*SEHEMU YA KWANZA*
★★★★★★★★★★★★★★★★★
“Nashindwa kuelewa kwa nini nakupenda kiasi hiki Jay, nahisi kuchanganyikiwa juu ya penzi lako my” Jacqueline alisema maneno haya huku akiwa amelalia kifua changu. Tulikua katika chumba changu kidogo nilichopangisha uswahilini. Kutokana na kazi yangu ya kuuza karanga, sikuweza kumudu kupangisha katika vyumba vyenye thamani nzuri. Niliishi kwa kuungaunga.
“Mimi nadhani upendo wangu unaotoka moyoni ndio unaokufanya uzidi kunipenda kila leo, sidhani kama kuna jingine”. Nilimjibu huku nikijifanya kama sijui niyafanyayo.
“Na kweli, maana huwezi kuamini sijawahi kulala nje ya nyumbani tangu napata fahamu hadi leo, lakini tazama hii ni siku ya tatu sasa nipo hapa kwako halafu sihisi kujuta hata kidogo”. Alizidi 'kuropoka' Jacq na kunifanya nijihisi wa kipekee sana.
“Penye mapenzi ya dhati majuto wala usiyakaribishe kamwe my” Nilikazia ili kuendelea kumpa moyo Jacq ahisi niko pamoja naye kwa kila hali.
★★★★★★★★★★★★★
Jina langu naitwa Jumanne, ingawa najulikana zaidi kama 'Jay'. Nimezaliwa mkoani Tanga miaka 22 iliyopita. Kutokana na utundu pamoja na ukorofi niliokuwa nao sikubahatika kuendelea na elimu yangu ya sekondari baada ya kufika kidato cha pili. Niliona shule inanichelewesha nikaamua kuingia mtaani kutafuta maisha.
Maisha yalikua magumu sana mtaani. Nilihangaika sana hadi pale nilipoamua kujikita katika biashara ya kuuza karanga ambayo kiasi fulani ilikua ikiniingizia walau pesa kidogo za kuendeshea maisha ya kila siku.
Nilianza biashara hii nikiwa bado na umri mdogo wa miaka 17 tu, na sasa ni miaka mitano naendelea na biashara yangu nikiwa nimejizolea umaarufu sehemu mbalimbali za jiji hili la wastaarabu.
Kutokana na pirika za maisha na jinsi hali yangu ilivyo duni miaka yote hii ambayo nauza karanga, nilijikuta napitia kipindi kigumu sana katika habari za mahusiano. Nguo zangu chakavu pamoja na haiba yangu isiyovutia vilinifanya nitengwe sana na wanawake karibu wote na kutotaka kabisa kuanzisha uhusiano na mimi licha ya kujaribu 'kurusha mshipi' kwa wanawake kadhaa mara kwa mara. Hapa ndipo nilipojihisi mnyonge sana na kuamua kutafuta njia mbadala itakayonifanya nipendeke mbele ya wanawake.
Hapa ndipo nilipotafuta hirizi ya mahaba ijulikanayo kwa jina maarufu la 'ndere'.
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Jacqueline alikuwa ni msichana aliyetokea kwenye familia yenye maisha ya kawaida sana, babaake akiwa mwajiriwa wa serikali na mamaake akijishughulisha na ujasiriamali. Sifa pekee aliyosifika nayo Jacqueline ni uzuri wake wa sura pamoja na umbo. Alikuwa mrefu mwenye umbo la wastani, lililojichonga kwa 'shape' nzuri ya kuvutia. Lipsi zake pana zilizidi kuushajihisha wajihi wake. Rangi yake ya maji ya kunde pamoja na ngozi yake ya kuvutia ilizidi kumpa 'marks' kwa amuangaliae.
Wanaume wengi wakware walishamtokea kumtongoza lakini kutokana na jinsi alivyokuwa anajichukulia, ilikua ngumu kumkamata.
Wengi wa wanaume waliishia kumnyooshea vidole tu huku yeye akijisikia furaha kila siku anavyozidi kuwakataa wanaume tofauti tofauti.
Kwa mara ya kwanza nilivyokutana nae wakati amejipumzisha katika moja ya bustani za jiji hili, huku mimi nikipita na kapu langu la karanga, moyo wangu ulishtuka sana. Hii ni kutokana na uzuri wake. Na kwakuwa kwa sasa nilishazoea kuwatokea wasichana wote warembo huku nikiwa na uhakika kuwa sikataliwi, ndipo nilipomfuata pale alipokuwa na kuamua kumuonjesha karanga. Nikabahatika kukaa nae kwa dakika chache kabla sijachukua namba yake ya simu na kuondoka.
★★★★★★★★★★★★★★★★
Nikiwa bado pale kitandani huku Jacq amelala kifuani kwangu, nilisikia simu yangu ndogo iliyokuwa katika meza ndogo iliyokuwa chumbani humo ikiita.
Nikapeleka mkono na kuikamata kwani meza haikuwa mbali na kitanda. Wakati naileta karibu niangalie nani anapiga ili nipokee, ikaniponyoka na kuanguka chini. Mpira niliokuwa nimeifunga kuishikilia isije kuachana na battery ukafunguka na kufanya battery itoke. Nikainuka pale kitandani na kuiokota kisha nikarudishia battery na ule mpira kisha nikaiwasha.
“Saa ngapi hapo?” Nilimuuliza Jacq ili niweze kurekebisha saa katika simu yangu. Jacq akaangalia saa yake ya mkononi aliyokuwa amevaa.
“Saa 4:30 baby..” Alinijibu na kubaki nimehamaki. Ni siku ya pili sasa nipo na Jacq na hata kwao hakumbuki. Na hii ilishakuwa usiku sana hawezi tena kurudi kwao usiku huu. Hii ilimaanisha kuwa nitalala nae na atatimiza siku ya tatu akiwa hapa kwangu.
Wakati narekebisha saa ya simu yangu, mlio wa 'sms' ukasikika katika simu yangu. Nikaamua kuisoma..
“Wewe kata tu simu, lakini huyo binti wa watu uliyenaye siku ya pili leo atasababisha karanga ukaziuzie jela” Ndivyo ilivyosomeka sms ile na kunifanya nimuangalie Jacq jinsi alivyojiachia pale kitandani huku nikishusha pumzi ndefu.
★★★★★★★★★★★★★★★★
Itaendelea....