Mazungumzo ya James na Upendo yaliendelea huku James akiendelea kuchombeza“Nikupe muda gani Upendo.” Alihoji James huku akishusha pumzi kwa nguvu. Kisha akaendelea kuongea. “Nashindwa hata kusubiri. Ila sawa nitakupa muda ili uweze kunifikiria, fahamu kuwa nakupenda na ni wewe pekee unaye utesa moyo wangu kwa sasa. Natumaini nitapata jibu zuri. Au siyo?” Aliuliza James huku akitabasamu na kuweka mkono wake wa kulia begani kwa Upendo. “Jamani mbona una haraka hivyo usijali tutaona itakavyokuwa.” Alijibu Upendo huku akitabasamu kama alivyofanya James lakini akiuondoka mkono wa James uliokuwa juu ya bega lake.
Baada ya hapo chakula kilikuwa tayari kimeletwa, walikula na kuendelea kunywa vinywaji vyao na kuzungumza mambo mbalimbali. Ilikuwa tayari imetimia saa tatu za usiku.
“Heh! Kumbe muda umeenda hivi hebu nirudishe hostel James, nina kazi za chuo sijazimaliza.” Alitamka Upendo.“Acha hizo Upendo yaani saa tatu tu ndo muda umeenda. Mimi ningependa twende na disko lakini kwa vile umesema kuwa una kazi za kufanya, sina namna ngoja tu nikupeleke. Ila tumalizie vinywaji kwanza.” Alishauri James.
Baada ya kumalizia vinywaji waliondoka kuelekea hosteli. Wakiwa njiani, James aliendelea kubembeleza na kusisitiza juu ya ombi lake.
“Please (nakuomba) usiache kunifikiria nakupenda sana Upendo.” Alisisitiza James.
Upendo alinyamaza kimya huku akimwangalia James bila kumjibu chochote. Walipofika hosteli kabla hajashuka katika gari James alimshika mikono yote miwili kisha akamkumbatia na kumbusu shavuni.“Nakupenda sana Upendo. Nakutakia usiku mwema na ndoto njema.” Aliongea James wakati akiendelea kumbusu huku Upendo akijaribu kumzuia. Mapigo ya moyo yalimwenda mbio Upendo, huku akijitoa kifuani kwa James. “James asante kwa yote nakutakia usiku mwema nawe.” Alishukuru Upendo kisha akashuka kwenye gari na kuingia hosteli huku James akiondoka kuelekea Kinondoni.
Usiku kucha Upendo aliwaza sana akimwaza James moyoni mwake.
“Mmh! Mmh! James ni kijana mtanashati siwezi kumpoteza nampenda pia. Lakini wanaume nao hawatabiriki, leo ananibembeleza sana akidai kuwa ananipenda halafu akinipata ataniacha. Ikitokea hivyo ataniumiza moyo wangu sana. Mmh! lakini sidhani kama James atakuwa hivyo, natamani awe baba wa watoto wangu. Sijui nimpigie simu ni mwambie sasa hivi! Lakini hapana! Aa! Hebu ngoja nimpigie sasa hivi.” Alichukua simu yake na kuanza kumpigia simu James,
Wakati simu ikiwa inaita Upendo alikuwa na hofu kubwa.
“Haloooo! Alipokea simu James.
“Yaani nilitaka kukupigia simu muda huu umeniwahi, niambie mpenzi wangu.” Aliongeza James bila kumpa nafasi upendo ya kuongea.
“Aha vipi James uko wapi? Unafanya nini saa hizi? Unajua kuna kitu nataka nikwambie ila basi, nitakwambia kesho, usiku mwema.” Akakata simu Upendo.
“Aah! Kakata simu.” Aliwaza James kisha akaamua kupiga yeye.
“Halooo! Mbona umekata simu kabla hatujamaliza maongezi? Aliuliza James
“Haya niambie ulichotaka kuniambia kwani natamani sana kusikia kutoka kwako la sivyo utanifanya nisilale.” Aliomba James.
“Hakuna kitu jamani James nilikuwa nataka kujua kama umefika salama.” Alijibu Upendo.
Usiku ule Upendo hakumwambia chochote James akabaki akijilaumu baada ya kukata simu huku akiwaza; “Hivi kweli nimeshindwa kumjibu! Ila kesho tukionana nitamwambia.” Upendo aliendelea kumwaza James hata kusoma kulimshinda usiku ule akaamua kulala.
Kesho yake ilikuwa ni siku ya Jumamosi, asubuhi Upendo aliingia darasani kujisomea kama kawaida yake. Ilipofika saa sita na nusu aliamua kurudi hosteli. Akiwa chumbani na rafiki yake Grace aliamua kutoka nje ili apate muda mzuri wa kutafakari kuhusu ombi la James. Alimuaga Grace na kumwambia kuwa atakuwa chini ya mti mkubwa ulio nyuma ya hosteli akijipumzisha.
Baadaye James alikuja pale chumbani kwa Upendo bila taarifa, baada ya kugonga mlango na kuruhusiwa kuingia alimkuta Grace akiwa amejilaza kitandani akisoma gazeti.
“Habari gani dada!” Alisalimia James.
“Nzuri kaka karibu kiti.” Alijibu Grace.
“Asante dada. Aaahmm! Nimemkuta Upendo?” Aliuliza James huku akitabasamu.
“Ndiyo! Ila yupo nje amekaa chini ya mti mkubwa nyuma ya jengo hili.” Alijibu Grace huku akiamka na kukaa vizuri kitandani.
“Haya asante hebu nimfuate.” Aliaga James na kuondoka.
Upendo alikuwa amekaa kwenye kiti cha plastiki huku amegeukia uzio unaozunguka hosteli akichezea tawi dogo la mti. Mara James alikuja kimyakimya akitokea kwa nyuma na kumziba Upendo usoni bila ya yeye kumwona akiwa amebeba chakula kwenye mfuko. Upendo alishtuka sana katu asijue ni nani aliyemziba macho.
“Nani tena jamani? Mimi huwa sipendi michezo ya hivi.” Alilalamika Upendo.
“Usiogope Upendo ni mimi.” James alitoa mikono yake na kumbusu Upendo.
“Waoo! James mbona hukunipigia simu kunitaarifu kama unakuja?” Aliuliza Upendo huku akisimama kupokea mfuko aliokuwa ameubeba James.
“Nimekuletea chakula cha mchana Upendo.” Alitamka James bila kujibu swali aliloulizwa
“Mmh! Nilijua ni watu wameamua kunichokoza. Asante sana kwa kuniletea chakula, umejuaje James kwani mpaka saa hizi sijala njaa inaniuma kweli. Ehee! umeniletea chakula gani?” Aliuliza Upendo.“Fungua uone.” Alijibu James.
“Ooh! Chipsi na kuku napenda sana chakula cha aina hii, vipi njoo basi tule wote.” Aliongea Upendo kwa shauku huku akimalizia kufungua mfuko.
Upendo alichukua maji ya chupa aliyokuwa nayo na kumwomba James anawe mikono ili wale wote. “Hapana mimi nimeshakula we kula tu usijali nimekuletea wewe.” Alijibu James huku akipokea chupa ya maji ili kumnawisha Upendo. Akiwa anaendelea kula Upendo alikuwa ana mawazo mengi sana juu ya James.
“Upendo napenda sana uwe mke wangu, kwa nini unaamua kuutesa moyo wangu hivi?” Aliuliza James huku akimwangalia Upendo kwa kumtamani.
“Kwanini unasema nakutesa James nataka tu kuwa na uhakika kwani naogopa sana kudanganywa.” Alijibu Upendo huku akimwangalia James kwa kurembua macho.
“Niamini Upendo, mimi kamwe siwezi kukudanganya nakupenda kutoka moyoni mwangu.” Alijibu James huku akimkazia macho upendo.
“Kweli James? Hata mimi nakupenda sana James ila...” Alisita Upendo.
“Ila nini.” Aliuliza James huku akiweka mkono wake begani kwa Upendo.
“Ngoja nije.” Aliinuka Upendo kuekelea chumbani kwake akimwacha James akishangaa kulikoni.
Baada ya dakika kama tano, Upendo alirudi akiwa ameshika bahasha mkononi iliyoandikwa “JAMES” ambayo aliiandika usiku ule, ili wakionana ampe. James alimwangalia Upendo kwa mshangao asijue chochote.
“James! Nimefikiria sana kuhusu ombi lako, nikatamani kukujibu usiku kwenye simu, lakini ulimi ulinikwama nikashindwa kuongea. Hivyo majibu ya ombi lako yako humu.” Alimaliza kuongea Upendo huku akimkabidhi James ile bahasha. Mambo ndiyo yanazidi kunoga nini kitaendelea. usikose sura ya ....4......