TAFUTA HAPA

SIMULIZI YA DADA YANGU SURA YA 4

Ilipoishia“James! Nimefikiria sana kuhusu ombi lako, nikatamani kukujibu usiku kwenye simu, lakini ulimi ulinikwama nikashindwa kuongea. Hivyo majibu ya ombi lako yako humu.” Alimaliza kuongea Upendo huku akimkabidhi James ile bahasha.

Inaendelea hivi,,,,,,James alipokea ile bahasha huku mkono ukitetemeka kidogo na kumwangalia Upendo usoni ambaye aliukwepesha uso wake na kuangalia pembeni kwa aibu. Kisha akaamua kuifungua bahasha na kusoma yaliyokuwemo ndani kwa makini huku akiinuka kumwangalia Upendo, ambaye sasa alikuwa amefunika uso wake kwa viganja vyake vya mkono. Haya ndiyo maneno aliyoyakuta James:

Mapenzi ni matamu kama asali wawili tukipendana.
Mapenzi ni machungu wawili tukisalitiana.
Mapenzi ni zawadi daima tukipendana.
Mapenzi ni lulu dhati tukipendana.
Mapenzi ni kufa na kuzikana.
Nakupenda JAMES!
Uwe Baba!
Watoto!
Wangu!

 Baada ya kumaliza kusoma ile karatasi James alimwendea Upendo na kumnyanyua kisha akamkumbatia huku naye Upendo akizungusha mikono yake na kumkumbatia James kwa nguvu kiunoni.
“Nashukuru sana mpenzi nakuahidi wewe ndio mke wangu.” Aliongea James huku akiendelea kumrushia mabusu motomoto, huku naye Upendo akijibu kwa kumbusu James ikiwa ni ishara ya kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa James na Upendo.


************* Baada ya miezi sita ********************

Baada ya mapenzi kukolea James aliamua kumtambulisha Upendo kwa wazazi wake.  Baba na mama wa James walimpenda sana na kuwashauri wafunge ndoa pindi tu Upendo akimaliza Chuo. Upendo alikuwa ndo anaingia mwaka wa mwisho ili ahitimu katika shahada ya Sheria. Kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele James na Upendo waliyafurahia sana mapenzi yao. Ili kuimarisha zaidi uhusiano wao James alimwomba Upendo waende kwa wazazi wake ili kutambulisha rasmi. Basi walipanga safari ya kwenda Morogoro ambako walipokelewa vizuri sana na wazazi wa Upendo. Baadaye wazazi wa Upendo waliwaasa juu ya uhusiano wao kuwa usiathiri masomo ya Upendo. Wazazi wake Upendo walishauri kwamba Upendo amalize Chuo kwanza na atafute kazi ndipo wafikirie suala la kufunga pingu za maisha.


Wakati James akiwa Morogoro mdogo wake Upendo alikuwa chuoni. Baada ya kukaa siku kadhaa Morogoro James na Upendo walirudi Dar es Salaam. Kutokana na ushauri wa wazazi wa pande zote mbili maisha ya James na Upendo yalikuwa ni ya furaha siku zote yenye mategemeo mazuri katika kuleta maendeleo ya maisha yao ya baadaye.

Akiwa chuoni Upendo alisoma kwa bidii sana na James aliendelea na biashara zake. Siku moja Upendo alimpigia simu mdogo wake na kumwambia juu ya uhusiano wake na James.
“Haloo! Mambo mdogo wangu! Mzima wewe! Habari za Chuo?” Ilikuwa ni sauti ya Upendo katika simu.
 “Nzuri ndugu yangu mambo magumu sana chuoni, bora wewe mwenzangu unakaribia kumaliza.” Alisema Eliza.
“We! Hakuna cha uafadhali wowote na hiyo mitihani inavyokuja migumu nimetingwa ile mbaya. Kumbuka wewe si ulisema ukienda chuo utajirusha sana. vipi imekuaje.” Aliuliza Upendo.

“Yaani, we acha tu ‘my sister’ (dada yangu) sina hata huo muda wa kujirusha nikicheza mbona nitafeli mmh nipe umbea maisha vipi.” Alihoji Eliza.
“We nawe kwa umbea, Eliza mwenzio nimepata mchumba nikimaliza Chuo naolewa.” Alisema Upendo huku akicheka.
“Usiniambie! Hongera mwaya, haya huyo shemeji anafanya kazi gani?” Aliuliza Eliza.
 “Ni mfanyabiashara na pia huwa anakuja Arusha mara kwa mara, nadhani mtaonana au ukija likizo utamwona. Nyumbani nilishampeleka kumtambulisha kwa wazazi.” Alieleza na kufafanua Upendo.“
“He! Kumbe mmefika mbali hivyo hata kuniambia mwenzio.” Alilalamika na kulaumu Eliza. 
Eliza huku akiwa na shauku ya kutaka kumfahamu shemeji yake, Upendo akajitetea;
“Wala sio hivyo ‘my young sister’ (mdogo wangu) mambo yalikwenda harakaharaka lakini, utamfahamu na wewe ndiye utakuwa mstari wa mbele kwenye harusi yangu.” Aliongea Upendo kwa majivuno.
“Haya bwana mimi nakutakia mafanikio mema Mungu awajalie mfikie malengo yenu.” Alisema Eliza basi wakaendelea kuzungumza na baadaye walikata simu na kuendelea na mambo mengine.

Kutokana na kazi kuwa nyingi za kusafiri mara kwa mara James alipata safari ya kwenda Arusha kikazi. Wakati huo ilikuwa ni kipindi cha mitihani kwa Upendo basi, waliagana.  Siku hiyo walikuwa pamoja ikiwa ni siku moja kabla ya James kuondoka .
“Mpenzi wangu, utanikosea sana ukichelewa kurudi si unajua nimekuzoea.” Aliongea Upendo kwa sauti ya mahaba.
“Usijali mpenzi ni kazi zinanifanya nisafiri nitawahi kurudi ila na wewe si una mitihani kwa sasa inabidi usome kwa bidii ili ufaulu vizuri sawa mama?” Aliongea James huku akimsogeza Upendo kifuani mwake na kumkumbatia.
 “Sawa lakini si unajua sipendi kukukosa siyo uende huko ukanisahau kwa kujirusha na vimwana vya Arusha.” Upendo alisisitiza.
 “Ina maana huniamini mamii nakupenda sana hakuna mwanamke wa kunidanganya wala usijali.” Alijibu James huku akitabasamu.
Walizungumza sana siku ile wakiwa nyumbani kwa James na baadaye walikwenda kupumzika. Nini kinaendelea usikose sura ya 5