TAFUTA HAPA

HADITHI: Utamu wa Sukari Guru- 8

Mara ya mwisho tulipoachana kibua katika anga zake aliwasili mtu mwingine, ambaye jinsi alivyofanana na mwenye nyumba, alichoka na kujikuta kitu fulani kinashuka taratibu katika mwili wake. Akajisahau kusema karibu.  sasa endelea


"Hapa ni nyumbani kwa Luteni kanali Richard" alisema mvulana yule kwa bashasha baada ya kukutana na mtu asiyemfahamu na ambaye anamkodolea macho tu wala hasemi kitu.
"Ahh Chioma, samahani nina tabia mbaya Karibu"
"Umelijuaje jina langu?"
"Ni kukudhihirishia kwamba hapa ndipo nyumbani kwa baba yako, tukupokee mzigo"
"Tumeshafika, wapi wazazi wangu"
"Wako kazini unadhani wanaweza kuwa wapi saa hizi?"
"Nakuuliza wewe manake walistahili kuja kunipokea"
"Mkubwa wewe na unamjua mama yako anafanya nini na baba yako anafanya nini kama wote wako nje unasema vipi?"
"Ahh ni hamu tu ya kuwaona" alisema akianza kuvuta hatua. Kibua alimpokea sanduku lake na kutangulia naye kumpeleka chumbani kwake.
" Karibu tena Chioma"
"Mhh Aksante ... " alivuta maneno kidogo kuonesha nia fulani na Kibua aliinyaka:
"Kibua"
"Kibua"
Kibua aliweka sanduku lile na kuanza kuondoka wakati Chioma alipomsimamisha.
"Kibua"
"Labeka"
"Aksante"
"Aksante kwa kushukuru lakini ni kwa lipi hasa mpaka unishukuru"
"Ulivyotengeneza chumba changu"
"kwanini uamini ni mimi ambaye nimekitengeneza?"
"Huwa nakikukuta kama nilivyokiacha"
"Mama aliniambia jana nitengeneze chumba hiki na anayekuja kulala ni mvulana kwa hiyo nimefanya kwa kadri ya uwezo wangu.Naelekea shule kwa sasa lakini chakula ki tayari mesini."
"Hautakuwepo?"
"Hapana nimechelewa kwa sababu ya kukusubiri lakini kwa kuwa umeshaingia wacha niwahi shule."
"Pasi shaka naipenda hiyo. Nyumbani kuna msaidizi ambaye anakwenda shule"
"Utapenda vitu vingi sana" akasema kama kwa kujishaua huku anakimbia mdogomdogo.
Chioma alishangaa, hakuweza kutambua kama nyumba ile ina heri au ina balaa, alikuwa amechoka alihitaji kuoga, kulala na kisha aende kutafuta chakula hakuwa na haraka nacho.
Kibua kwa upande wake aliona ni afadhali akamalize mitihani yake aende kidogo kupumua nyumbani. Mtoto wa mwenye nyumba alikuwa dhahiri anaitesa roho yake na hakujua yuko salama kiasi gani.
****
Wiki moja ilikuwa imepita tangu Chioma arejee pale na kila juhudi anayoifanya awe karibu na kibua  ilikuwa inasomwa mapema na kutafutiwa geti kubwa mithili ya lango la gereza la Ukonga, lile linalolinda watu wenye kuhisiwa mashaka duniani.Haikuwa rahisi kufikiria kitaendelea nini kwani binti alikuwa mjanja mno na hakuelewa kama kwa namna ile atafanikiwa.
Lakini siku moja  alifanikiwa kumbana binti yule.
"Mbona unanikimbia kila ninapotaka kuzungumza nawe?"
"una mazungumzo gani nami"
"Nataka kukujua inakuaje?"
"Si unanijua naitwa Kibua, msaidizi wako unahitaji nini?"
"Zaidi ya hayo unayosema, kukufahamu"
"ili itokee nini?"
"Mkubwa wewe"
"Sijui, lakini semtensi yako ina maana nyingi just be specific"
"Duhh mfanyakazi wa ndani anazungumzi kiingereza,tunatoka taratibu katika ukoloni"
"Hujaambiwa kwamba nasoma?"
"Anambie nani nawe hukai hata sebuleni , saa zote kwenye kota yako"
"Ndiko visonoko siye tunakostahili kuishi"
"Naona unabadilisha topic, nambie"
"Jamani Chioma mimi niseme nini"
"Nambie tu kama tunaweza kupata happy Hour"
"Nikuambie ukweli"
"Ndio"
"Sikuelewi"
"Haiwezekani"
"kisichowezekana nini?"
"Kusema ninachosema chote hukielewi"
"Wewe msomi unashindwa nini kujieleza"
"Haya ngoja niseme mimi.. mimi.. mimi"
"Naona unashikwa na kigugumizi"
"Yote kwa sababu nakupenda halafu sijui nifanye nini na wewe"
"Mtu kumpenda dada yake ni dhambi kweli?"
"Ha nikupende kama dada angu ? La hasha mimi nakupenda kama mwanamke?"
"Maneno hayo Chioma umeshasema kwa watu wangapi"
Alisita kusema, akamshangaa akamuona kwamba ni mwanamke mwenye tabia ya ajabu kabisa ambayo hajawahi kukutana nayo ikizingatiwa kwamba yeye ni mvulana handsome.
"Naona nimekukwaza. kwaheri.jipande bado una muda wa kusema unachotaka"
"Ninachotaka ni mapenzi kwako, nataka kukujua nataka kukuoa"
akageuka akamtazama kwa upendo mkubwa.
"Mimi mama yako wewe, huwezi kunioa"
Akaduwaa.
Wakati anatafakari jibu baba na mama yake wakaingia kwa pamoja, wakawaondoa wale wawili katika malumbano ambayo huenda yangelimwaga matama zaidi katika eneo ambalo halistahili.
"hii dady"
"Hi son!"
Walisalimiana kabla ya kumkumbilia mama yake kumbusu na kumpokea kifurushi kilichokuwa na mapochopocho. wakati anageuka mzee alikuwa anamtazama Kibua ambaye rangi yake ya tunu ilikuwa inameta na hata macho yake yalikuwa kama ncha ya almasi iliyopigwa na jua kwa uwako wake.
"Mlikuwa mnazungumza nini?"
"Tulikuwa tunaambizana mambo mbalimbali, mimi nampa michapo ya nyumbani kwetu na yeye akawa ananisimulia shuleni kukoje?"
"Sawa" alisema huku akiwa haamini kwani alimuona mwanawe akiwa na macho makali, dalili ama palikuwa na ugomvi au palikuwa na mapenzi kwani yote mawili yanaweza kuwa sawasawa.

itaendelea