TAFUTA HAPA

SIMULIZI YA DADA YANGU SURA YA 7

Ilipoishia........ “Juliasi karibu utaondoka kwenda Dar hivi kweli utanikumbuka? Na jinsi warembo walivyo wengi huko Dar?” Aliuliza Esta huku akimpapasa uso James.
“Hapana siwezi kukuacha mpenzi wangu tutawasiliana usijali. Arusha nitakuja hata wewe utakuwa unakuja Dar es Salaam.” Alijibu James huku akimbusu Esta katika shavu la upande wa kushoto.
 “Sawa hakuna tatizo mimi naomba tuendelee kuwasiliana nakupenda sana mpenzi wangu.” Alijibu Esta huku akiwa amemkumbatia na kumbusu James.

******************
Inavyoendelea.....Huko Dar es Salaam Upendo alikuwa anaandaa mapokezi ya kumpokea mchumba wake James ambaye walikuwa hawajaonana yapata miezi minne. Alifanya usafi wa mazingira ya nyumba na kubadilisha baadhi ya vitu ili kuonekane tofauti.  Alikuwa na furaha sana siku hiyo ambapo kesho yake James ndiyo alikuwa akirud.i Alinunua maua mazuri ya rangi nyekundu pamoja na mvinyo. Kesho yake James alirudi, Upendo alikwenda kumpokea uwanja wa ndege yapata saa moja jioni. James alishuka kwenye ndege na kuelekea sehemu za mapokezi na kumkuta Upendo aliyempokea kwa furaha sana.
“Darling (mpenzi) umependeza sana, umezidi kuwa mweupe, nimefurahi sana kuwa nawe tena” Aliongea James huku akiwa amemkumbatia Upendo.
 “Yaani James nimefurahi sana umerudi nilikuwa mpweke sana.” Alijibu Upendo huku akimpokea James begi.
Walielekea  Kinondoni nyumbani kwa James. James alishangaa sana kuona mabadiliko ya nyumba yake na jinsi ambavyo Upendo alikuwa amepamba.
“Mpenzi unafaa sana katika mambo ya upambaji nyumba imekuwa tofauti kabisa nimefurahi kweli wewe ni mke mzuri.” Aliongea James kwa furaha huku akikaa kwenye sofa.
 “Asante mpenzi wangu nenda ukaoge uje tule chakula halafu unipe habari za Arusha.” Upendo alimsihi James. Usiku ule ulikuwa ni usiku wa furaha kwa wote wawili walikula na kunywa na kulala huku wakiwa na mikakati ya kufunga ndoa haraka.

Hatimaye maandalizi ya kumuaga Upendo yalikamilika na wakati huo wazazi wa James walikuwa wakiandaa harusi. Mawasilianao ya Esta na James yalipungua sana. Kila Esta akimpigia simu alikuwa akimdanganya kuwa ametingwa sana,  kitu ambacho kilikuwa kikimuumiza sana Esta. Hata hivvyo Esta aliendelea kujipa moyo kuwa Juliasi anampenda bila kujua kuwa alikuwa ni tapeli wa mapenzi.  Baada ya miezi miwili kupita Esta aliugua homa na kwenda hospitali ambapo alipimwa na kukutwa akiwa na ujauzito wa miezi miwili.  Kutokana na hali hiyo Esta alichanganyikiwa sana.
“Mungu wangu nina mimba ya Juliasi nitafanyaje mimi na huyu mwanamume sijui ana mpango gani na mimi. Nafikiria kuitoa mimba lakini naogopa sana. Hapana lazima nimfahamishe hali halisi kwa sababu sijui nifanyeje. Kwani nyumbani baba akijua ataniua na  ndugu zangu watanifikiriaje, nikifika chuo ni lazima nimpigie simu leo.” Aliwaza Esta huku machozi yakimlengalenga
 
Esta aliondoka pale hospitali akiwa na mawazo mengi sana.  Alipofika chuoni aliingia chumbani kwake na kupiga simu. Simu iliita muda mrefu bila kupokelewa. Aliendelea kupiga kama mara mbili bila mafanikio hadi alipojaribu tena ndipo simu ilipokelewa na James aliyekuwa kazini kwake muda huo.
“Haloo vipi Juliasi mbona nakupigia simu yangu hupokei?” Auliza Esta.
 “We mwanamke mjinga kweli inamaana niache kazi zangu nipokee simu yako? Je, hujui kwamba huu ni muda wa kazi? Je, unasemaje?” Aliuliza James kwa sauti  iliyojaa hasira .
 “Samahani mpenzi kwa usumbufu nimekupigia nikwambie leo nimekwenda hospitali kupima nina mimba yako ya miezi miwili.” Esta alimfahamisha James. “Hee! Nini? Mimba! Ya nani!” Alihamaki James huku akionyesha kama mtu aliyekanganyikiwa.

 “Kweli Juliasi unaweza kuniuliza kuhusu mimba hali unajua ni yako? Halafu unaniuliza ya nani?” Aliuliza Esta huku amebana pua kumuigiza James.
“Sikiliza nikwambie Esta, mimi sina mpango wa kuwa na mtoto sasa hivi, kama wewe ulitaka mtoto ni juu yako ninachoweza kukusaidia ni pesa ya kutoa hiyo mamba.” Alisema James kwa sauti ya kutetema tofauti na siku nyingine.
Esta hakuamini maneno anayoambiwa na James”
“Sikujua kama utanifanyia hivi Juliasi, unajua ni kiasi gani nakupenda, nashukuru sana ila hii mimba sitaitoa na huyu mtoto ni wako na nitamleta huko huko Dar es Salaam.” Kisha akakata simu na kulia kwa uchungu huku akijilaumu moyoni mwake na kujipa matumaini”
 “Nilijua Juliasi ni mwanaume mkweli kumbe yuko hivi au kwa sababu ya hii mimba imekuja ghafla, sijui nifanyeje naamini mambo yatakwenda sawa, ngoja nimwache kwanza kwa sasa.” Alijipa moyo Esta.
Esta aliendelea kuwaza sana na baadaye akamua kuendelea na shughuli zake za kawaida.
James naye alibaki akiwaza moyoni mwake.
“Hivi nimefanya nini mimi huyu msichana ana mimba yangu na hataki kuitoa na mimi nafunga ndoa hivi karibuni. Sijui itakuwaje ila ngoja nimwache siwezi kumpoteza Upendo nampenda sana na ndio mke wangu, sitaki mawasiliano na huyu mwanamke tena.”
Basi naye aliendelea na mambo yake huku akiwa anajiandaa na harusi yake. Wakati huo Upendo alipanga safari ya kwenda Morogoro kwani ilikuwa imebaki kama mwezi mmoja afanyiwe sherehe ya kuagwa na wazazi wake.

Baada ya wiki kadhaa kupita mawasiliano kati ya James na Esta yalikwisha kwani kila Esta alipojaribu kupiga simu James alikuwa hapokei. Na ikitokea amepokea alimtaka asiendelee kumpigia simu tena. Upendo aliondoka na kwenda Morogoro kwa ajili ya kuandaa sherehe. Akiwa Morogoro mdogo wake alikuwa bado yupo chuoni, hivyo wazazi wake walimpigia simu na kumwambia ni lazima awepo kwenye sherehe ya dada yake.Je nini kinaendelea usikose sura ya 8..