TAFUTA HAPA

DADA YANGU SURA YA ...5..

Ilipoishia “Ina maana huniamini mamii nakupenda sana hakuna mwanamke wa kunidanganya wala usijali.” Alijibu James huku akitabasamu.
Walizungumza sana siku ile wakiwa nyumbani kwa James na baadaye walikwenda kupumzika. Nini kinaendelea usikose sura ya 5..........

Inavyoendelea.....  Kesho yake mapema saa mbili asubuhi James aliondoka na huku akisindikizwa na mpenzi wake hadi Uwanja wa Ndege tayari kwa kuanza safari.  Baadaye Upendo alirudi chuoni kuendelea na masomo. Alipofika Arusha James alikwenda moja kwa moja hadi katika hoteli  ya Ngurdoto yenye mandhari nzuri sana. Alipata chumba na baada ya kuingia kwenye chumba chake alimpigia simu mpenzi wake kumtaarifu kuwa amefika salama.

“Mambo mpenzi wangu! Nimefika salama nipo Hoteli ya Ngurdoto natamani tungekuwa pamoja,” Aliongea James kutoka Arusha.
“Hata mimi pia natamani tungekuwa pamoja mpenzi, ila majukumu ndiyo yanatubana. Hapa nilipo najisomea yaani hii mitihani inayokuja inaniumiza kichwa sana.” Aliongea Upendo kwa unyenyekevu.
Nakuomba usinisaliti mpenzi, najua kuna wanaume wengi wanakufuatafuata. Ziba masikio yako usisikie neno lolote kutoka kwa mwanamume yeyote. Alitahadharisha James.

 “Mmh we nawe kwa wivu, nakupenda sana siwezi kufanya hivyo hata siku moja.” Alijibu Upendo.
Baada ya mazungumzo kila mmoja aliendelea na mambo yake.
Akiwa Arusha James alianza kufanya kazi zilizompeleka akiwa na marafiki zake ambao ni wenyeji wa huko walizunguka sehemu mbalimbali ikiwa ni wiki mbili tangu James aondoke Dar es Salaam. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya Ijumaa muda wa saa mbili usiku ambapo James na marafiki zake walikwenda katika matembezi maeneo ya Sakina.

Walipofika huko walikunywa sana pombe huku wakiwa wanafurahi pamoja wakati huo walikuwa Sakina Bar, waliendelea kunywa hadi ilipofika saa tano usiku.
“Aisee washikaji kwa nini tusiende disko Triple A.” James aliyekuwa ameshalewa aliwashauri wenzake.
“Swadakta! Hilo neno! Washikaji twendeni disko sijaenda siku nyingi sana nadhani itakuwa safi sana.” Mmoja wao aliongea huku akionyesha ishara ya kuondoka.
Walikubaliana na kuanza safari ya kwenda ukumbi wa Disko wa Triple A ambao haukuwa mbali sana na mahali walipokuwa. Kabla ya kupanda gari waliokuwa nalo James alichukua simu yake na kumpigia Upendo.
“Haloo mamii vipi umelala mamaaa!” Aliongea James.
 “Safi mpenzi wangu nilale kwa raha gani niliyonayo? Hapa nilipo nipo bize sana  na maandalizi ya mitihani. Vipi uko wapi mbona nasikia kelele?” Alijibu na kuuliza Upendo.
“Nipo na washikaji tunafurahi mpenzi wangu. Mimi nakutakia usiku mwema.” Alijibu James ambaye hakusema kama alikuwa anaelekea disko.
 “Vipi James yaani huyo mwanamke amekubana mpaka umwambie unakwenda wapi? Kweli ninyi ndiyo wale hata ukitaka kula utampigia simu na kumwambia unachokula. Aaa! hebu twendeni alishauri Rama mmoja wa rafiki zake wapendwa wa James.
“Acha hizo Rama huyu mama watoto wangu na kuhusu disko sijamwambia kwani ingekuwa balaa muda huu”. Alijibu James huku akitabasamu.

Walipofika disko walikaa na kuendelea kunywa sana. Huko disko kulikuwa na watu wengi wakiwemo wasichana warembo sana ambao James na marafiki zake walianza kutafuta wasichana wa kucheza nao. James alisimama na kumfuata dada mmoja aliyekuwa amekaa karibu naye na kumuomba wacheze. Yule dada alikubali na kusimama na kuanza kucheza naye. Kama kawaida, katika kucheza kuna mambo mengi, wakiwa wanacheza James alimshika yule dada mkono na kumsogeza pembeni sehemu iliyokuwa haina kelele na kufanya mazungumzo naye.


“Mrembo umependeza sana, halafu unajua kucheza sijui unaitwa nani.” Aliuliza James huku akimwangalia kwa makini yule dada usoni.
”Asante kaka mimi naitwa Esta.” Alijibu yule msichana huku akitabasamu na kurembua macho.
“Una jina zuri sana Esta kama ulivyo mwenyewe.” Alisema James huku akimtazama Esta ambaye alikuwa akitabasamu.
  “Mbona wewe hujaniambia jina lako.” Aliuliza yule msichana.
 “Usijali mrembo mimi naitwa Juliasi.” Alijibu James.


Basi wakafahamiana na kuendelea kucheza pamoja baadaye James alimwomba Esta waondoke pamoja naye Esta alikubali na kuondoka huku akiwaacha marafiki zake bila hata ya kuwaaga. Walichukua teksi nje na kuelekea katika hotelini, wakiwa njiani walikuwa wamekumbatiana kila mmoja akimwambia mwenzake maneno ya kimahaba hadi walipofika hotelini na kuingia chumbani. Wakiwa ndani James alikuwa amechoka sana kutokana na pombe alizokunywa.  Lakini Esta yeye alikuwa amelewa kidogo hivyo alimsogelea James na kumvua shati taratibu pamoja na suruali yake kisha kumwacha akiwa katika bukta. Baada ya kumaliza kumvua kila kitu alimpandisha kitandani James akawa ametulia kimya kama vile amemwagiwa maji.

Naye Esta alivua nguo zake na kuziweka pembeni na kisha akamsogelea James.
“Juliusi we ni mwanamume mzuri sana nafurahi kuwa pamoja na wewe haijawahi kunitokea nikamwamini mwanaume kwa haraka kama ilivyo kwako nimekupenda naomba usiniache.” Esta aliizungumza maneno huku akiwa anamshika katika paji la uso naye James taratibu alinyanyuka na kuanza kumbusu Esta bila hata ya kuzungumza lolote huku akimkumbatia na baadaye walilala usingizi wa pono.Haya sasa James anamsaliti Upendo huku akimdanganya Esta kuwa anaitwa Juliasi nini kitaendelea usikose sura ya ...6..