“Nini kinaendelea hapa?” Alihoji mmoja wa askari polisi wawili ambao waliingia ndani, mmoja wao alikuwa na silaha ya moto. Swali lile halikujibiwa hivyo askari wale wakaamua kuendelea na jambo ambalo liliwapeleka pale, “tuna shida na James” alisema askari ambaye hakuwa amebeba silaha, James akajitambulisha kwamba alikuwa ni yeye, askari yule akatoa pingu na kuanza kumfunga huku akimwambia kuwa alikuwa chini ya ulinzi. James aliishiwa nguvu, akakosa hata swali la kuhoji, akatii maelekezo ya askari wale ambao walimtaka kuelekea kituoni. Monica alikuwa tayari amejua kilichopelekea James kukamatwa lakini Paul bado alikuwa gizani, japo hakuweza kuhoji chochote, alibaki akiwa amepigwa na bumbuwazi wakati James akiondoka na polisi wale.
“Nilikuonya kistaarabu kabisa lakini hukutaka kusikia, sasa tusilaumiane kwa maamuzi ambayo nitachukua” alisema mama Julieth ambaye walimkuta kule kituoni. James akaingizwa mahabusu akimuacha mama Julieth akiwa anaongea na askari wale. “Kwahiyo mama tunamfungulia kesi?” Aliuliza askari ambaye alionekana kupokea maelekezo ya nini afanye ama nini asifanye kutoka kwa mama Julieth. “Ngoja kwanza, mzee amesema tumaubirie. Ataingia usiku” alisema mama yake Julieth akimtaka askari yule kungojea baba yake Julieth afike kutoka ughaibuni ambako alikuwa akifanya kazi.
Mara simu ya mama Julieth ikaita, ilikuwa ni namba ngeni kwenye simu yake. Akaipokea na kupata habari ambazo zilimchanganya na kumfanya aondoke pale kituo cha polisi mbio mbio.
*******************************************
Baba yake Julieth alipotua tu akakutana na habari ambazo hazikuwa nzuri hata kidogo, Julieth alikuwa mhututi hospitali baada ya jaribio la kujiua. Moja kwa moja akaenda hospitali ambapo alimkuta mkewe akiwa amechanganyikiwa akisubiri kuona kama jitihada za madaktari zingetosha kuokoa maisha ya mwanae, wakaungana kusubiri pamoja huku wakiendelea kumuomba Mungu anusuru maisha ya mtoto wao wa pekee.
******************************************
“Hali ya mgonjwa inazidi kuimarika, tumemtundikia drip ya maji ili kuweza kupunguza kiasi cha sumu ambacho tayari kipo kwenye mzunguko wa damu, itachukua muda kidogo hivyo mngeenda kupumzika tu” yalikuwa maneno ya daktari ambaye alikuwa akimshughulikia Julieth. “Tafadhali docta, fanya kila uwezalo mwanangu apone” alisema baba yake Julieth ambaye alionekana kuchanganyikiwa. “Hali yake inazidi kuboreka, tumuombe Mungu tu” alisema daktari yule kwa kifupi kisha akawaacha na kwenda kuendelea na majukumu yake.
********************************************
Kule kituoni majira ya saa kumi za jioni James akatembelewa na shemeji yake, Monica, ambaye alijaribu kumdhamini lakini ikashindikana. “Tuhuma alizonazo mtuhumiwa ni miongoni mwa tuhuma mbazo hazina dhamana, hii ni kesi ya ubakaji” alielezea mkuu wa kituo ambaye Monica aliomba kuonananaye baada ya askari aliyekuwa zamu kimnyima dhamana. “Jambo unaloweza kumsaidia ni kumtafutia wakili mzuri tu, maana kama atashindwa kesi hii mtuhumiwa atahukumiwa miaka mingi sana”. Maneno yale yalimkata maini Monica, akakaa kimya kwa muda, kisha akapata cha kusema. “Naweza kumuona?”, hili halikuwa gumu kwa mkuu yule wa kituo, akaagiza Monica apelekwe ambapo angeweza kumuona James. James alipigwa na butwaa kuona Monica alidiriki kumfuata tena mpaka kule baada ya kuwa wamefumaniwa muda mfupi uliopita. ” kaka anajua kama umekuja huku?” Alihoji James. “Sina mpango tena na kaka yako, wala sina ndoa naye tena, sasa nafanya ambacho najisikia” aijibu Monica na kumfanya James azidi kuchanganyikiwa, Paul alikuwa amechangia kwa kiasi kikubwa kumfikisha ambapo alikuwepo kielimu, alijiona mkosaji sana kumvunjia ndoa yake. “Shem nakuomba ufanye kila uwezalo kuhakikisha hamuachani, hivi nani atanielewa hata huko nyumbani wakisikia mimi ndo chanzo cha kuachana kwenu?” Aliongea kwa uchungu mkubwa James ambaye aliona kama maisha yake yalikuwa yameharibika tayari.
“Sina mpango wa kurudi kwa Paul, mimi nakupenda wewe James. Mpango wangu ni kuhakikisha unatoka kisha tukaishi mbali, ambako hatutopata usumbufu wa mtu yeyote” alisema Monica..
********************************************MWISHO******************************