TAFUTA HAPA

HADITHI NZURI YA MAPENZI


 HADITHI NZURI YA MAPENZI

Mume wangu ni mhandisi, ninampenda sana, kiukweli napenda sana muda mwingi kuwa nae karibu.

Miaka mitatu ya uchumba na miaka miwili sasa katika Ndoa, naweza nikakubali kwamba hivi sasa nimemchoka.

Sababu kubwa ya kumchoka ni kutokana na yeye alivyobadilika tofauti na mwanzo.

Mimi ni mwanamke ambae napenda sana kudekezwa na niko 'sensitive' sana katika suala la mahusiano na hisia.

Kila siku namlilia mume wangu juu ya mapenzi aliyokuwa akinionesha mwanzoni kama mtoto anavyolilia pipi.

Ila mume wangu amekuwa mbishi na hataki kurejesha yale mapenzi ya mwanzo, hii imenifanya niichoke sana ndoa yangu mapema.

Siku moja niliamua nimueleze maamuzi yangu kwamba nataka talaka yangu.

"Kwanini?" aliniuliza huku akinishangaa. "Nimechoka, hakuna sababu ya kila kitu duniani!" nilimjibu. Alibaki kimya usiku mzima, kwa hili alinikatisha sana tamaa, nikajiambia kuwa mume ambaye hataki hata kunibembeleza juu ya haya maamuzi yangu, wala hataki kutoa maoni yoyote, mimi wa nini sasa?

Ila mwishoni aliniuliza, "nifanye nini ili ubadili maamuzi yako?"

Kuna mtu ashawahi sema kwamba, ni vigumu mno kubadili maamuzi ya mtu mzima, na mimi nafikiri nilikuwa nishaamua kufanya hayo maamuzi kutokana na kutokuwa na imani nae tena.

Nilimwangalia machoni mwake na taratibu nikamjibu; "Hili hapa ni swali langu, ukiweza kulijibu ninaweza nikabadili maamuzi yangu, mfano nikakwambia nataka ukanichumie ua ambalo lipo upande wa mlima mrefu, na wote tunao uhakika kwamba kwenda kulichuma hilo ua kutakusababishia kifo. Utafanya hivyo kwa ajili yangu?

Akaniambia kwamba majibu atanipa kesho, matumaini yangu yakapotea kwa hilo jibu lake la mkato.

Niliamka asubuhi na kukuta ameshaondoka kwenda kazini, nikaona kipande cha karatasi kilichoandikwa kwa mkono chini ya bilauri ya maziwa katika meza ya chakula.

Kilisomeka hivi "mke wangu mpenzi, jibu langu ni kwamba sitaweza kulichuma hilo ua, ila niruhusu nikuelezee sababu za kutolichuma....." niliposoma tu aya hii ya kwanza moyo wangu ukaniuma kweli, nikawaza kumbe kweli huenda hanipendi anataka niondoke.....

Nikaendelea kusoma, "mke wangu sababu zenyewe ni hizi, unapotumia kompyuta yako mara nyingi hua unakosea kuitumia vizuri na hulia mbele ya kompyuta kwamba hujui umeharibu nini, mimi hutumia muda wangu kukuelekeza namna njema ya kutumia...

Mara nyingi tunavyoenda kazini asubuhi wewe husahau funguo zako za nyumbani, na hua unawahi kurudi wewe nyumbani, hivyo hunibidi mimi nirudi nyumbani kukufungulia mlango halafu nirudi tena ofisini...

Unapenda kukaa peke yako nyumbani, hua nina hofu juu ya upweke wako hivyo hua najitahidi nikitoka ofisini nije kuongea na wewe na kutaniana ili kukuondolea upweke...

Unapenda sana kuangalia TV, ninahofu sana utaharibika macho, ninajitahidi niyatunze yangu ili tutakapokua wazee wote tusiwe na muono hafifu, ili nikushike mkono na kukuongoza kokote tutakapokuwa tukitaka kwenda..."

Mara nyingi unavyoniambia hujisikii vizuri mimi huingia jikoni na kukutayarishia chakula ukipendacho......

Hivyo basi mke wangu, labda kama kuna mtu mwingine anakupenda zaidi yangu, mimi siwezi kulichuma hilo ua nikafe na kukuacha peke yako..."

Machozi yakanidondoka.....na nikaendelea kusoma..."sasa umemaliza kusoma jibu langu, kama umeridhika tafadhali fungua mlango wa mbele wa nyumba nimesimama nje nikiwa nimekubebea mkate na maziwa uyapendayo.."

Nilikimbia haraka na kwenda kufungua mlango, na kweli nilimkuta akitabasamu na huku akiwa amebeba mkate na maziwa niyapendayo....

Sasa nina uhakika kwamba hakuna anayenipenda zaidi yake na nimeamua nimzuie asiende kulichuma hilo ua.

_____________________________________

Maisha ndivyo yalivyo. Pale mtu anapokua amezungukwa na upendo, mara nyingi huweza kujisahau na kuona ni jambo la kawaida tu kwa vile mapenzi yapo.

Mapenzi hujionyesha kwa namna mbalimbali, hata kwa namna zilizo ndogo kabisa. Hakuna 'standard form' ya mapenzi. Ila kujaliana ni msingi imara wa kukuza mapenzi kati ya wawili wapendanao kweli.