TAFUTA HAPA

SIMULIZI YA DADA YANGU SURA YA ..........8.

ILIPOISHIA..............Baada ya wiki kadhaa kupita mawasiliano kati ya James na Esta yalikwisha kwani kila Esta alipojaribu kupiga simu James alikuwa hapokei. Na ikitokea amepokea alimtaka asiendelee kumpigia simu tena. Upendo aliondoka na kwenda Morogoro kwa ajili ya kuandaa sherehe. Akiwa Morogoro mdogo wake alikuwa bado yupo chuoni, hivyo wazazi wake walimpigia simu na kumwambia ni lazima awepo kwenye sherehe ya dada yake.

INAPOENDELEA........
Zikiwa zimebaki kama wiki mbili kufanyika sherehe ya kumuaga Upendo, Eliza alirudi Morogoro kwa wazazi wake ili kusherekea pamoja na dada yake. Siku Eliza alipofika, wazazi wake hawakuwepo ila Upendo pekee. Upendo alipomwona mdogo wake alifurahi sana, alimpokea begi wote wakaingia ndani.
“Jamani hatujaonana siku nyingi sana my young sister (mdogo wangu) mbona umenenepa hivyo ulikuwa unasoma kweli wewe?” Alisema Upendo.
 Eliza alimwangalia sana dada yake:
“Dada Upendo kuna kitu nataka nikwambie, ila iwe siri yako sitaki mama wala baba wafahamu hili.“ Aliongea Eliza kwa kusihi.
Upendo alishtuka na kuwaza moyoni mwake: “Je, atakuwa ana tatizo gani?”Aliwaza Upendo. Hebu niambie tafadhali.

 “Upendo mwenzio nina mimba hapa nilipo ndio maana unaniona nimenenepa.” Alianza kueleza Eliza.
“Acha utani wako wewe una mimba ya nani.” Upendo alihoji kwa mshangao.
 “Nina mimba ya kijana mmoja anaitwa Juliasi sijui hata nitampatia wapi najua anakaa Dar es salaam, lakini sijui nitaanzia wapi kumpata.” Alisema Eliza huku akiwa ameinama.
 “Inamaana wewe umepata mimba ya mtu ambaye hata ha umjui vizuri, kweli mdogo wangu umechezea maisha yako.” Aliongea Upendo kwa kejeli.
Eliza machozi yakiwa yanamtoka,
 “Nisaidie dada yangu mimi sijui nifanyeje hapa nilipo kwani hata mwanamume mwenyewe nikimpigia simu hapokei na ameshakataa hii mimba ameniambia niitoe na mimi siwezi kufanya hivyo”.

 “Haiwezekani! Hiyo mimba usitoe kumbuka nilikuonya mdogo wangu uwe makini na hawa wanaume. Wengi wao ni matapeli sasaa…    ngoja, tutajua cha kufanya kesho lakini usijali sana kwani tayari jambo limetokea, kulia siyo sulihisho.” Aliendelea kumbembeleza na baadaye alimtaka akaoge ajiandae kwani wazazi wao wangerudi muda huo.

Wazazi wao walikuwa wamekwenda kuwachukua ndugu wengine, lakini walikuwa wanafahamu kuwa Eliza anakuja siku hiyo. Baada ya dakika kadhaa kupita wakiwa wanaendelea na mazungumzo Baba na Mama yao pamoja na ndugu wengine walifika. Upendo aliwakaribisha wageni, na kuwaelekeza sehemu za kukaa. 

 
“Karibuni sana, wengine wakae pale na wengine hapa, waswahili husema ‘sherehe ni watu’, na watu wenyewe ni ninyi, sisi na wengine watakao kuja.” Upendo aliwaelekeza wageni. Baba Upendo (Mzee George) alimtuma Upendo akamwite mdogo wake aje awasalimie wageni. Upendo aliinuka haraka na kuelekea chumbani.
“Eliza unaitwa na baba ili ukawasalimie baba, mama na wageni. Nakuomba uvae gauni kubwa ili wasielewe mabadilko uliyonayo, kwani mimba uliyokuwa nayo imeanza kujionyesha.” Alishauri Upendo.

Eliza alijiandaa kama alivyoshauriwa na Upendo kisha wote wakaelekea sebuleni.  Alipofika aliwasalimia wazazi na shangazi yake na wageni wengnie waliokuwepo
”Jamani ni wewe wajina wangu Esta umekuwa mkubwa hivi”. Shangazi yake alishangaa kuona Eliza amekuwa mkubwa.
“Yaani dada, hilo jina la Esta mwenzio halitumii anatumia jina la Eliza, wamekuwa wakubwa sana. Hata sisi hatujawaona siku nyingi. Huyu yupo chuoni Arusha anaingia mwaka wa mwisho.“ Alifafanua Baba Upendo huku akimwangalia shangazi yake Eliza na kucheka.
“Kweli siku zinakimbia na hilo jina la Esta ha ulitumii unapenda kuitwa Eliza mama jamani watoto wa siku hizi.” Aliendelea kushangaa na kucheka shangazi yake Eliza.

 “Hapana shangazi, huwa nalitumia mara moja moja.” Alijibu Esta huku akiinamisha kichwa chini kwa aibu.
“Lakini bora usilitumie kwani haya majina ya kurithi wakati mwingine sio mazuri unaweza ukampa mtoto jina la mtu mwenye mikosi na mtoto akajikuta anakuwa na mikosi katika maisha kwa sababu ya majina ya kurithi.” Alisema shangazi yake huku watu wote wakiangua vicheko.
 “Hakuna wifi hizo ni imani tu za watu.” Alijibu mama Upendo huku akiinuka kuelekea jikoni.
“Haya jamani huku jikoni vipi?” Aliuliza mama Upendo.
“Tayari mama hakuna tatizo.” Alijibu Upendo.Nini kitaendelea usikose sura ya 9..