ILIPOISHIA
“Pole sana mama mwili wa mumeo upo katika chumba cha …..? Kabla ya kumaliza kusema mama Julieth alianguka chini na kupoteza fahamu. Haraka wale askari walimbeba Mama Julieth na kumwingiza katika chumba maalumu ambako alipata huduma na kupata fahamu baada ya saa 3. Kisha daktari aliwaomba wale askari kumsindikiza mama Julieth nyumbani kwake.
INAPOENDELEA
Majirani zake mama Julieth walikwisha kusanyika nyumbani huku mmoja wao akienda shuleni kuwafuata watoto. Baada ya kufika mama Julieth vilio na kelele za kila aina vilitawala huku mama Julieth akianguka chini nakukosa nguvu kabisa. Mipango ya mazishi ilifanyika na kuamua kuzika siku iliyofuata. Siku ya mazishi watu walijaa sana huku simanzi na masikitiko vikitawala katika eneo lote la Kaloleni kwani Mzee Magesa alikuwa maarufu sana.
Mwili wa Mzee Magesa ulizikwa kwa taratibu zote huku viongozi wa dini na serikali kutoka Kaloleni wakihudhuria na kutoa nasaha zao. Huo ndio ulikuwa mwisho wa maisha ya Mzee Magesa ‘Muuza mboga’ sokoni. Wiki mbili baada ya mazishi Mama Julieth alikuwa bado hajapata nguvu za kuanza kufanya chochote. Siku moja alikuwa amekaa katika ngazi amejiinamia kama mtu ambaye amekata tamaa ya maisha, akiendelea kulia kwa uchungu. Julieth alitoka ndani akiwa ameshika kikombe cha chai na kumpa mama yake huku akimfariji.
“Mama usilie, sisi tupo na wewe Mungu atatusaidia.” Julieth alimfariji mama yake huku akimpa chai. “Mwanangu baba yenu alikuwa nguzo ya familia na sasa hayupo tena. Kumbuka mnatakiwa msome nani atawasomesha? Hivi ni kwa nini Mungu amemchukua mapema hivi?” Alijibu mama Julieth huku akibubujikwa na machozi. “Mama tusikate tamaa hata baba kabla hajafariki alisema tuwe na mshikamano na upendo katika familia yetu. Mama mimi nitakuwa nawe bega kwa bega kukusaidia.” Julieth aliendelea kumfariji mama yake.
Mama Julieth alimwangalia Julieth kwa macho ya matumaini kisha akamkumbatia mwanawe. “Sawa mwanangu kwani yote haya ni mapenzi ya Mungu.” Alijibu mama Julieth na kuanza kunywa chai. Basi Julieth aliendelea na kazi za ndani na kumwacha mama yake akiwa amepumzika.
******************************************************
Baada ya mwaka mmoja kupita tangu Mzee Magesa afariki mama Julieth aliugua ugonjwa wa moyo, kwa hiyo akashindwa kuendelea kufanya kazi zake za kila siku na hata biashara ya sokoni aliyokuwa akiifanya baba Julieth hakukuwa na mtu wa kuwasaidia kuiendeleza. Hali ya kipato ilizidi kuwa ngumu kutokana na kuugua kwa mama Julieth kwani hata kazi ya kupika chapati hakuweza kuendelea nayo tena. Kutokana na hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu Julieth aliamua kuacha shule akiwa Darasa la Sita ili kumsaidia mama yake kazi za pale nyumbani na ikiwa ni pamoja na kuuza chapati.
Julieth alianza kuuza chapati biashara ambayo haikuwapa kipato kikubwa kuweza kujikimu kutokana na wateja kuwa wachache. Kutokana na maisha kuwa magumu walilazimika kula mlo mmoja kwa siku ili kukusanya kodi ya vyumba viwili walivyokuwa wanaishi. Julieth aliendelea kuvumilia bila kukata tamaa kwani mbali na kuwa ni binti mdogo lakini alikuwa na majukumu makubwa ya kutunza familia. Katika kuuza chapati Julieth alikutana na watu mbalimbali waliozipenda sana chapati alizokuwa akipika. Siku moja asubuhi alikuja kaka mmoja kununua chapati akatokea kumpenda sana Julieth.
“Habari yako mrembo!” Yule kijana alimsalimia Julieth huku akitabasabu. “Nzuri kaka karibu.” Alijibu Julieth huku akimwangalia usoni. “Mimi naitwa John sijui mwenzangu unaitwa nani?”Alijitambulisha yule kijana. Julieth alisita kidogo halafu akajibu; “Naitwa Julieth karibu kaka chapati shilingi mia moja na hamsini nikupe chapati ngapi?” Alijibu Julieth. “Naomba chapati mbili.” Alitamka John huku akimpa noti ya shilingi elfu kumi.
“Mmh jamani huna hela ndogo kaka au kuna kitu kingine unataka kununua dukani nikakuchukulie, asubuhi hii chenchi zinasumbua kweli.” Alisema Julieth kwa kulalamika.
“Usijali Julieth nipe hizo chapati na fedha inayobaki ni zawadi yako.” Alijibu John. “Mh we kaka, hela yote hii nibaki nayo kuna usalama kweli? Hapana kaka ngoja nikutafutie tu chenchi.” Alisema Julieth huku akinyanyuka kwenda dukani. USIKOSE SURA YA .....4.....