TAFUTA HAPA

Hadithi: Utamu wa Sukari Guru 16

Naam ugomvi kati ya Kibua na Semie umeshamalizika na kwa maneno yake mwenyewe Kibua amekubali yaishe.Je kuna jipya gani litazuka hasa ukizingatia kwamba Kibua anajua baba yake amemkataa. Kumbuka safari iliyopita kuliletwa kondoo pale nyumbani kwa akina Kibua.Ambatana name kwenye simulizi hili lenye mihemko ya mapenzi.


KIBUA aliporejea nyumbani kutoka kwa akina Semie alikuwa amechoka sana.Hii ilitokana na ukweli kuwa alikuwa ametumia nguvu za ziada kumwadhibu Semie na mume wake.Ni matumizi ya nguvu hizo zilimfanya arejee nyumbani pale kimya kimya, akamsalimia mama yake na kwenda kulala bila kuoga.
Katikati ya usiku ndoto zilimwamsha, zilikuwa si ndoto rafiki  akakumbuka kwamba katika maisha yake hajawahi kulala na janaba na ndio maana akili ilimcheza, akatoka akaenda jikoni akakuta mama yake ameinjika maji katika chungu na vijinga vya moto vilikuwa bado vinawaka.Asingeliweza kulala hadi asubuhi, kwani mwili wa Kibua ulikuwa si wa kawaida, uligombana mno na uchafu.
Akachukua maji yale akayachanganya vyema na kuelekea uani, mwanga wa mbalamwezi ulimpa kampani kubwa akaamua kujiogea nje kwani hakuna haja ya kwenda bafuni katika usiku huo mkubwa.Akasaula nguo zake akazitupa upenuni, akaanza safari ya kujiogesha, ilikuwa safari ndefu na aliifanya kwa utaratibu sana.
Pale alipokua akiogea palikuwa karibu sana na chumba ambacho mama yake analala, zile kelele za maji zilimwamsha bi mkubwa Yule.Huku akipepesuka kwa usingizi alikwenda  kufungua mlango wake akatoka nje na kuona mlango wa nje umesindikwa tu.Akaufungua na kumuona mtoto wake akioga kwa taratibu sana, hakutaka kumshtua kwani alionekana kama vile yuko mbali sana. Kila kata ya maji ilionekana kuwa na kusudio fulani katika mwili wake.
Alimsubiri amalize, lakini ilionekana kwamba itamchukua muda mrefu sana. Alipoona sasa anakwenda kasi akajua kwamba akili imemrejea na akaamua kumuita.
“Kibua”
“Unasemaje mama” alijua ni mama yake.
“mbona chilo chikulu (usiku mkubwa)vipi mwanangu?”
“mama nilirudi nimechoka sana, nikasema nijipumzishe kumbe ndio nimelala.Nimeshtuka nikiwa naota ndoto mbaya sana,nikagundua ahaa kunbe sijaoga ndio naoga mama”
“umechukua muda mrefu sana mama kuoga”
“Ha mama yaani kumbe muda wote huoupo unaniangalia tu?Nimekuwa mwanasesere?”
“Kwangu mimi wewe ni mwanasesere, kwa wengine wewe ni mtoto  na kwa wanaume wewe ni mwanamke.Haya tuache hayo.Nilikuwekea ugali na mboga ya beze ikichanganyika na konge.Konge lakini lipo peke yake .Utahitaji kula si vyema kulala na njaa, bado sijafa.Kabla sijasahau kesho kuna ugeni hapa nyumbani usiondoke.”
“Enhee kuna ugeni gani mama wa mwanasesere?”
“Kwani lazima uujue mama”
“kweli kabisa si lazima niujue, lakini si unanijua mwanao ninapokuwa na mambo yangu hakafu kuna vitu ambavyo si vya lazima kuvifanya?”
“Najua”
“Haya”
“Sikia Kibua nadhani hapana usitoke.Nadhani ni vyema ukabaki.Nadhani kuna mambo baba yako anataka kusema nawe”
“Achana naye mama.Nimeenda kanizodoa, sina shida naye. Nimemjua,nimemwelewa. Yangu kuanzia sasa ni macho tu”
“hapana mama nadhani kuna kitu anataka kukifanya kwako.Kaletwa mnyama hapa ni dalili kwamba baba yako anataka kupata nawe.”
“Hapana mama nilimwambia kwamba kama yeye si baba yangu basi amruhusu Siri alete posa, hiyo ni posa mama”
“Haiwezekani si posa! Wale ni wanyama wa tambiko walioletwa hapa”
“Ndio mama, tambiko la kutenganisha ukoo,sijui nitazaa Mtitu mimi Dah”
“kama hilo sitakubaliana nalo”
“Ndio maana nikasema wala usimsikilize alishamaliza mambo yake”
Mama Kibua alimtazama mwanae akamuona ametulia sana.Akajua kwamba sasa mwanae huyo wa pekee ataanza kufanya maamuzi kama aliyoyafanya yeye na lile lilimpatia shida, hakuyapenda na hajawahi kupenda maamuzi yale.
“Sikiliza Kibua”
“Unasemaje mama?”
“Nenda kale, kisha kalale nina hakika mpaka kesho utajisikia vyema sana. Wala usiondoke tuwangoje tuwasikilize”
Hakusubiri amjibu aliondoka kurejea chumbani kwake akimwacha Kibua akipiga mwayo huku naye akienda jikoni kupata chakula kama mama yake alivyomshauri.
XXX
Huku Dar es salaam mambo hayakuwa kama vile yalivyokuwa yakitarajiwa kuwa.Mtotobaba mwenye nyumba kama baba mwenyewe alivyokuwa alianza kuchongeka. Na kikubwa alichokuwa anakifikiria ni jinsi alivyomkosa Kibua , mwanamke wa haja ambaye alidhani kwamba anafaa sana kuwa  mtu wa kumkosha katika nafsi yake ya upweke kwa jinsi binadamu walivyoumbwa.
Wakati wa mtoto anachongeka akiakili na kimwili kwa ajili ya Kibua na hasa akitafakari maneno ya baba yake,  kwamba Kibua ni mama yake mdogo na hana la kufanya,baba mtu naye aliona miezi minne kama mwaka. Hali haikuwa njema ingawa mkewe kwa mara ya kwanza alianza kuwapo nyumbani kwa muda mwingi sana kuliko awali na alikuwa akijitahidi kupika walimu mtamu ambao yeyhe alijua kabisa ameukozesha nazi.
Mama alijitahidi sana kuhakikisha kwamba tui analotengenezea wali limekoza na lipo shatashata lakini mzee mzima kila akila wali ule alikuwa kama vile anataka kuutema.Ilifika siku akaamua kumuondolea uvivu na kumchana laivu.
“Enhee nambie kanali wa jeshi, komando” akajenga uso wa tabasamu kisha akaendelea siriazi kidogo;” kuna tatizo gani siku hizi mbona kila ukila unazidi kunyong’onyea?”
Alimtazama, yale macho ambayo baba mwenye nyumba anayajua, ya baridi. Hakumuelewa.
“Sina tatizo lolote lile kwani vipi?”
“Asiyekujua atasema upo sawa, sisi wengine tunakujua.Tueleze baba chanja tatizo nini?”
“sina tatizo mama”
“Kweli kabisa?”
“Ndiyo”
“Au ndio mawazo ya Kibua.Yule mtoto kakupa nini hasa?”
“ushaanza”
“Wala Mwaya!Lakini dawa ya maradhi  yasikuue kwanza ni kuyakubali, kisha kutafuta dawa yake, kuyakataa wakati yanakutesa si sahihi.Nataka kusema hivi baba chanja dawa ya maradhi yako ni kukiri, usipofanya hivyo utakufa utaacha kila kitu pamoja na Kibua mwenyewe”
“unanitaka nini?”
“Mimi nauliza Yule mtoto kakupa nini mpaka unachanganyikiwa?”
“Mbona hivyo mama watoto?”
“kuna mawili ama wewe ni mjinga ama hutaki kukubali hofu yako.Utakufa kw akihoro mpenzi”
“kama hakuna maongeze hapa sebuleni ila hayo, basi naomba twende tukalale”
“huwezi wewe”
“Kwanini siwezi”
“Nikuambie ukweli?”
“Nambie”
“Sasa hivi staili na miondoko ni ya Kibua. Umekwisha wewe!Hufurukuti”
“Mhh”
“Mhh nini?Kila siku ukikolea unaliita jina lake na halafu unasema hivi..” akaaenda kumnong’oneza sikioni.
“Sio kweli”
“Ukweli ni nini laazizi?Nambie basi”
“Ninachotaka kusema unachosema si cha kweli mimi si mvulana bana”
“Unaona sasa?”
“Ninaona nini”
“mimi nishampoteza mpenzi na mapenzi yako kule.Siku zote hizi unajisikia kuniamrisha kama jeshini fanya hivi, kaa hivi kama unapiga picha ya mmodo khaa,”
“na wewe unafanya”
“Nifanyeje na bwana mkubwa kesha jenga mazoea.Tusipofanya si tutaharibu picha nzima”
“Mazoea?Mazoea gani”
“Hivyo unavyoagiza”
“Sikiza…” akakatwa kauli.
“Nisikilize mimi babachanja.Simchukii mtoto Yule! Lakini jinsi unavyokwenda na damu changa ile utatuletea majanga nyumba hii! We endekeza tu” akanyanuka kuelekea chumbani.
Hakujibu lilikuwa limepigwa chini ya mkanda mzee mzima ilibidi atulie kusikilizia maumivu.Akagundua kwamba  hawezi tena kuficha mkewe alikuwa anamjua alipolala na alipoamkia.
Itaendelea