nameza tu dawa. Nisamehe
baba Jamal.” Alitamka mama Jamal huku akilia kwa kutoa kwikwi.
“Usilie mke wangu Mungu atakusaidia utapona.” Alitamka Mzee Said
huku akisogea na kumshika mkono.

Kesho yake mama Jamal alipewa dawa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Akiwa nyumbani hali yake ilizidi kuwa mbaya na alitaka mtoto wake Jamal
akaitwe shuleni ili aje azungumze naye. Mzee Said aliondoka kuelekea
shuleni anakosoma Jamal.
“Itakuaje kwa Jamal akigundua kuwa mama yake anaumwa kansa na
hawezi kupona?” Aliwaza Mzee Said akiwa njiani kuelekea shuleni.
Alipofika katika ofisi za utawala aliwaeleza walimu hali halisi kuhusu
kuugua kwa mama yake. Walimu walimwita Jamal.
Baada ya Jamal kumwona baba yake alishtuka kwani haikuwa kawaida yake
kwenda kumtembelea shuleni. Je nini kinaendelea usikose sura ya .....3