Kama umeshushwa thamani unakuwa  kwenye hatari ya kuachwa. Hata kama mwenzako alikuwa ameshafikiria suala  la kuingia kwenye ndoa na wewe lakini kwa sababu ameshakushusha thamani  ndoa inaweza kuyeyuka.
Ukiwa kwenye ndoa ni hatari zaidi  maana mwenzako hukuchukulia wa kawaida – mazoea huzidi na hapo ndipo  uhitaji wa kuwa na mwingine wa pembeni unapoanzia. Haoni cha muhimu tena  kwako, ndiyo maana wazo hilo huvamia ubongo wake kwa kasi sana.
Itafikia hatua, kama upo ndani ya  ndoa, mwenzako atagoma kuongozana na wewe na kama ikitokea hivyo  mkikutana na rafiki zake njiani hatakutambulisha. Hisia kwamba  hamuendani humwingia.
UNAFANYAJE SASA?
Kubwa unalotakiwa kufahamu rafiki  yangu mpendwa, suala la kupanda au kushuka thamani lipo mikononi mwako.  Yapo mambo ambayo ukiyazingatia, mwenzako hawezi kukuchoka na kufikia  hatua ya kukushusha thamani.
Tayari tumeshaona athari zake  lakini hapa sasa nataka kukupa mbinu ambazo ukiwa nazo makini basi  itakuwa rahisi kwako kubaki namba moja na mtu muhimu zaidi (ndiyo  inavyotakiwa kuwa) kwa mpenzi wako maana ni haki yako.
ANZIA MWANZO
Ni rahisi zaidi kulinda thamani  yako kuanzia mwanzo wa uhusiano wenu. Ikiwa tayari mmeshakomaa halafu  tatizo hilo likajitokeza, hutumika nguvu nyingi zaidi kulirekebisha  kuliko kujizatiti kuanzia mwanzo wa uhusiano. Ni mambo gani hayo? Twende  hapo chini.
CHUNGA KAULI ZAKO
Naomba ieleweke wazi kuwa mada  hii ni maalum zaidi kwa wanawake. Kitu muhimu cha kwanza kabisa kwa  mwanamke ambaye anataka kuilinda thamani yake kwa mpenziwe ni kupima  sana kauli zake.
Acha kuropoka hovyo, pima maneno  yako na ikiwezekana kama unadhani kuna jambo huna uhakika nalo  usizungumze kabisa. Katika eneo hili, uwe makini zaidi mnapokuwa na watu  wengine. Kama mwanamke usiwe mchangiaji hoja sana.
Utulivu wako unaweza kuwa silaha kubwa ya kukufanya ubaki na thamani yako kama mwanamke anayejitambua.
USIRUHUSU MAPENZI
Msichana mwenye kujitambua na  kufahamu thamani yake sawasawa hawezi kuruhusu mwili wake ujulikane na  mwanaume harakaharaka. Onesha unajitambua na usikubali kirahisi kuuacha  mwili wako uchezewe.
Mpe hoja; kwanza mapema, hajakuoa  wala kukuchumbia, haraka ya nini? Wakati unawaza kuhusu kutoa penzi  lako, lazima ufikirie kuhusu athari zinazoweza kukupata kwa kukurupukia  mapenzi. Mwanaume ambaye bado hamjachunguzana na huna uhakika naye wa  kutengeneza maisha, kichwani mwake hakuweki kwa asilimia kubwa.
Ukumbuke kwamba, ukipata matatizo  yoyote – binafsi au yanayosababishwa na uhusiano wenu, anakuwa hana  uwajibikaji wa asilimia kubwa kwa tatizo hilo. Utabaki wewe na matatizo  yako!