TAFUTA HAPA

HADITHI: Damu, mabusu na machozi SEHEMU YA KUMI

Alitamani kumshirikisha mama yake katika tatizo alilokuwa nalo lakini alishindwa angeanza vipi! Alihisi angeonekana mjinga. Alitembea kwa unyonge kichwa chake kikiwa kimejaa mawazo mengi, mbele kidogo alitengana na akina mama aliokuwa nao na yeye kuendelea na safari hadi nyumbani kwao.
Hakumkuta mama yake lakini mlango ulikuwa wazi, alifungua na kuingia, mezani alikuta kipande cha karatasi na kukichukua, juu yake kiliandikwa jina lake, ilikuwa ni barua kutoka kwa mama yake! Aliisoma mwanzo mpaka mwisho, hayakuwa maneno mengi zaidi ya taarifa kuwa mama yake aliondoka kwenda kituo cha polisi kama yeye Nancy angeweza basi amfuate huko.
“.....lazima niondoke kwenda Tabora sasa hivi! Tena imekuwa vizuri sijamkuta mama!” Aliwaza Nancy akikimbia kwenda chumbani kwake ambako alianza kupanga nguo katika begi, kutoka hapo alikimbia tena chumbani kwa wazazi wake, alielewa mahali pesa zilipohifadhiwa! Hivyo alichofanya ni kufungua kabati na kutoa shilingi milioni moja katika pesa zilizokuwepo.
“Mama atanisamehe sana! Nafanya hivi kumsaidia baba, ninachotakiwa kufanya sasa hivi ni kuwahi Tabora haraka iwezekanavyo na kama nitamkuta huyo mganga na akaniondolee balaa nililonalo mwilini nitarejea haraka iwezekanavyo nikiwa tayari kufanya lolote na Danny!” Aliwaza Nancy.
Alitoka ndani ya nyumba yake na kukimbia mbio hadi stendi ya basi ambako alipanda daladala lililomchukua moja kwa moja hadi katikati ya jiji la Dar es Salaam ikiwa tayari ni saa tano na nusu mchana, hakutaka kwenda mahali kokote zaidi ya stesheni ya treni na kukata tiketi ya daraja la tatu.
“Nitakwenda hivyo hivyo kwa taabu ili mradi nimpate huyo mganga!” Aliwaza baada ya kukata tiketi yake.
Alibaki stesheni hadi saa 11 jioni muda wa kuingia katika mabehewa ulipofika na saa kumi na mbili treni ya abiria kwenda Kigoma na Mwanza iliondoka Nancy akiwa mmoja wa abiria. Moyoni alijawa na huzuni isiyo na kipimo, maisha yake yalikuwa yamecheza tikitaka na kujikuta akiwa kichwa chini miguu juu, furaha yote aliyowahi kuwa nayo ilikuwa imepotea na aliamini yote hayo yalisababishwa na Tonny! Alimchukia mwanaume huyo kuliko kitu kingine chochote.
“Sitamsahau Tonny! Na sitampenda mwanaume na kama ikitokea nikafanya tendo la ndoa na Danny, nitakuwa nimefanya kwa sababu nataka kumsaidia baba yangu! Vinginevyo nisingediriki kufanya hivyo!” Aliwaza Nancy wakati treni ikizidi kukata mbuga kuelekea Morogoro, hakulala usiku mzima akiwaza na wakati mwingine alilia machozi, mawazo juu ya baba yake aliyekuwa akiteseka mahabusu hayakumwacha.
Kulipokucha asubuhi walikuwa Dodoma, kulikuwa bado kilometa nyingi sana mbele yake kabla ya kufika Tabora, alitamani kupaa na kufika Tabora dakika hiyo hiyo.
Kutwa nzima alikuwa ndani ya treni akisafiri bila kula wala kunywa chochote! Mdomo wake ulikuwa mchungu kupita kiasi, hakutamani kula chochote alichohitaji wakati huo ni kukutana na mganga tu basi hakuna kingine hapo ndipo angeweza kula chakula kwa furaha.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kusafiri kwa usafiri huo na hata kuwa nje ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani! Ilikuwa ni safari iliyompeleka mbali na alikokulia, mahali asikomfahamu mtu yeyote, bila wazazi wake kuelewa kwamba alikuwa amesafiri! Kwake huo ulikuwa ni uamuzi mkubwa kupita kiasi.
*****
Saa tatu usiku treni liliingia Tabora na watu kuanza kuteremka, tangu Dar es Salaam hadi anashuka behewani alikuwa bado hajafungua mdomo wake kuongea na mtu! Lakini alipokanyaga ardhi ya Tabora alilazimika kuuliza kwani hakuelewa hata hicho kijiji cha Kisanga kilikuwa umbali gani kutoka mjini Tabora.
“Dada habari yako?” Alimwita dada mmoja aliyekuwa akipita mbele yake huku akiwa na begi mkononi pamoja na mtoto mdogo mgongoni, alimwamini mama huyo kwa namna alivyoonekana! Tabora ilitisha kwa vibaka katika kipindi hicho, asingeweza kumuuliza mtu yeyote aliyemwona.
“Nzuri tu!”
“Naomba nikuulize!”
“Uliza tu!”
“Unakifahamu kijiji cha Kisanga?”
“Ndiyo ninakokwenda!”
“Kweli?”
“Kwanini unauliza kwa mshangao?”
“Kweli Mungu ni mkubwa! Hata mimi nakwenda huko huko na ni mgeni kabisa, hata hapa Tabora ni mara ya kwanza kufika!”
“Unakwenda kwa nani Kisanga?”
“Mzee Mwinyimkuu!”
“Mwinyimkuu gani?”
“Ni mganga wa kienyeji!”
“Ahaa! Huyo namfahamu!”
Moyo wa Nancy ulijaa furaha isiyo kifani, bila kutegemea alijikuta akishangilia na kumfanya mwanamke aliyekuwa mbele yake ashangae na kutaka kufahamu ni kwanini alifurahia kiasi hicho.
“Ni babu yangu sijamwona muda mrefu sana, nilikuwa nje ya nchi nikisoma na niliporudi nikakuta alihamia Kisanga!”
“Wewe ni mwenyeji wa Bagamoyo? Maana nasikia huko ndiko alitokea”
“Ndiyo!”
“Basi umefika!”
Nancy hakuwa tayari kuyaamini masikio yake kutokana na kauli alizozipata kutoka kwa mwanamke aliyekuwa mbele yake, hakutegemea kama ingekuwa rahisi kiasi hicho kumpata mzee Mwinyimkuu na hapohapo alianza kumshawishi mwanamke huyo waondoke mara moja kwenda Kisanga.
“Kisanga saa hizi?”
“Ndiyo!”
“Hakuna magari mpaka kesho!”
“Kwani hakuna gari la kukodi?”
“Kama pesa unazo litapatikana!”
“Unafikiri inaweza kuwa shilingi ngapi?”
“Sielewi labda twende stendi tukaulize!”
“Nafurahi sana kukutana na wewe dada! Umekuwa msaada mkubwa sana kwangu!” Alisema Nancy wakati wakiingia kwenye teksi.
“Dereva unapafahamu Kisanga?”
“Ndiyo!”
“Tunaweza kupata gari la kutupeleka huko?”
“Kama pesa ipo hata mimi naweza!”
“Shilingi ngapi?”
“Ipo sitini elfu?”
“Nikikupa hamsini huendi?”
“Poa!”
“Basi nyoosha moja kwa moja!”
Mambo yalizidi kumshangaza Nancy kwa jinsi yalivyokuwa yakienda bila mkwamo wa aina yoyote, alipata picha kuwa alikokuwa akielekea pia yangekwenda hivyo hivyo na ikiwa mganga angefanya kazi ya kumwondolea yamini usiku huo basi siku iliyofuata angerejea Tabora na kupanda tena treni au basi kurejea Dar es Salaam, hiyo ndiyo mipango iliyoendelea kichwani mwake wakati gari likipita katika mabonde kuelekea Sikonge.
Waliingia wilayani Sikonge saa saba usiku, Nancy akiwa amechoka taabani sababu ya ubovu wa barabara na safari ya siku mbili, hawakutaka kusimama walinyoosha moja kwa moja wakipita katika barabara mbovu katikati ya mashamba ya watu.
“Mh! Huku mbunge wenu nani?”
“Ah! bwana wee, sisi tulishajizoelea, nyie watu wa mjini ndio mnateseka!”
“Kwa kweli mna shida!”
“Lakini tumekaribia, kutoka hapa hadi Kisanga ni kama kilometa mbili!”
“Afadhali!”
Nusu saa baadaye sababu ya ubovu wa barabara waliingia kijijini Kisanga, kila sehemu ilikuwa giza na nyumba zilionekana kwa taabu sana chini ya miembe mikubwa! Haikuwa rahisi kwa Nancy aliyezaliwa na kukulia mjini kuamini kuwa binadamu waliishi eneo hilo. Palionekana porini zaidi kuliko makazi ya watu.
“Twende kwanza nikupeleke wewe, ndio mimi nitakwenda nyumbani!”
“Nashukuru sana kwa kipaumbele ulichonipa!” Nancy aliongea.
Alikuwa amefurahi mno kufika kijijini Kisanga na hatimaye angekutana na mzee Mwinyimkuu mkombozi wa maisha yake kwa wakati huo, alipomuuliza mwanamke aliyekuwa naye ndani ya gari ambaye tayari alishamfahamu kwa jina la Mariam juu ya ni lini alimwona mzee Mwinyimkuu kwa mara ya mwisho.
“Miezi miwili iliyopita kabla sijaondoka kwenda Morogoro alikuwepo!”
“Kwa hiyo bado yupo?”
“Lazima, atakwenda wapi? Dereva simama hapo!” Mariam alimwamuru dereva wa gari na akakanyaga breki na kuegesha pembeni.
“Nancy umefika twende nikusindikize!” Aliongea mwanamke huyo wakishuka garini, giza lilikuwa kila upande! Nancy alizidi kutishika.
Begi lake likiwa mkononi walianza kutembea pamoja wakielekea bondeni, mwendo wao ulikuwa wa taratibu sababu hawakuwa na tochi! Ghafla Mariam alisimama.
“Mh!” Aliguna.
“Vipi?”
“Mbona pako hivi?”
“Pakoje?”
“Hapa ndio nyumbani kwa mzee Mwinyimkuu lakini pananishangaza, sikupaacha hivi!”
Ingawa ilikuwa katikati ya usiku, pamoja na giza kutanda kila upande, bado Nancy na Mariam walikuwa na uwezo wa kuona nyumba zote zikiwa zimeteketezwa kwa moto! Mariam alishika mikono kichwani mwake, akiwa haelewi nini kilitokea wakati akiwa hayupo! Aliogopa kuonekana mwongo na kuwa amemsumbua Nancy kumtoa mjini Tabora hadi Kijijini Kisanga bila sababu yoyote.
“Hakyanani kabisa dada, mzee Mwinyimkuu alikuwa hapa sijui kitu gani kimetokea wakati mimi nikiwa Morogoro!” Aliongea mwanamke huyo akiwa na mtoto wake mgongoni.
Nancy alikuwa kimya, mwili wake wote ukitetemeka, furaha yote aliyokuwa nayo iliyeyuka akagundua safari ya kumtafuta mzee Mwinyimkuu ilikuwa haijafika mwisho na hakufahamu angeimaliza lini na vipi! Ilikuwa ni lazima aendelee kumtafuta mganga huyo hadi ampate na kumwondolea Yamini aliyomwekea mwilini mwake.
“Laiti ningejua nisingefanya kitendo hiki, nilimwamini mwanaume ambaye baadaye alikuja kunisaliti! Mapenzi, mapenzi ni kitu kibaya sana!” Aliongea kwa sauti Nancy.
“Kwani kuna nini mdogo wangu?” Mariam aliuliza Nancy akiwa amekaa chini akilia, alikuwa akimfikiria mama yake na baba yake aliyekuwa mahabusu kwa kosa la kumpiga risasi Danny!
Maisha yalikuwa yamemgeuka, kila kitu kilionekana kuwa adui yake, alishindwa kuelewa ni kwanini alikuwa katika hali hiyo, imani yake kwa Mungu ilianza kupungua! Isingewezekana kama kweli Mungu angekuwepo amwache yeye ateseke kiasi hicho.
“Kwani kuna nini mdogo wangu? Unaumwa? Bahati mbaya hujanieleza nini tatizo lako, hivi kweli huyu mzee ni babu yako tu au kuna kitu kingine?” Mariam aliuliza maswali mfululizo baada ya kuona Nancy hajajibu swali lake la mwanzo na kuendelea kulia.
Picha hiyo ilimwonyesha Mariam wazi kwamba kulikuwa na tatizo katika akili ya Nancy na si tatizo dogo pengine yeye angekuwa wa msaada kwake katika kipindi hicho ukizingatia Nancy hakuwa na ndugu yeyote Kijijini Kisanga.
“Sio babu yangu!” Nancy aliamua kueleza ukweli.
“Sasa tatizo ni nini? Na kwanini unamtafuta?”
“Niliwahi kufanya makosa Fulani katika maisha yangu!”
“Makosa gani?”
Badala ya kujibu Nancy aliangua kilio tena, ikabidi Mariam akae naye kwenye nyasi na kuanza kumbembeleza ili aeleze ukweli, kwikwi ya kulia ilipomwachia Nancy alijikaza akafungua mdomo wake na kuanza kueleza kilichotokea, Mariam alisikitika kupita kiasi.
“Sikulaumu Nancy! Hata mimi ningeweza kufanya hivyo, ni wazi ulimpenda sana Tonny lakini alikusaliti, Mungu anajua jinsi ya kukufariji! Furaha yako inakusubiri mbele, hata hivyo nisingekushauri ufanye tendo la ndoa na mwanaume mwingine kabla hujampata mzee Mwinyimkuu, ni hatari! Haya mambo si ya kufanyia mchezo, rafiki yangu mmoja naye alifanya mchezo huu huu, sikutishi hivi ninavyoongea na wewe ni marehemu, yeye na mwanaume waliyetembea naye waling’ang’aniana hadi kifo!” Mariam aliongea na kuzidi kumtia hofu Nancy.
“Sasa nifanye nini dada? Nitampata wapi huyu mzee ili aniondolee hii balaa mwilini mwangu? Haya ni mateso na si mshauri mwanamke mwingine afanye kitendo hiki! Hata kama anampenda mwanaume kiasi gani!”
“Twende nyumbani tukalale, kesho tukiamka tutaulizia vizuri hapa kijijini nini kilitokea nyumbani kwa mzee Mwinyimkuu, si ajabu yupo hapahapa kijijini lakini amehamia sehemu nyingine!” Aliongea Mariam na kumpa matumaini Nancy, moyoni aliamini lazima mzee Mwinyimkuu alikuwa sehemu fulani kijijini na siku iliyofuata wangempata.
Je nini kitaendelea?
Je Nancy na Mariamu wataweza kumpata Mwinyimkuu?