Nakumbuka siku nilipomtaarifu baba na mama kuhusu kumuoa Angela Shiri. Ilikuwa siku ya mapumziko, siku ya juma pili tulivu, nilikuwa nimepumzika nyumbani na wazazi wangu. Ni baada ya kupata mlo wa mchana, vyombo vilikuwa angali mezani. Nilikuwa na tizamana na wazazi wangu wawili katika meza ya chakula. Baba akiwa kushoto mwa mama, wakiendelea kunawa mikono. Niliwasubiri hadi walipomaliza kunawa, ndipo nami nikanawa. Sikupenda kupoteza muda, nililainisha koo langu kwa ajili ya kusema kile kilichokuwa akilini.
“Baba na mama, kumradhi. Nawaombeni kuzungumza….” Nilibwabwaja nikiwatizama kwa zamu, ambapo nilianza na baba kisha nikapeleka jicho kwa mama.
“Sema usijali, mwanangu” Ilikuwa sauti ya baba ikionekana kuchangamka si kidogo, baba akahamisha macho usoni mwangu akamgeukia mama, “Au unasemaje mama Bakari?”
“Hataa, kauli yako tosha ni jibu zuri katika familia. Hatuwezi kumnyima mtoto wetu kuongea na wazazi wake, tueleze baba” Mama nae alitii sheria.
“Eeh, Baba na mama. Naona sasa mtoto wenu nimefikia wakati wakuoa. Nimepata mchumba, isipokuwa mchumba niliyempata…” Nilikatishwa na sauti ya furaha ya mama.
“Loo!! hongera sana mwanangu. He! He heee!! Aiy!aiy!. Nimeshakuza dume langu la pekee” Mama alitokwa na maneno kwa furaha, akanishika mkono, pia aliona haitoshe kumalizia furaha yake kwa kunishika mkono, aliinuka na kuruka ruka huku akipiga vigelegele. Baba alibaki akitabasamu pana lililoshiba midomoni mwake.
“Hongera sana mwenetu, kufikia hatua hiyo ambayo ni hatua kubwa sana katika maisha ya mwanadamu, hata mimi nilitaka nikukumbushe kuhusu jambo hilo kwani ni miaka thelethini sasa, umri umekwenda sana isitoshe magonjwa yamezagaa sana si sawa na enzi zetu tukiwa vijana kama rika lenu…..nakupa pongezi sana mwanangu…pia nasema hakuna kazi nzito kama kuchagua mchumba, kwa haraka haraka unaweza kudhania kwamba ni kazi ndogo lakini sivyo mwanangu” Baba alijaribu kunipongeza huku akinishauri mawili matatu.
“Nashukuru sana baba, hata mimi naelewa kumpata mchumba yataka muda na umakini zaidi, hata huyo nitakaye waletea naamini mtampenda kwani ana kila sifa ambazo mwanamke hutakiwa kuwanazo, kuanzia tabia, sura hata umbo….”
“Tutashukuru kama ndivyo, hakuna ulazima kwamba mkeo awe mzuri sana, hapana. Tunachotaka ni nidhamu, uvumilivu, mwenye upendo kwako na wazazi na mcha mungu”
“Baba huyo anasifa zote….” Niliwatoa wasiwasi akilini mwao.
“Ehee! Mchumba wako ni kabila gani?” Mama aliniuliza swali baada ya kuvuta kiti karibu, huku akijifunika ushungi wake.
“Ni mtu wa Kilimanjaro……..” nilijibu kiujanja, sikutaka kutaja kabila lake.
“Ndio, ni mtu wa kilimanjaro lakini unaelewa Kilimanjaro kuna makabila mengi, wapo wachaga, wapare na makabila mengineyo ya wageni, sasa mchumba wako ni kabila gani?” Mama alizidi kunidadisi
“Ni kabila lako, mama” Nilimjibu nikitabasamu.
“Du!! Hapo sikushauri lolote mwanangu, kabila letu ni wanawake wakorofi sana. Tuna ule ubabe wa kuwakalia waume zetu” Nilitamani kumwuliza mama inamaana naye anamletea baba ukorofi lakini nikajua swali lile nitakuwa nimemkosea mama heshima. Nikatulia nikimsikiliza kwa makini, ingawa sasa mapigo ya moyo yaliongeza kasi kidogo. Tayari nilishaanza kuingiwa na hofu ya kumkosa Angela katika maisha yangu. Katika akili yangu, nilifikiri swali lingine la kumwuliza mama, mwanamke mzuri si kabila lake ama mwanamke mbaya si kusoma kabila lake, yawezekana kabila lake likawa lenye sifa hizo lakini binti yule akawa si mkorofi, mtu ni utu wala si kabila. Sasa wakati huo nikaamua kuyamezea akilini maswali hayo, hata kama ni wewe usingethubutu kubishana ovyo na wazazi wako.
“Sema mwenyewe kama kibuyu cha mganga, kumbe mnajijua eeee!” sauti nzito ya baba ilipata mwanya wa kukoroma.
“Lakini si wote, mbona miye naishi na baba yako vizuri. Hatujawahi kufarakana?.
Tunapendana kama kumbikumbi, bibi mbele bwana nyumba, lakini mchumba wako
anaonyesha upendo wa dhati kwako?. Ama ni muungwana wa sura na macho?”
“Hapana, ananipenda sana na ananijali” nilizidi kuwatoa hofu ili wasiweze kutoa pingamizi lolote juu ya mchumba wangu.
“Tunaweza kujua jina lake?” baba aliniuliza akinitizama kwa makini zaidi.
“Ndio, anaitwa Angela Shiri”
“Sawa, sawa …….. eee! Mama Bakari naomba unipishe kidogo kuna jambo nataka kumuelimisha mwanangu, Bakari, si vema ukawepo kikao hiki ila baada ya muda nitakuita, kaendelee kuandaa chakula cha jioni”
“Sawa mume wangu” mama aliinuka kinyonge akijongea jikoni, akaniacha mimi na baba sebuleni.
“Ni hivi mwanangu……” alianza kuongea kwa sauti ya chini kama vile ananinong’oneza jambo Fulani la siri.
“Najua wewe ni mtu mzima mpaka sasa, sivyo?”
“Ndivyo”
“Sawa sawa…eee!, wewe ni mwanangu pekee, sina mtoto mwingine yeyote zaidi yako, hivyo basi napaswa kukuelimisha chochote juu ya ndoa kwani wewe ndio kwanza unataka kuelekea huko. Naomba ufahamu kuoa si jambo la mzaha kama udhaniavyo. Kuishi na mwanamke ni kazi ngumu sana, moja unapaswa uwe na subira, pili uwe mvumilivu si kidogo, tatu umpende mkeo kuliko wanawake wote duniani, sina maana umpende mpaka akukalie, hapana. Mpende mkeo kama mkeo, usitokeo ovyoo nje magonjwa mengi sana sasa hivi hasa UKIMWI, naomba unielewe vizuri……. Wewe ni mwanangu na mwanangu ni rafiki yangu mkubwa, najua nikifa wewe ndiye utakuwa muhusika mkuu katika mazishi yangu, hivyo basi napaswa nikueleze bayana . Nikikuficha utasema kwanini baba hakunielimisha juu ya jambo hili, sitaki mwanangu ukaingia kwenye majuto, mimi naishi na mama yako lakini ni mvumilivu sana angekuwa mwanaume mwingine hata wewe usingefikia hatua ya kuoa, pengine ungekuwa mtoto wa mtaani. Ninachokueleza kabila hilo unalotaka kuoa halikufai kabisaa, utateseka sana mwanangu na isitoshe dini zenu hazichangamani, wewe Muislam yeye Mkristo, lakini swala la dini halina uzito kama anakupenda anaweza kubadili dini. Pia ninataka ufahamu kuwa uchumba si sawa na ndoa, si kwamba nataka kuingilia kati mapenzi yako na umpendaye…hapana ….nataka uoe chaguo lako ili hata baadae usije ukatulaani, ukajuta ukisema kama si baba na mama nisingeteseka na ndoa hii, tunataka uchague mwanamke umpendaye na akupendaye, asiye na tamaa, awe mvumilivu, zama za kutafutiwa mchumba zimepitwa na wakati isipokuwa sisi tutachunguza tukiwa kama washauri wako kuhusu mke unayetaka kumuoa, au kuna baya nililokueleza mwanangu?. Sema usinifiche hizi ni zama za ukweli na uwazi” Yalikuwa maneno mazito ambayo yaliniingia akilini angali ya moto.
“Hapana, isipokuwa kuna jambo ambalo linanitatiza sana kuhusu mchumba wangu”
“Jambo gani?”Akaniuliza baba ambaye sasa alisogeza kiti jirani kabisa, ili nimweleze kinagaubaga.
“Mchumba wangu alinieleza kama sitomuoa basi ataweza kujiua akiwa ameacha ujumbe sababu ya kujiua na kuhusu swala la kubadili dini hataki anasema mimi ndiye nibadili maana baba yake wa kambo ni mchungaji…”Baba alinikatiza maneno, Nikasikia sauti kali ya ukemi ikiniingia masikioni.
“Anataka ubadili dini?!”
“Ndio”
“Pamoja na elimu yako unaweza kubadilishwa dini na mwanamke?. Elewa kwamba huo ni utangulizi wa utumwa wa mapenzi, kubadili dini ni maamuzi yako lakini si kwasababu unataka kuoa mke hata kama ni mzuri kiasi gani, najua mwanangu unakimbilia wanawake weupe, weupe wa nini bwana ambao unapatikana madukani!! Yeye mtoto wa mchungaji nawe mtoto wa Shekhe Maliki”.Sasa sauti aliipoza kidogo tofauti na mwanzoni akiongea utadhania ananikaripia.
“Kwa kukurahisishia mwanamke hana dini hivyo lazima abadili yeye, pia kama ndilo kabila la mama yako nina imani utateseka ……..”
“Kivipi baba, mimi nimeshampenda naye ananipenda” nililalamika kidhaifu kabisa nikihisi baba anaingilia mapenzi yangu na Angela. Pia miye moyo ulikunja ngumi kwa maneno ya wazazi wangu, niliamini nitawapinga kila hali ilimradi Angela awe mwanamke wa ndoa yangu. Nilimuona baba akikunja uso na kunitizama kwa ghadhabu, sasa nikaamini alikerwa na swali langu.
“Ngoja nikushauri mwanangu……” alianza kusema kwa upole tofauti na nilivyodhania mwanzoni, baada ya kuona makunyanzi yametawala pajini mwa uso.
“Ndio, nishauri baba” nikajikuta nami nikimwitiki, macho na masikio nikiwa nimeyafungua kuona na kusikia chochote asemacho baba.
“Kabla ya yote, maana naelewa kama unatafuta mchumba basi kwa vyovyote ulichagua mmoja kati ya wale marafiki zako, ambao uliwachunguza ndipo ukampata huyo Angela, hivyo basi naomba urudi nyuma katika wale marafiki zako ulipompatia huyo mchumba Angela, uchague mchumba mwingine…..tena hakikisha unamchunguza vizuri tabia zake, malezi aliyolelewa utotoni mwake, kabila lake na hata dini ikiwezekana ili usiweze kupata shida ya kubadilishana dini, ambapo baadaye ikawa umejiingiza kwenye majuto……”Akatulia na kuokota glasi yenye maji na kuigugumia kinywani kisha akaendelea.
“Nisikilize vizuri Bakari….” Akili yangu iliingiwa na ufinyu wa nidhamu nikajikuta nikimkatisha baba bila hata kutegemea.
“Baba, hilo litakuwa zoezi gumu kwangu, mke niliyeona ananifaa ndiye huyo huyo, siwezi kupoteza muda tena. Kama nyie mnanipangia mke wa kuoa mtakuwa mnajisumbua bure, mi’sitaki. Ushauri wenu haunifai kabisaa!, Angela ndiye chaguo langu sina haja ya kuhangaika tena na isitoshe nimetoka naye mbali si kidogo” Kila nilipofikiri kumuacha Angela, nilishikwa na hasira sikujali naongea na baba au laa! Nilichotaka wasikilize kile ninachotaka.
“Hatuna nia ya kuingilia kati mapenzi yako, hatujui mmejuana lini na vipi, mmepeana nini hadi leo, ila tunajaribu kukuelimisha juu ya ndoa. Mwanangu hivi unajua nini maana ya ndoa?"
"Ndio Baba"
"Maana yake nini?" Alizidi kuniuliza Baba.
"Ndoa ni Ukamilifu wa makubaliano ya muungano wa mwanamke na mwanaume wanaopendana kuishi pamoja kuwa mke na mume kulingana na sheria ya dini, mila na desturi" Nilimjibu Baba akafurahia, japo alionekana kulazimisha furaha.
"Sawa, nasukuru kujua nini maana ya ndoa. Ndoa si kuoa na kuishi na mwanamke ndani ilimradii umetamka mbele ya mashahidi kwamba unampenda fulani, naomba uelewe mapenzi siri ya mtu, kumpenda mtu si kwa maneno, ‘Ooo!! Nakupenda sana Bakari’, anaweza akakwambia hivyo na badae anamwambia sijui Hamisi, John na wengineo, maneno hayo hayo. Mwanangu naomba usiuseme moyo wa mwenzako, hujui anafikiri nini akilini mwake, hujui anakupendea kitu gani, kumtambua kama mtu anakupenda ni jambo zito sana na ingekuwa rahisi endapo moyo wa mtu ungekuwa unafaa kutoa hadharani kama pesa mfukoni. Tafadhali mwanangu kama unaona tunania ya kuingilia kati mapenzi yako, tutakuacha uchague yupi bora Angela na wengineo lakini elewa kwamba sisi tunaona mbali….”
“Baba, naomba msinifikirie vibaya. Nimetokea kumpenda Angela na sina uhakika kama nitaweza kupumua endapo nitamkosa maishani mwangu. Najisikia mpweke sana, si kwamba nimewakosea heshima kama ni kulaumu naombeni muulaumu moyo wangu ambao umemuhifadhi Angela kwenye kiota cha huba, mfano wa mlima kilimanjaro unavyohifadhi theluji karne na karne” Nilizidi kulalamika, machozi yakinitoka bila kujijua. Nilijua kwa kufanya vile ingesaidia kidogo kama changa moto kwa Baba.
“Sawa, mkataa pema pabaya panamwita. Uko huru kuoa ama kuolewa, uko huru kubadili dini ama kutobadili. Hatukulazimishi bali tunakushauri kama wazazi wako. Mke bora si uzuri, naelewa umechanganyikiwa na weupe wa mchumba wako, tunakuachia utende………” baba alikatishwa maneno yake na ukemi.
Mama alichomoka jikoni baada ya kusikia maneno ya ukali.
“Heee! Baba Bakari mbona kelele tena. Kuna nini?” Mama akatokwa na maneno akiwa amesimama mlango wa kuingilia sebleni, yawezekana hofu ilishamuingia .
Kimya kilitawala, mama akatembea hatua za haraka huku kanga zikimdondoka bila kuzikwapua.
“Jamani, imekuwaje? Inamaana hayo ndio mazungumzo ya faragha?” sasa mama alimfuata baba na kuketi kiti cha jirani kabisa. Baba akawa ameinamisha kichwa kwa uchungu.
“Baba Bakari, mwanao anasemaje?” kimya kilitawala, ingawa safari hii baba alitikisa kichwa kwa masikitiko. Miye nilitulia kama maji ya mtungi. “Sema basi baba Bakari……” alipoona baba anachelewa kusema, akanigeukia
“Wee Bakari umemfanya nini baba yako?” Mama akaniuliza kwa ukali, nikakata shauri kumueleza.
“Baba amekasirika kutokana na kumpinga mawazo yake”
“Yapi?”
“Ya kuachana na binti ambaye ni chaguo langu”.
“Lazima uwasikilize wazazi wako, wazazi wanajua mengi”
“Ndio, lakini siweze kusikiliza jambo ambalo najua fika haliniingiii akilini. Naona niwaeleze bayana kuhusu kutokuachana na mchumba wangu….. nasema nyie ni wazazi wangu lakini hamna majukumu yeyote juu ya maswala ya mahusiano, niliwaeleza tu ili mfahamu mtoto wenu nimefikia hatua ya kuoa. Kumbukeni nina matilaba ya kumchagua nimpendaye…” niliongea kwa jeuri kama askari jela kwenye kutoa adhabu kwa mfungwa mkorofi.
“Pamoja na hayo, wewe ni mtoto tu bado. Ndio kwanza unaanza maisha, hujui hili wala lile, najua wanakupenda kwa sasa kwa vile huna shida, unawapa pesa za kutosha lakini ukumbuke maisha ni safari ndefu. Pia maisha hubadilika kama upepo, mara kusini, kaskazini na hata magharibi. Ipo siku watakukimbia utabaki peke yako kama maiti inavyobaki peke yake kaburini, hutakuwa na mshauri, msaidizi. Mwanangu usibwatuke ovyo kwa sababu una pesa ama kwa vile unafanya kazi Benki….” Yalikuwa maneno ya mama ambayo aliyatoa huku akibubukikwa na machozi. Hakika niliingiwa na uchungu sana, bila kutarajia machozi yakanitoka. Moyo ukajikuta ukinilaumu kwamba nilishawakosea heshima wazazi wangu. Taratibu niliinuka kitini na kumfuata mama.
“Mama naombeni msamaha, naomba mnisamehe nimewakosea heshima” niliposema maneno yale, nikatembea kwa magoti hadi kiti alipoketi baba. Nilijua wazi nimewakera na kuwakosea heshima wazazi wangu walioshirikiana kunilea na kunisomesha hadi nilipopata kazi benki, nikiwa meneja Msaidizi. Walihisi niliwajibu vibaya kutokana na pesa nilizokuwa nazo ingawa si kweli, nilimpenda sana Angela zaidi ya wanawake wote ambao nilishawahi kukutana nao.Nilikaa kimya kifupi nikagundua kwamba niliwakosea sana wazazi, ndipo nikajikuta nikitokwa na maneno ya huzuni.
“Baba nisamehe mwanao, sikutarajia kwamba ningewakosea heshima” Baba hakujibu alikaa kimya, nikajua kimya kile kilikuwa cha hasira.
“Baba naomba unisamehe, sitorudia tena” Nilimkaribia kabisa na kumshika mkono wake wa kuume angali nimepiga magoti.
“Tutakusamehe endapo utakubali kuachana na huyo Angela wako. Tunajua umechukizwa na mawazo yetu, ndio maana ukabwatuka maneno ya ajabu sababu ni Angela, usipoangalia mwenetu kwa hali hiyo unaweza ukapata shida katika ndoa yako, tunakuomba tena tupo chini ya nyayo zaka. Tuliza akili wanaotaka uwaoe wapo wengi sana, isipokuwa wanachotaka ni pesa zako. Siku hizi wanakausemi kasemao, ‘Hapendwi mtu, yapendwa pesa’. Hao wanataka kuja kukuibia kisha waondoke zao, na mwizi hana alama wanajua unafanya kazi benki, ndio maana hawaachi kukupigia simu na kukutumia ujumbe kwenye simu. Sasa kama hujui endelea…”
“Nimejua, nawaahidi nitamuacha Angela kisha nitatafuta mchumba mwingine”
“Hapo umenifurahisha mwanangu, nimekusamehe na nakuombea kwa Mungu upate mchumba haraka na awe mwaminifu”.
“Kuwa makini na mabinti wa sasa, ni wepesi kuleta matata wengi wao hawana upendo wa kweli. Isipokuwa wanajali pesa” Baba alipomaliza kuongea, mama nae akadakia kabla sijazungumza chochote.
“Hata mimi nimefurahishwa na tamko lako, nimekusamehe. Nakuombea kwa Mungu upate mke mwema atakaye kuzalia watoto” niliona muda mfupi wazazi walijawa na furaha tele moyoni. Nilisema maneno yale kwa ujasiri ingawa moyoni niliumia, sikutaka kamwe nitengane na Angela. Tulishazoeana siku zote tupo pamoja, si matambezini wala nyumbani kwangu.
Nilipomaliza mazungumzo na wazazi, niliondoka na gari yangu ndogo RAV4 ambayo nilitegemea kumpa Angela kama zawadi siku ya harusi yetu. Nilishapanga mambo mengi na Angela. Akili yangu iliingiwa na ganzi, sikuwa najijua niendako, nilichojua nipo kwenye gari langu. Ila nilijikuta nipo barabara ya Shekilango nikielekea barabara ya Morogoro.
Ghafla nikagutushwa na mlio wa simu. Nikashituka kidogo kama niliyetoka usingizini, nikajua sasa nipo barabara yenye msongamano wa magari. Nikawasha taa za kuegesha gari kando ya barabara, nilipaki gari langu eneo la Sinza madukani karibu na maegesho ya teksi. Sasa nikapokea simu.
“Hallo!, Bakari naongea hapa. Sijui wewe nani na nikusaidie nini, tafadhali!” nilijikuta nikiponyokwa na maneno huku nikiwa nimekunja uso. Sikukumbuka hata kutizama namba ya mpigaji.
“Inamaana hujui namba zangu, dear” Ilikuwa sauti murua na mororo mithili ya kinanda ikiingia maskioni mwangu huku ikitoa miremo ya huba. “Ooohph!” nilishusha pumzi kwa nguvu. Baada ya kugundua kwamba alikuwa Angela, sauti yake hainipotei kamwe hata nikiwa wapi. Kisha nikaendelea kuongea.
“Nazijua, naomba unipigie simu baadaye…. au usinipigie nitakupigia kwa wakati wangu”
“Hapana dear, kwanini unasema hivyo, ama upo na mwenzangu nini?”
“Hapana” Nilimjibu kwa ukali kidogo.
“Sasa mbona unaongea na mimi kwa hasira? Halafu unasema nisikupigie utanipigia kwa wakati wako?….sema kama ndio ushaanza kunisaliti hababi wangu..eeee!”
“Hapana, najisikia kuumwa na kuna jambo zito linanitatiza, upo wapi?” Hapo niliongea mithili ya mgonjwa tena sauti ya chini.
“Nipo kwenye daladala maeneo ya Shekilango hapa nakuja nyumbani kwako”
“No! no! shuka kituo cha Legho, nakuja hapo. Nipo maeneo ya Sinza Madukani, sawa”
“Sawa, lakini jambo gani linakutatiza”
“Nitakueleza nikija hapo, una haraka gani?”
“Nimeingiwa na hofu kubwa mwenzio, heri usingeniambia kwenye simu.Jambo lenyewe linafurahisha?”
“Kuna jambo lenye kutatiza likafurahisha?. Nisubiri sikawii”
“Sawa, dear” Nilikata simu na kuwasha gari kuelekea kituo cha Legho maeneo ya Shekilango. Nilikuwa naenda kuonana na Angela lakini sikujua pa kuanzia kumweleza, niliamini wazazi ni Mungu wa pili lazima niwasikilize. Pia nilizidi kufikiri, safari ya Angela kuja nyumbani kwangu ambapo huishi jirani na wazazi wangu, ilikuwa kuona gari lake nililomweleza nimemnunulia, na nilipanga kumkabidhi siku ya harusi yetu. Ghafla kiza cha mawazo kikarindima akilini,
“Hivi nikimweleza Angela itakuwaje? Ni kusema anaweza kufanya kila alichosema siku za nyuma, kwamba nisipo muoa atajinyonga ama kunywa sumu? Kama itakuwa hivyo, nitafanyaje kumnusuru Angela na mauti?. Hatujawahi kufarakana hata kidogo, leo natenganishwa mwanamke wa maisha yangu, kisa hoja zisizo na msingi za wazazi! Hapana …. Kwanini wazazi wananinyima uhuru? Ni kwa vile wamenizaa? Hata kama kwani wao walichaguliwa waoane na wazazi wao?…. ni kusema kama nitatengana na Angela nitapata zaidi yake?. Yawezekana, wazuri ni wengi lakini siwezi kuwalinganisha na Angela…Eee hee nimekumbuka maneno ya wazazi yanaweza kuwa na ukweli, Angela anaweza kuwa ananipenda niwe na gari la kifahari… lazima nimweleze kwamba sitobadili dini, najua hataki kubadili yeye kwa sababu ni mtoto wa mchungaji, sababu hiyo itanirahisishia kutengana nae” mawazo yalitawala ubongo wangu, bila kujijua nilijikuta nipo kwenye foleni ya magari, taa za shekilango. Nilipogutuka nikatamani kurudi nyuma lakini haikuwezekana, kulikwepo na magari zaidi ya matatu yakiwa nyuma yangu. Taa ziliporuhusu kuingia barabara ya Morogoro niliingia kushoto nikageuza kama vile naingia kituo cha mafuta ambacho kipo karibu na barabara ya Shekilango.
Nilipofika stendi ya Legho, nikaegesha gari langu. Kabla hata sijazima gari, niliguswa begani kisha nikageuka taratibu. Kabla ya kumuona mtu aliyenigusa, nilifumbwa macho kwa viganja, nikakumbwa na gharika la manukato murua yaliyolisha pua zangu hadi ziliposhiba. Manukato hayo hayakuwa tofauti na yale ya Angela.
“Angela! Angela najua ni wewe, dear” nilisema nikimpapasa vidole vyake ambavyo nilijua wazi kama angekuwa amevaa pete niliyomnunulia lazima ningemjua, pete yake ilikuwa kubwa ambayo ilifunika vidole vitatu, nikajua hakika alikuwa Angela.Pia viganja vyake laini na vyenye kuteleza vilinifanya nihisi ni Angela.
“Mmmh kumbe unanijua kiasi hiki!” Yalimtoka maneno akitoa viganja usoni mwangu.
“Ndio, kwasababu ya manukato yako, kucha zako, vidole vyako na pete ambayo niliishika wakati umenifumba macho, pia najua hakuna mtu atakayeweza kunifumba macho hali yakuwa hanijui” Nilimweleza nikijitahidi kuchangamka ingawa bado dalili za jakamoyo zilijitokeza.
Angela akaingia kwenye gari kupitia mlango wa kushoto kwangu, “Vipi dear wangu”
“Poa”
“Safari ya wapi?” aliniuliza
“Safari hii ilikuwa kwako, tena tungepishana kweli” nilijaribu kuongea kiuchangamfu ili asigundue kile kinachonifanya nitingwe na mawazo. Japo sura yangu ilipambwa na tabasamu lakulazimisha lakini bado nilionekana mwenye kila dalili kuchukizwa jambo fulani. Wakati huo huo, niliwaza jinsi ya kumueleza Angela yaliyonisibu.
“Imekuwa kama bahati, nikaona nikujulishe ujio wangu. Moja, nilipanga kuliona gari ulilonifahamisha kwamba umeninunulia, RAV4 eee!”
“Ndio hili hapa” nilitokwa na sauti ndogo ya upole.
“Waaooo!, ni zuri sana….vipi mbona huonyeshi uchangamfu wowote leo, mpenzi?. Au unaumwa”
“Hapana, ni heri ningekuwa naumwa najua pengine ningepelekwa hospitali kupata matibabu”
“Sasa kama huumwi ni nini, dear wangu?” Sikumjibu kitu, swali lake lilinipa nafasi ya kuganga maumivu ya kutenganishwa na Angela. Kabla sijanena neno, nilibaki nimeduwaa, pale nilipotizama ndio hapo hapo.
“Ehee nimekumbuka, nieleze jambo gani linakutatiza?. Maana yawezekana hali uliyonayo ndio kile ulichosema kina kutatiza”
“Hakuna, ila kuna….” nilishindwa kuongea chochote, nikainamia usukani huku matone ya machozi yakinidondoka kama mvua ambayo imekoma kunyesha huku ikiacha mabati ya dondoshe matone. Nilishindwa kumueleza, nikakumbuka jinsi nilivyo muahidi Angela mambo mengi, ikiwa kuwajengea wazazi wake nyumba. Uwanja nilishanunua, nikakumbuka pesa zangu nyingi nilizotoa kwa ajili ya kumsomesha Angela, nikiwa na nia ya kuoa mwanamke msomi. Wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumsomesha Angela, nilimsomesha kuanzia kidato cha tano hadi cha sita pia sikuona Angela ni mzigo kwangu, alipata division three kidato cha sita, nikamchukulia fomu katika chuo cha uandishi wa habari TSJ ambako alihitimu, alikiwa amepata Digrii ya Uandishi wa habari. Angela akapata kazi ya utangazaji katika moja ya Redio maarufu jijini iliyompatia jina. Niliona uchungu sana kumwacha Angela. Hata kama ni wewe usingeweza kumuacha mpenzi wako umetoka naye mbali, mmevumiliana kwenye shida na raha.
“Hakuna nini Boka? Mimi nimekuzoea siku zote, sijakujua leo wala jana, ni miaka mingi sasa. Leo unaonekana tofauti kabis…..” Sikumjibu, kila niliposikia maneno yake ndivyo matone yalivyoongezeka.
“Usilie nieleze kitu gani kimekusibu, honey?” Angela alizidi kunibembeleza, akainua kichwa changu ambacho nilikiegemeza kwenye usukani wa gari. Sasa macho yangu aliyaona yalivyoiva na kuwa mekundu ile mbaya.
“Dear, usilie nieleze mwenzio kama ni mawazo nikusaidie” Sauti ya Angela ilinipa matumaini angalau kidogo ingawa sikuwa nikiamini kama angeweza kunielewa sawasawa.
“Lazima nilie Angela, sikutegemea kwamba yangetokea hayo yanayoniliza”
“Yapi?, Sema basi laaziz wangu” Alizidi kunibembeleza.
“Angela nakupenda sana, sikuwa tayari kuachana nawe….” Sasa nilikuwa nikimtizama Angela huku machozi yakiwa yamejaa machoni na kunifanya nisiweze kuona vema.
“Mbona unanichanganya Boka…hukuwa tayari kuachana nami? Inamaana unataka kuniacha mi…” Taratibu niliona machozi yakimtiririka Angela. Wote tukawa tunalia kama watoto wachanga wenye kukosa ziwa la mama mchana kutwa.
“Angela sikutaka kuachana nawe, lakini inanibidi kufanya hivyo”
“Yawezekana vipi tutatengana bila sababu, Kwanini Boka unataka kuniacha?. Kitu gani nimekuudhi mpaka unaamua kufanya hivyo?. Nieleze kosa langu kama nikujirekebisha nijirekebishe, Dear”
“Hujanifanyia madhila yeyote, Angela. Kumbuka nakupenda sana, nimekusomesha zaidi ya miaka mitano, lengo nioe mwanamke msomi ambaye tungeweza kusaidiana katika maisha. Nielewe Angela sikutaka kwa hiari yangu, nimelazimishwa”
“Yaani Boka umeuchezea mwili wangu sasa unanibadilikia? Usitoe visingizio visivyo na msingi. Kumbuka ahadi ulizotoa juu yangu, kweli wanaume ni matapeli…” kilio kiliongezeka, Angela akawa mbogo kweli kweli, alilia bila kukoma huku akinitingisha kwa hasira kama vile alitaka kunipiga. Nilishindwa namna ya kumwelewesha zaidi, nimwambie vipi anielewe?. Nikaona kama vile hajanielewa maneno yangu ndipo nilipoamua kurudia.
“Angela nyamaza nikueleze unielewe. Sikutaka kutengana nawe…Angela”
“Hukutaka, nani kataka utengane nami?. Niambie kama nimekukosea, dear” Angela aliniuliza kwa hasira, uso ukiwa umeumuka kama andazi lililozidishwa amira.
“Hujanikosea, isipokuwa wazazi wangu hawataki tukaoana” nikamjibu nikijifuta machozi.
“Wazazi wako!!!” Sasa aling’aka huku jicho akiwa amelitoa kama jicho la fundi saa.
“Ndio, wamesema kabila lenu ni wakorofi sana na huwa hamjui namna ya kuishi na mwanaume ndani, zaidi ya ukorofi na unyanyasaji”
“Hapana Boka, siamini ….najua umepanga hivyo ili uniache baada ya kuuchezea mwili wangu. Nimefanya kosa sana kukuruhusu uujue mwili wangu, mambo ya wazazi yanahusiana vipi na makubaliano yetu….” Akakohoa kidogo kulainisha koo lake lililojaa dukuduku. “Kumbe Boka uliamua kunisomesha ilinijue una upendo wa kweli kwangu kumbe…” Maneno yake yaliuchoma moyo wangu ingawa sikuwa na ujanja. Nilishindwa kuzungumza nikabaki namtizama kwa unyonge, lilikuwa pigo takatifu moyoni mwangu. Hakuna kitu kibaya kama kuingiliwa kati penzi lako, niliona wazazi wangu wameidhulumu nafsi yangu kiasi kikubwa. Pia sikuwa na uhakika kama pengo la Angela nani Angeliziba, mbaya zaidi Angela ndiye niliyemuotesha kwenye kiota cha huba moyoni. Nikajua kama nitamkosa Angela ni wazi sitoweza kuoa tena maishani mwangu. Labda nisikie Angela amefariki dunia, pengine mawazo ya kuoa yangenijia. Si utani moyo wangu ulitumbukia katika sura na mwili wa Angela, ambaye kila nimkosapo hata siku moja humdhania anaumwa ama naye huniwaza miye kwamba nafanya nini wakati huo. Nisipomuona kwa siku nzima hujisikia mgonjwa, natamani niwe nae kila wakati. Sijui huu ni upendo gani, nilishindwa kujinasuka katika kumuwaza Angela, muda mwingi namwona katika mtiririko wa mawazo akilini. Nashindwa kumtoa akilini mwangu, nimejitahidi lakini nashindwa. Siwezi kuelezea kwa maneno kiasi nilivyozama kwenye dibwi la mapenzi kwa banati, Angela. Mpaka inafikia hatua humdhania aliniwekea dawa ya mapenzi.
“No! no! sikia Angela, ukisema nimeamua kukusomesha ili ujue nakupenda unakosea, kuujua mwili wako si kigezo cha kuachana na wewe. Naomba uelewe nakupenda sana kuliko hata unavyonipenda, Siwezi kulinganisha pendo langu kwako na kitu chochote duniani, najua ni vigumu kuniamini isipokuwa ukweli upo, nakupenda Angela, sikutaka nikuache na sitakubali kukuacha kirahisi kama wazazi wadhaniavyo. Angela …Angela naomba unisikilize basi” nilizidi kumbembeleza Angela ambaye muda wote alikuwa akilia kwa kwikwi akiwa ananitizama kwa chuki. Nilipoona bado anazidi kulia, nikajaribu kubuni maneno matamu pengine yangembadilisha Angela na kumfanya ajue bado niko nae bega kwa bega kama ulimi na meno.
“Angela…Angela, tafadhali naomba utulie basi wa moyo wangu” Nilimwita kwa majonzi.
Nilikuwa kama namzidishia hasira, alizidi kukoroma kwa kwikwi, “Angela nadhani hujui kiasi gani nakupenda, please listen to me ”
“Nakupenda sana Angela na maneno ya wazazi wangu yasikutie wendawazimu, nakupenda na sikotayari kukuacha hata kidogo. Nikifanya hivyo nitakuwa nimempinga mungu kwani wewe umeubwa kwa ajili yangu, kitendo cha kukuacha ni sawa na kuzikimbia riziki mungu alizonipangia” nilizidi kumbembeleza, tararibu nikizishika nywele zake ndefu zenye kuvutia. Sasa nikajua amekasirika, Angela hakutaka hata nizishike nywele zake, kila nilipopitisha mkono aliutoa na kunisonya.
“Hivi Boka umeniona miye mtoto mdogo wa kudanganywa, etii wazazi! Umepata chombo kipya leo unaniona Angela sina hadhi ya kuolewa nawe, kwani kabila ni nini? Inamaana wanawake wote wa kabila letu ni wakorofi na wananyanyapaa waume zao? Huo ni ubaguzi wa kabila, na kuharibia kabila zingine sifa, hata kama ndivyo lakini mimi sina tabia hiyo, siwezi kubadili maamuzi yako, nikifanya hivyo nitakuwa najikomba nikiwaomba ukoo, kama ni uzuri ninao, kama nimepangiwa kuolewa nitaolewa, si lazima wewe, naomba ujue hilo. Nimekuwa nikiwakataa wanaume wengi kwa sababu nilijua kuwakubali ni kukusaliti. Leo umenisaliti Boka, kama ni kabila nibadilishe nichukue kabila la mama yangu” Hakika Angela alilia sana, macho yakawa yamemuiva ile mbaya. Nilimuonea huruma sana, nilitamani kulia zaidi nikaona ingekuwa haileti maana.
“Angela hakuna mtu achukuae kabila la mama yake. Ila nitafanya kila njia tuoane bila wazazi wangu kutambua kabila lako”
“Usinidanganye Boka, nishajua mbinu zako” Ilikuwa kazi kumfanya Angela aniamini nisemayo. Alishajua kwamba ni janja ya nyani niliyojaribu kutumia ilikuachana naye, pengine alihisi nimeshapata mchumba mwingine baada ya kuuchezea mwili wake.
“Sikudanganyi Angela, naomba uniamini nisemayo”
“Nikuamini usemayo!!, ok. Naweza kukuamini lakini uaminifu sasa umepungua si sawa na siku za nyuma”
“Mbona umgumu kuelewa Angela, niamini nikueleze ukweli wa mambo” Ikawa shughuli pevu kumfanya Angela anisikilize na kunielewa.
“Sawa, nakuamini nieleze”Aliitikia akiwa amebadilika kidogo.
“Wazazi wangu hawakujui, wanachojua wewe unaitwa Angela na kabila lako sawa na la mama yangu, hivyo basi nitakutambulisha kabila la mama yako. Nitasema wewe ni Mgogo wa Dodoma, japo si kweli nitakuwa naogopa, najua watakubali kwani hawakufahamu. Wakiniuliza jina lako, nitakutambulisha kwa jina la Kiislamu, Amina” Taratibu nikaona Angela akitoa tabasamu kwa mbali, kisha akanikumbatia machozi yakimbubujika mashavuni.
“Usiniache mpenzi, nakupenda kuliko hata niwapendavyo wazazi wangu”
“Naamini hilo, Angela. Kitakachotutenganisha ni mauti wala si mtu ambaye nae ameumbwa kama sisi. Naomba penzi letu ling’ae kama dhahabu, pengine limulike dunia nzima kama jua na mwezi zinavyo angaza duniani” Nilitulia kidogo nikijaribu kumtuliza Angela, kisha nikaendelea.
“Kuanzia leo nitapenda uwe unavaa majuba kama mwanamke wa Kiislamu, nitahakikisha utakuwa ukijifunika uso, kiasi cha kumfanya kila mtu ashindwe kukutambua kirahisi, umenielewa?”
“Ndio, lakini Boka mi’sijui chochote juu ya uislam, hata kuvaa vazi lile. Itakuwaje?” Angalau sasa Angela alionekana kufurahia maneno yangu.
“Hilo halina tabu, nitakutafutia binti wa Kiislam, atakufundisha namna ya kuvaa, hata vipengele baadhi vya dini. Kwa njia hiyo tutafaulu kuoana, sivyo?”
“Ndio” Alijibu akitabasamu.
“Ninachokuomba Angela, usiwajengee chuki wazazi wangu. Wapende kama unavyonipenda, hata kama wanaonyesha kukuchukia, wale ni wazazi. Siku tukifunga ndoa tutakaa nao miezi kama mitano kisha nitakuwa nimemaliza nyumba yangu ya Mbezi ya Kimara tutahamia huko, sawa” nilijaribu kumuelewesha Angela, ndivyo nilivyopanga nyumba zote tuwaachie wazazi wetu. Tuliongea mengi na Angela tukakubaliana kutumia ujanja ambao wazazi wasingeuelewa, ujanja wa kumtambulisha Angela kama binti wa kigogo, aitwaye Amina.
Siku zilikwenda, nikawahakikishia wazazi wangu kutengana na Angela, ambaye hawakutaka hata kumuona sura yake. Kisa kabila lake, dini ambayo haikuchangamana na yangu. Kingine ni maneno ya Angela aliyodai miye ndiye nibadili dini niwe Mkristo. Jambo ambalo niliridhia kutokana na kumpenda sana, kinyume na wazazi wangu waliokataa wakitoa sababu chungu nzima.
Baada ya mwezi mmoja, niliwataarifu wazazi juu ya binti mwingine aitwaye Amina, si kwamba alikuwa kweli Amina ni jina tu, binti huyo ndiye yule yule wasiyemtaka, Angela. Tena niliwapatia sana kwani walikuwa kwenye maongezi ya furaha, walipanga wanitafutie binti waniozeshe, ikiwa miye mtoto wao pekee ambaye nilizaliwa kwa upasuaji. Sikuwa na dada wala kaka, hata ndugu wengine zaidi ya mama na baba yangu.
“Shikamoo baba, shikamoo Mama” niliwasalimia baada ya kuingia sebleni, tena nilipita nikiwashika mikono.
“Marahaba! Mwanangu” Baba aliitikia, akafuatia mama, “Marahaba mwanangu, vipi umetokea mjini?”
“Ndio, tena leo nina habari njema”
“Habari gani?”
“Habari nzuri sana, nimepata mchumba wa Kiislamu aitwaye Amina. Na kabila lake mgogo wa huko Dodoma” Niliwapasukia bila hata kuwapa nafasi ya swali, nilijua nikisema mchumba wa kiislam, basi wangeniuliza kabila gani.
“Eee! Huyo ndiye tunamtaka, habari za makabila mengine makatili hatutaki, sasa mbona hukuja nae?” mama alionekana mwenye furaha zaidi. Nilipomtizima baba, niligundua nae alifurahia.
“Nimeona niwataarifu kwanza ndipo mkikubali tupange siku ya kumtambulisha”
“Sawa, ni utaratibu mzuri”
“Sisi tumekubali kwa moyo mkunjufu, tunamkaribisha mchumba wako awajue wakwe zake” Ilikuwa sauti ya baba iliyojaa furaha tele.
Tulipanga siku ya kumtambulisha iwe jumapili iliyofuata, ambapo ni siku ya mapumziko. Wazazi wangu walikuwa na furaha kubwa, walitamani kusikia siku moja nikiitwa Baba kwani walijua baada ya ndoa ningepata mtoto ambaye angekuwa mridhi wa mali zangu.
Niliondoka na gari langu kwa kasi ya ajabu, nikielekea nyumabani kwa Angela alikopangisha maeneo ya Magomeni mapipa Jijini Dar, Moyo wangu ulifura kwa furaha iliyotoka kwenye keto za moyo, nikiwa njia katika foleni ya magari, nilihisi kama nachelewa na pengine nisingemkuta Angela nyumbani kwake, nikachukua uamuzi wa kutoa simu mfukoni, nikabofya namba za Angela.
“Hallo, Pretty girl, Boka naongea”
“Yaah, vipi mambo dear”
“Poa, nitakukuta nyumbani sasa hivi?…nipo kwenye taa za magomeni hapa”
“Ndio, njoo utanikuta…vipi wazazi wanasemaje?”
“Nakuja kukupa stori nzima, wala usihofu”
“Sawa, bye” Aliitikia kwa upole na kukata simu.
Dakika tano baadaye niliigesha gari langu nje ya nyumba ya kina Angela alikopangisha. Kabla sijafunga gari milango, nilipandisha vioo vya madirisha, kitendo cha kufungua mlango ilinitoke, kuna kitu kikaniambia hebutizama nje, nami sikubisha nilitizama kama nilivyoelezwa, ghafla macho yangu yakagongana na uso murua wa Angela akiwa anatoka nje. Bila kujizuia nilimtolea macho yaliyojaa ubembe, hakika macho yangu yalishawishika kutokana na mavazi yake. Alivaa sketi fupi ambayo iliacha mapaja wazi, nilishuhudia miguu yake minene iliyobeba umbo la figa namba nane, miguu yake nilitamani niikodolee macho hadi ya shibe, Angela aliumbika vema. Kifua chake niliumbwa kikamilifu kwani chuchu zake zenye ukubwa wa pipi machungwa zilijitegemea hazikuhitaji msaada wowote, kidevu chake kilibarikiwa mzunguko wa ncha ya yai. Nyusi zake ungeweze kuhisi zimetindwa kumbe ndivyo zilivyotegenezwa na muumba. Ngozi yake nyororo utadhani ute wa yai. Kwa binti huyo, nilikuwa na kila sababu ya kuwa mpole. Muda wote nilikuwa nikitamani nipate binti mwenye sifa alizonazo Angela. Sasa ulikuwa wakati wangu wa kujivunia kwamba ipo siku nitakuwa kitanda kimoja na Angela, nikiwa mume halali, si amesema atakubali kubadili dini?. Niliwaza akilini. Mwendo wa taratibu kama nguva akataye maji baharini, ndivyo Angela alivyokuwa akinifuata huku mikono yake akiitupa kwa madaha na mikogo ya maringo, naaam! Nilikuwa na kila sababu za kujisifu, endapo ningefanikiwa kufunga ndoa na Angela Shiri. Kitu kilichonifanya nimpende zaidi, hakuwa akijichubua ngozi yake, ajichubue nini na mungu alimtunukia ngozi nyororo na nyeupe kama ya mchina?. Atawezaje kumpenda mwingine wakati nilishamwonyeshea kwamba nampenda, namjali si kwa maneno na vitendo!, nani ataweza kumlaghai kipenzi changu Angela?. Alinivutia na kunichanganya kama zege.
“Mwanamke ndiye huyu, hakika anafaa kuwa mama wa watoto wangu” Nilizidi kuwaza zaidi huku nikiwa nimemtolea tabasamu pana lililoshiba midomoni mwangu. Nilijiona kidume kweli kweli iwapo niongefanikiwa kufunga pingu za ndoa na Angela binti Shiri. Nilipoona anakaribia, nikashuka na kufunga mlango, nilichokuwa nikisubiri ni busu zito ambalo lingetua sekunde yoyote.
“Ooowaoo!” Ilikuwa sauti ya Angela kwa kasi ya umeme akanikumbatia huku akinimiminia mabusu moto moto ambayo kwa kiasi flani yalinisisimua na kutibua nyongo ya huba. Tukatizamana kwa karibu mithili ya jicho na miwani. Angela alinitizama kwa ubembe, nilikuwa mrefu kidogo kama futi moja kwake, hivyo ilipendezea kwa jinsi tulilivyokuwa tumekumbatiana.
“Vipi dear, pole na safari”
“Ahsante” Niliitikia angali ninashauku ya kumkumbatia.
“Karibu ndani, tena nilikuwa kinikuwaza sasa hivi, kumbe ungenipigia simu”
“Mimi sio sasa hivi, dear. Haiwezi kupita hata dakika bila kukuwaza, mara nyingi nawaza kama unafanya nini wakati nikuwazapo, nahisi pengine unateseka sana juu yangu, pia natamani kupata likizo fupi angalau niweze kutumia muda mwingi karibu nawe. Sikudanganyi mpenzi wangu” Nilikuwa wazi kwa kile kinisumbuacho moyoni mwangu.
Tuliingia ndani tukiwa tumeshikana viuno hadi sebleni kwa Angela ambako nilipajaza kila kikorokoro kinachostahili kuwekwa sebleni, kazi yangu ya benki ilinipa mshahara mkubwa. Nilimjazia si Kompyuta, luninga, majokofu, masofa, kabati za vyombo za kisasa, redio ya CD tano na vingine vingi. Nikaketi kwenye sofa la kuketi watu wawili, pia Angela hakusta kuketi karibu nami, tena akakunja nne na kunigeukia akionyesha kila dalili za upendo wa dhati. Sikukawia kumweleza Angela kuhusu kukubalika kwa wazazi, alifurahi sana, “Nashukuru sana, nilikuwa nikiwaza jibu gani ungekuja nalo. Sasa ndoto yetu imetimia, natamani siku ya jumapili ifike. Kwani nitavaa juba na kujisitiri kama mwanamke wa-kiislamu kweli. Naamini kwa kufanya hivyo nitakuwa nimewateka vyakutosha na wataamini miye muislam mwenye kusali sala tano”.
“Ndio…ndio, lazima wakukubali, tena najisikia furaha kubwa, sijui kama nitaweza kuifananisha siku ya leo na siku zingine zote ambazo nilishawahi kuwa na furaha”
“Eee! Darling, nakupenda sana na ndoto yangu ni kuwa nawe maishani, sina mwingine wa kutibua akili yangu zaidi yako, Boka” Angela alitokwa na maneno murua yenye majonzi hasa, wakati huo alinikumbatia kwa muda kidogo, mikono yake laini kama ya mtoto mchanga ikitambaa kifuani angali ikitekenya nywele za kifuani. Hasa kucha zake ndizo zilizonifanya nihisi usingizi, kwa jinsi zilivyonikuna na kunibembeleza. Nilijiona kama mfalume, nikajua na kuamini Angela alikuwa na mapenzi ya kweli. Asingeweza kushawishika akanisaliti, nilijivunia moyoni kwamba miye ni miongoni mwa vijana wenye wanawake wazuri kwa sura na tabia. Kila nguo aliyotia mwilini mwake, hakika ilimpendeza iwe ya mtumba, dukani na hata yakuazima, kwake ingemsitiri vema na kumpendeza.
“Usijali wa moyo, tutakuwa wote katika gurudumu la ndoa, miye nikiwa dereva mwenye leseni, nina uwezo wa kuendesha gari masafa marefu usiku na mchana, sitakubali ajali za kizembe zitokee. Nitahakikisha tutafika katika safari yetu kwa usalama na amani, sitokusaliti, dear. Niamini usiku na mchana, hata ukiwa njozini niamini miye wako wa milele, nife unizike, ufe nikuzike”
“Nakuamini hababi wangu, nakuamini unavyosema huna mwingine, nakuamini utanilinda usiku na mchana, nami naomba uleweze kama wewe ni dereva mwenye leseni Class C, mimi ni gari New Brand utaniendesha upendavyo, lakini hakikisha gari lenyewe linapata matengenezo, usiniendeshe ukitaka faida, ukifanya hivyo nitakupeleka bila kukulaza porini, kama mungu atanipa uhai, nitakutunza sana dear wangu, usisikilize maneno ya abiria” Tuliongea mengi juu ya maisha yetu ya baadae, pia tuliahidiana kuoana hata ndoa ya makofi ikibidi, ilimradi kuishai pamoja.
Tulikubaliana siku ya jumapili ningekuja kumchukua Angela kwenda kumtambulisha kwa wazazi wangu, hakuwa na budi kuridhia. Siku ya jumapili ilipotimu, nilikwenda kwa Angela na kumchukua ikiwa kwenda naye nyumbani kwangu ambako niishiko na wazazi wangu, Sinza kwa Remmy. Ningemtambulisha Angela kama tulivyopanga nimwite Amina. Angela alipata mafunzo ya kuvaa mavazi ya kiislamu na jinsi ya kusalimia kiislamu, “Asalaam aleykum” “Waleykum slam” Ndivyo alivyokariri kusalimia na kujibu salamu hizo.
Tuliingia nyumbani kwangu niishiko na wazazi wangu, ingawa nyumba zilikuwa mbili, miye nilikuwa nikiishi nyumba yangu, nao yao lakini nilichokuwa nakula na wazazi wangu walikula.
Angela alivaa juba utadhani mwanamke wa kiislamu, kumbe zilikuwa magirini zetu ili wazazi wakubali tufunge ndoa, na mwanamke ambaye niliamini ningemkosa sikuwa na uhakika kama jua la kesho yake ningeliona.
“Karibu sana Amina” Nilisema baada ya kushuka kwenye gari.
“Ahsante Bakari, nishakaribia” Taratibu Angela alimega hatua ndogo ndogo, akiwa amelishikilia juba lisiburuze chini, usoni alijifunika kisawasawa, aliacha sehemu ya macho na pua tu, mkononi pia alishikilia Tasbihhi.Naaam!,hakuna ambaye angeweza kuhisi binti niliyekuwa naye pale alikuwa Angela binti wa mchungaji, Shiri. Alipendeza kweli kweli, niliamini ingemchukua miaka kumi mpelelezi kugundua kama Angela ndiye aliyekuwa akijiita Amina. Juba lilikuwa la rangi nyeusi.
“Hodi hodi humu ndani” Nilinguruma nikiwa nimetangulia, nyuma akiwa Angela.
“Karibuni!, Karibuni ndani” Mama alitukaribisha, “Asalaam aleykum”Sauti ya heshima ya Angela ilitoka.
“Waaleykum-slam” Mama alimwitikia Angela ambaye alimshika mama mkono akiinama kwa heshima.
“Shikamoo, mama”
“Marahabaa, karibu mwanetu. Jisikie upo nyumbani”
“Ahsante, nishakaribia”Angela alimjibu.
“Asalam aleykum” Nami nilimsalimia mama, baba hakuwepo.
“Waaleykum slam, huyu ndiye mchumba uliyetueleza juzi kwamba anaitwa Amina?”
“Ndio, mama”
“Loo! Hongera sana, nakupongeza sana mwanangu kwa kuchagua, si siri hapa umepata. Hawa ndio tuliokuwa tukiwahitaji, mwanamke mwenye heshima anaonekana kwa mavazi na salamu, haina haja ya kumchunguza miaka nenda rudi, karibuni sana”
“Ahsante, mama. Nishakaribia”
Baba alikuja nae nikamtambulisha kwa mchumba wangu, Angela ambaye tulimbatiza jina la uwongo Amina, wakaamini Amina alikuwa Muislam kweli kumbe zilikuwa mbinu za magirini ilinikamilishe ndoa na Angela, sikuwa na njia nyingine zaidi ya kuwadanganya wazazi wangu. Tulifunga ndoa na Angela, nikawa mume halili naye akawa mke wangu halali, tukafungua ukurasa mpya wa Ndoa.
Tulifanya sherehe ya harusi yetu watu walihudhuria hasa wafanya kazi wenzangu wa benki niliyokuwa nikifanyia kazi. Tulialika bendi mbali mbali za muziki na wanamuziki wakizazi kipya, Bongo Fleva. Walituburudisha tukiwa jukwaani, ulifikia muda wa bwana na bibi harusi kupanda mbele kucheza muziki laini, Mc akaachia vitu, tukacheza taratibu huku tukiwa tumekumbatiana vilivyo. Watu walishangilia sana, kwa jinsi tulivyokuwa tunaendana na Angela.
Baada ya miezi miwili, Angela mke wangu alipata kazi ya utangazaji katika redio moja kati ya redio maarufu nchini. Wote tukawa tunafanya kazi, miye Benki nikiwa meneja msaidizi. Jina la Angela, mke wangu likawa gumzo kila kona nchini Tanzania, nani asiyemjua, labda kwa wachache ambao hawakuwa wakisikiliza redio.
Miezi mitatu, Angela alionekana kubadilika tabia, hakuwa akiniheshimu kama mumewe, aliniona kama kijakazi wake wa ndani. Baada ya kutengewa chakula na kijakazi, yeye hakutaka kula meza moja nami, alikuwa ameketi sofani akiwa amekunja nne, taratibu akichezesha mguu wake mmoja, jicho la dharau likiwa limeganda usoni mwangu. Kila nilipomwuliza kuhusu kula alisema alikula huko kazini kwao.
“Mke wangu, mbona siku hizi umebadilika” Nilimwuliza Angela kwa sauti ya upole
“Nimebadilika!, nimekuwa wanjano, sivyo?” Swali langu ndilo lililomfanya Angela ainuke, alinikaripia kwa ukali bila woga. Akiwa amenishikia kiuno, midomo yake ameibetua kwa dharau kali. Nilitikisa kichwa kwa kumsikitikia kiasi ambacho alikosa nidhamu, sikutegemea kwamba maneno yale yalitokea kinywani mwake. Sasa nikamtizama kisha nikalamba midomo yangu.
“Angela hivi kweli unaweza kunijibu hivyo miye mumeo!, siamini kama kweli maneno hayo yanatoka midomoni mwako”
“Kwanini usiamini wakati umesikia yalipotoka?”
“Itanichukua muda kuamini kwa jinsi ulivyobadilika, lakini elewa sasa hivi hunijali, Angela…” Niliongea moyo ukitukutika ndani kwa ndani, ni miezi miwili haijafika hata mitatu kazini, leo ananibadilikia. Dharau chungu nzima!!.
“Ni juu yako wewe. Sikujali na nini?, unataka nikubebe mgongoni ujue nakupenda na nakujali?”
“Angela, nimekukosea nini hadi kunijibu hivyo, niambie basi kama nikujirekebisha nijirekebishe, dear” Nikajaribu kuwa mpole zaidi, huku nikimbembeleza kama angenieleza kosa langu. Pengine nilimuudhi bila kujua.
“Hujanikosea kitu, miye sijisikii kula vyakula vyako vya kila siku. Nyumba haibadilishi lishe kila siku wali kuku..wali kuku. Nimeshachoka na vyakula vyako, bwana”
“Lakini Angela utakuwa unanionea bure, pesa ninatoa kwa siku matumizi elfu kumi, na kila kitu nishanunua si mchele, sukari, nyama, kuku wa kufuga na hata unga upo umejaa tele. Wewe ndiye unapaswa kupanga chakula gani leo unampikia mumeo, sijakupangia upike kila siku wali kuku, tena hata leo mbona kumepigwa ugali samaki?. Mwanamke anapaswa ampikie mumewe chakula si kijakazi, hilo hutaki, hata kupanga chakula mesini, Kwako NO!. Naona kama hunipendi….Siamini Angela kama hilo ndilo tatizo” Nilimweleza machozi yakinilenga lenga machoni.
“Boka, hivi unataka kusema Elfu kumi inafaa kubadilisha chakula ndani ya nyumba, wewe unajua elfu kumi ni nyingi sana. Wenzako wanakula vyakula vizuri..wewe kwako ni Kuku… kuku, nani kakuambia kuku ni chakula?”
“Usiangalie familia za wenzako, mke wangu. Hebu angalia na uwezo wetu” Nilizidi kumsihi Angela taratibu ingawa hakutaka kunielewa hata punje.
“Vijana wanafanya kazi ya vibarua hapa mjini lakini wanakula vizuri kuliko sisi, hushangai, Boka!”
Kadri nilivyo mwuliza ndio alivyozidi kuwa mbogo mjeruhiwa, ikanipasa niwe mvumilivu na nimchunguze nini hasa ninampa jeuri namna hiyo. Angela hakuwa na miezi miwili toka tumefunga ndoa. Nilitafakari nikahisi alibadilika kwa sababu alikuwa na uhakika wa kupata pesa, alishakuwa maarufu katika utangazaji, ingawa fikra zingine zilinifanya nihisi kwamba pengine Angela alishaanza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine aliyempenda zaidi yangu. Kama si hivyo, nilimfanya kitu gani hasa ambacho kinafanya anichukie kiasi hicho?. Nilizidi kujiuliza maswali mengi bila jibu la kunifaa.
************
Kilio changu ni hii ndoa yangu ambayo haina umri mrefu, lakini imejaa maovu na jakamoyo. Nilitegemea katika ndoa yangu ningeishi maisha ya raha na starehe kwa huyu mke wangu, ingawa sasa imekuwa kinyume na matarajio yangu, naishi kwa mateso kweli kweli, mpaka nimefikia kutoa kilio changu hadharani, nivingumu kuamini na hata kama utaamini basi yawezekana ukakerwa na tabia ya mke wangu.
Kila nikikumbuka tulipotoka na mke wangu, muda si punde machozi hunitoka. Hakuna sababu ya kunicheka ama kuniona miye mjinga, sikutaka maisha haya bali nimejikuta nikiwa katika wakati mgumu.“Eti kwanini dume-zima linalizwa na mkewe”. Nina kila sababu za kulia, Angela nimetoka naye mbali sana japo sisi wanadamu tuwepesi kusahau tulipotoka.
Ndoa yangu inayumba kama mlevi huku ikiwaya waya kama machela, sina uhakika kama itaweza kusimama imara, dalili kubwa ni kuvunjika, na isipovunjika pengine nikaendelea kuwa mtumwa wa ndoa.
Nakumbuka mwanzoni nilitamani sana kuitwa mume wa mtu, nikijiapiza moyoni na hata waziwazi kwa Angela Shiri sitojinasua, kama nitajinasua basi baada ya mauti kunifika. Leo najuta huku nikisononeka kwa mateso ya ndoa yangu. Wakati mwingine siamini kabisa ingawa kuna punje za fikra zenye kuchomoza ubongoni kama mshale wa sekunde. Fikra hizi kidogo hunifanya niamini kinachonisibu kila siku za maisha yangu.
Pindi mke wangu anifanyiapo madhila, fikra nyingi hunijia zikininong’oneza kwamba mke wangu hana mapenzi ya dhati kwangu na kwa sababu hiyo niachane naye lakini upande mwingine pia hunionya kwamba kuachana na mke wangu si suluhisho la jambo, pengine niendelee kuwa na subira, na nizidi kumwomba mwenyezi mungu atanitatulia matatizo katika familia yangu, kwani hata binadamu wenzangu wamelishindwa. Zaidi ya fikra hizo, ubongo huzidi kunisisitiza kama nitatengana nae, huenda nikawa nakimbilia mateso mengine zaidi ya haya ya mke wangu, Angela.
Naamini sana, mke wangu ananinyanyapaa ndani ya unyumba wetu, Pamoja na kuamini siwezi kutoa maamuzi yenye uzito wa kuweza kupingana na matakwa ya mke wangu. Wengi mtaniita mume bwege lakini si hivyo, naweza kusema mimi ni mume mwenye busara, mvumilivu na pia mwenye upendo wa dhati kwa mke wangu, hata kama yeye haonyeshi dalili yoyote juu ya upendo zaidi ya kunitesa. Kweli dunia sawa na mdomo wa mbuzi, wenye kutafuna huku na kule, Dunia gurudumu lililoisha upepo, tena lenye kuzoa kila chochote likikanyagapo, kiwe kibaya ama kizuri.
Toka nimeoa yapata miaka miwili sasa, lakini nimeona kama miaka arobaini. Nyumbani kwangu napaona kama kituo cha polisi, tena wakati mwingine nahisi ni Jehanamu, ambapo kuna mateso kwa wale waliotenda maovu duniani. Nikisema nimechakaa usinishangae, yaani sura yangu imejaa makunyanzi ya uzee utafikiri miye babu kumbe hata mtoto sina, tena mbaya zaidi umri wangu miaka thelathini. Angela, mke wangu amenifanya mtumwa tena yule mtumwa enzi za ukoloni, sina haki juu ya mwili wa mke wangu, sina matilaba juu ya mwili wangu, tena naweza kukushangaza kazi yangu ya meneja wa benki lakini nifikapo nyumbani unaweza ukanifananisha na kijakazi wa ndani, tena yule ambaye hana baba wala mama.
Wakati mwingine hujikuta nikiongea peke yangu barabarani kama mwendawazimu, yote ni juu ya madhila ya mke wangu. Nimenusurika kifo mara kadhaa, kutokana na kulemewa na mawazo yanayosababishwa na mke wangu. Nikiwa hata barabarani Kariakoo, Posta na pengineko, hushitushwa na honi za magari kwani hujisahau na kutembea katikati ya barabara. Si kwamba nimeamua kufanya hivyo, bali najikuta kwa lazima ambayo siifahamu, yawezekana nimechanganyikiwa. Nimeshapitishwa vituo kadhaa vya daladala na hata kile kituo nishukapo ili kwenda nyumbani, pale Sinza kwa Remmy. Mara nyingi nikumbukapo maisha ninayoishi na Angela, machozi hunitoka kwa uchungu sana. Ndugu yangu, jamaa na marafiki zangu msiombe kukumbana na mwanamke mbabe, mwenye sheria za kujitungia kama wale wanaume wenye mfumo-dume.
Sitomsahau Angela siku zote za maisha yangu. Mwanzo wa ndoa yetu niliamini na kutegemea kama ningekufa basi ndiye angekuwa mstari wa kwanza na pengine angekuwa wa kwanza kutupia maiti yangu udongo kwa uchungu, lau kama si miye basi angetangulia yeye, ningeufinyanga udongo kwa uchungu huku nikitokwa na machozi kufiwa na mwanamke wa maisha yangu. Lakini sasa, sijui kama nitatokwa na hata chozi iwapo Mungu akichukua roho yake kabla yangu.
Mateso ya Angela hata kama ndoa itavunjika, kidonda bado kingali rohoni, ijapokuwa namuomba Mungu kila wakati.
“Mungu nipe amani katika ndoa yangu, nipe uvumilivu, nipe heshima, niepushe na walimwengu wenye kuharibu ndoa yangu, Baba, mungu muumba wa vyote naomba umbadilishe mke wangu fikra mbovu kisha umpe heshima awe mcha-mungu, naamini kwako vyote vinawezekana, wewe ndiye muumba wa vyote na ndiye mwenye uwezo wa kumbadili tabia mke wangu, mungu ukinisaidia nina imani ndoa yangu itanusurika”. Haya yalikuwa maneno yangu kila panapokucha.
Najuta sana huku nikiwakumbuka wazazi wangu ambao walikuwa wakinishauri juu ya mwanamke wa kuoa. Nakumbuka vifo vya wazazi wangu zilisababishwa na huyu mke wangu ambaye pia ananitia jakamoyo, sina raha, sina amani ya kiroho na sina uhakika kama ni huyu mke ambaye nilitetea maisha yake toka utotoni, ndiye aliyetoa uhai wa wazazi wangu, nilio wapenda kama ninavyompenda mungu.
Kila siku nimekuwa nikipata mateso si chumbani, sebleni wala kazini. Mke wangu, Angela amekuwa akinionyesha hata vile visivyofaa kumwonyesha mwanaume wa Ndoa.
Sijui kama familia nyingine ndivyo zinavyoishi ama ni mimi peke yangu. Mke wangu tukiwa chumbani hunitesa kweli. Wakati mwingine naona hakuna upendo wa kweli. Nakumbuka miezi mitatu toka nifunge nae ndoa kanisani, alibadilika si kidogo. Tukiwa chumbani, ananuna na kunitizama kwa dharau isiyo ya kawaida, mbaya zaidi hataki kunipa haki yangu ya unyumba. Mwanzoni nilifikiri anafanya utani lakini nikaja kugungua kwamba haukuwa utani bali ndiyo alivyoamua.
“Angela wewe kila siku husema, unaumwa...mara hujisikii vizuri...hutaki kulala na mimi.....wakati mwingine unasema mara ni usiku mno, unasikia usingizi. Mchana unasema kuna joto. Nikuelewe vipi, dear”
“Unielewe vipi, bila pesa ya kununua cheni ya dhahabu silali na wewe” Yalikuwa maneno yaliyoniacha mdomo wazi, mke wangu wa ndoa anataka pesa ya cheni ya dhahabu ndipo alale nami. Bila hivyo hakuna mapenzi. Nilisikitika sana huku nikisononeka rohoni.
“Cheni si-nilikuambia nitakununulia ya gramu themanini kesho?”
“Hapana, sitaki ya gramu themanini, nataka ya gramu mia na ishirini” Alisema bila huruma mwanamke yule ambaye sasa nilimwona muungwana wa sura na macho. Niliamini alifanya makusudi kweli kwa jinsi alivyo vaa, alikuwa akiniumiza moyo wangu.
“Sawa, nitakununulia, usijali” Nilitii sheria kwa shingo upande, nilijua ni mwanzo wa kuingia katika utumwa wa mapenzi.
“Sio kuwa utaninunulia, nataka unipe pesa leo leo, nitaenda kwa Sonara kesho....Looo!!, nitajivunia vipi kazi ya mume wangu. Unafanya kazi benki..tena wewe meneja msaidizi..halafu mkeo anavaa vicheni vya gram ishirini, sikubali. Usiponipatia chumbani siendi” Angela mke wangu alicharuka kweli kweli, alikuwa amekaa kitini, akainuka na kwenda sebleni ambako aliketi sofani akinitizama kwa ghadhabu kali. Niliona kwa kumridhisha, nikubaliane na matakwa yake.
“Unataka kiasi gani cha kununulia cheni yako?”Nilimwuliza kwa upole.
“Nataka ninunue dhahabu halisi, itakayo nigharimu laki mbili na nusu” Nilimtizama, kisha nikatingisha kichwa kwa uchungu sana.
“Sawa, kwa vile umeamua hivyo. Chukua” Niliingiza mkono mfukoni nikatoa laki tano, nikamuhesabia shilingi laki mbili na nusu, pesa zingine nilizirudisha mfukoni. Alipo maliza kuzihesabu, alinikaribia na kunibusu shavuni, nilihisi kama amenipika kwenzi badala ya busu, hakika lilikuwa busu la utumwa. Siku nisikia furaha hata kidogo, ndio kwanza alizidi kunikasirisha.
“Umefurahi, twende basi chumbani” Nilimsihi, wakati huo nilitizama saa yangu ya mkononi. Ilikuwa akrabu saa saba na nusu usiku.
“Si-hisi usingizi, kabisa. Tangulia nitakuja baadaye”
“Hapana, dear. Si nimekuambia nataka kuwa karibu nawe?”
“Ndio, lakini miye si-hisi usingizi”
“Angela, unatatizo gani?”
“Sina”Alinijibu akinibetulia midomo.
“Sasa mbona hutaki kwenda kulala nami?”
“Sio kuwa sitaki, sihisi usingizi”
“Sawa, hata kama huhisi usingizi, kwende ukajipumzishe. Nataka kuongea nawe maswala ya maisha yetu”
“Mambo ya maisha yanazungumziwa kitandani!!. Du!!, sebleni ndio mahala pake, Boka”
“Sikiliza Angela usijifanye mwerefu kwa ujinga, mimi ni mumeo wa ndoa lazima unisikilize na unijali. Lazima umpe mumeo haki yake. Usiku huu hutaki kulala una maana gani?. Naona siku hizi Angela, mke wangu umebadilika si kidogo. Huna mapenzi ya kweli kama awali, siku zingine hulala kwenye sofa. Nikikuuliza unanijibu ‘NIMEAMUA’ Naona umeshanionyesha dalili ya mapungufu ya mapenzi kwangu, ukiwa unatangaza redioni unawachangamkia wasilkilizaji, lakini miye mumeo hutaki hata kuishi kwa raha ndani ya nyumba, niambie umempata nani anayekufanya unione kikaragosi?”.
“Hakuna”
“Kama hakuna basi twende tukajipumzishe”
Hakuitikia aliinuka, “Tunaenda lakini.....”
“Lakini nini Angela?”
“Naumwa, tutalala mzungu wa nne, tukubaliane hapa hapa” Sauti hiyo ndiyo iliyonifanya nikune kichwa, kila siku Angela amekuwa akitumia maneno hayo.
“Sawa, unaumwa na nini?”
“Tumbo” Tulielekea chumbani, alinisubiri hadi nilipolala kitandani ndipo nae alipopanda kitandani.
Asubuhi palipambazuka angali nipo macho, sikupatwa hata lepe la usingizi. Akili yangu ilijawa na madhila ya mke wangu, moyo ulikuwa ukiniuma sana. Tuliishi kwa maneno, hatukuwa na raha ndani ya nyumba, hata nilipokuwa kazini niliwaza sana maisha ya nyumbani kwangu, nilitamani nibaki pahali ama nitafute hata binti ambaye angeniliwaza shida zangu. Kwani Angela hakuniona kama mumewe zaidi ya kuniona Buzi lake. Asubuhi hiyo, kama kawaida yangu nilioga na kunywa chai niliyotengenezewa na kijakazi, mke wangu angali alikuwa kitandani.
Niliingia chumbani kumuaga mke wangu, hakunijibu lolote zaidi ya kunitizama kwa dharau. Nikakata shauri kuondoka, nikiwa kazini mawazo mengi yalinizonga. Wakati mwingine niliongea mwenyewe, si kwa ridhaa yangu. Nilijikuta nikitokwa na maneno kwa lazima nisiyoifahamu.
“Hivi kwani mke wangu ananitesa namna hii…nimemkosea nini hasa hadi kunipa adhabu hii kali, hanipendi......hafanani kamwe na Angela niliyemsomesha na kumtunza kwa hali na mali. Kama nimemkosea aniambie basi nijirekebishe, mimi kama mwanaume nahitaji kuwa na mtoto niitwe baba, mke wangu hilo halitambui kabisaa!!…kama ni mateso ndiyo haya…lakini yawezekana amepata mwanaume anayempenda…eee!! Ndio ndio…..” Nilizidi kuongea kimoyomoyo hadi niliposhitushwa na mtu aliyebisha hodi ofisini kwangu.
“Karibu..karibu uketi” Nilimkaribisha baada ya kumwona kwamba alikuwa sekretari wangu.
“Shikaamoo kaka, Bakari” Nilishituka badala kuitikia.
“Eee! Unasemaje, Nancy”
“Nimekusalimia”
“Marahabaa, nikusaidie nini, Nancy?”
“Nimetumwa na Mkurugenzi Hans Chopa, anasema una matatizo gani?”
“Sijakuelewa, ana maana gani?”
“Kutokana na yale madeni ya milioni mia mbili ya kampuni ya Ujenzi, hayajalipwa wewe umeandika yamelipwa. Mbona kwenye akiba yao hayajaonekana?”
“Kaaa!!, kwani ndivyo nilivyo andika?”
“Ndio, Bosi. Hebu ona, karatasi zake hizi hapa” Nilizitizama zile karatasi kwa muda kidogo, nikiwa siamini kama mimi ndiye niliyesaini nimepokea milioni mia mbili za kampuni ya Ujenzi.
“Umeamini, Bosi?”
“Ndio”Niliitikia kwa sauti ya chini ambayo hata mwenyewe sikuisikia vema. Sauti yangu tosha ilikamilisha sentensi kwamba nilitingwa na mawazo mazito.
“Siku hizi umebadilika sana, bosi. Una matatizo gani, wakati mwingine nakusikia ukiongea peke yako, na muda mwingi unakuwa ukisunya ovyoo hata ukiwa mwenyewe. Halafu naomba uniambie Angela ni nani?”
“Kwanini unaniuliza hivyo?” Nilitaharuku, sikutegemea kama Sekretari wangu angeniuliza swali kama hilo.
“Wee niambie, nitakuambia kitu” Nilikaa kimya nukta kadhaa, nikamjibu kwa majonzi nikitokwa na machozi taratibu.
“Ni mke wangu” Sekretari wangu aliniuliza maswali mengi ingawa sikuwa tayari kutoa siri yangu ya unyumba, nilimdanganya kwa maneno mengi ambayo nilihakikisha hayamfanyi akaamini kwamba nilichanganyikiwa kwa ajili ya madhila ya mke wangu.
Baada ya kutoka kazini, nilirejea nyumbani nikiwa nimechoka akili na mwili. Wakati mwingine nilifikiri dawa ya kupunguza mawazo ni pombe, nikawa nakunywa. Pamoja na kunywa bado nilizogwa na mawazo. Mke wangu hakuwa nyumbani, nilijaribu kumpigia simu, akawa hapokei. Sikuchoka kupiga nikihisi alikuwa mbali na simu, kama mara tano nilirudia. Simu haikupokelewa, mara ya sita alipokea na kusema yupo kwenye kikao ofisini, nikaona nijaribu kuchunguza, si kwamba nilikuwa na wivu, hapana. Matendo yake ndio yaliyonilazimu kufanya upelelezi wa kina. Nilimpigia rafiki yangu Aloyce Tilly, ambaye ndiye alikuwa anaingia baada ya Angela, mke wangu.
“Hallo, my Friend Aloyce. Habari za kazi”
“Nzuri bwana, Bakari…”
“Eeee!! Bwana Alocye, nina shida na Angela kidogo maana kuna wageni wangu kutoka Afrika kusini, wanataka kumsalimu, kisha wataondoka leo leo….Angela atakuwa kwenye kipindi ama amemaliza kipindi?” Nilimweleza uwongo wa ujio wa wageni, nikijitahidi kuficha uchungu moyoni. Nilishaanza kuwa na wasiwasi na mke wangu.
“Angela alimaliza kipindi nusu saa iliyopita, na hana kipindi mpaka kesho asubuhi”
“Ohooo!…ahsante sana, yupo hapo kazini?”
“Hapana, aliondoka na ile NISSAN TERRANO yake” Maskini miye Bakari. Moyo ulinipasuka sana, nilijikuta nikitokwa na machozi, mke wangu hakuwa na gari aina hiyo, nilimnunulia RAV 4, Aloyce anasema Nissan Terrano?.
“Mke wangu hana gari aina hiyo, Aloyce. Nilimnunulia RAV 4 new model”
“Yaah!, sijui kama umemnunulia gari aina gani, lakini ukweli Angela amekuwa akija na NISSAN TERRANO, siku hizi haji na la RAV 4. Samahani kama nimekukosea rafiki yangu, Bakari”
“Nisaidie, Aloyce. Mke wangu nampenda sana, nimempigia simu ameniambia yupo kwenye kikao ofisini. Aloyce nifanyeje?”
“Sorry Bakari, tutaongea nikimaliza kipindi. Naona mazungumzo marefu hadi nimekuwa nikipiga muziki, bila hata kuongea kidogo, ok, bye” Aloyce alikata simu, nilijua hata hivyo alifanya kwa vile miye ni rafiki yake mkubwa sana, tulisoma nae kuanzia kidato cha tano na sita na baadae Chuo kikuu.
Si utani ndugu msomaji, niliumia sana moyo wangu, nilijuta kwanini mungu alinikutanisha na Angela ambaye aliutesa moyo wangu hadi ilipofika wakati nikawaza kujiondoa duniani, lakini mawazo hayo nilijaribu kuyaondoa akilini yasinijie tena.
“Hakuna mapenzi ya kweli, Angela ambaye alinitamkia kwa ulimi wake hatoweza kuishi kwa raha endapo sitafunga naye Ndoa lakini sasa Ndoa yangu imekuwa ya Utumwa!!!. Nimemfanyia mengi mema lakini hafanani kamwe na watu wale walioumbwa na mwenyezi mungu”
Nilisubiri hadi Aloyce alipomaliza kipindi ndipo nilipomwomba tukutane mahala fulani ambapo pangekuwa tulivu, alikubali. Tulipanga tukutane ZOO BREAZE INN, maeneo ya Kinondoni, niliondoka na gari yangu ndogo, Corolla G – Touring. Kama robo saa kutoka Sinza hadi Kinondoni nilitumia, nikaegesha gari langu na kuelekea ZOO BREAZE INN, niliingia niking’aza macho juu juu bila kumwona Aloyce. Nikafikiri nimpigie simu, nilipompigia alinielekeza kona aliyoketi. Nikaenda ambako nilimkuta akijipongeza kwa Akari aina ya Guiness baridi kabisa.
“Yes..vipi best” Ilikuwa sauti ya Aloyce Tilly, akinipa mkono wa kuume.
“Poa, mambo vipi?”
“Safi, karibu….eee!! muhudumu”Alimwita muhudu aliyekuwa jirani na meza tuliyoketi. Muhudumu akaja,
“Msikilize, brother”Aloyce alisema akiinua glasi ya bia kwa safari ya kinywani.
“Karibu anko?”
“Naomba kama ya ndugu yangu hapo” Nilimwonyeshea kidole bia ya Aloyce.
“Ya baridi?”
“Nimekuambia kama ulivyomletea, hunielewi?” Nilisema bado angali hasira za mke wangu nikizileta hata sehemu za starehe. Lakini nilipaswa kusamehewa kutokana na akili kunganganyikiwa, niliona kila mwanamke ni mbaya kwangu. Muhudumu aliondoka, nikasogeza kiti changu karibu na Aloyce.
“Aloyce kwanza napenda uniwie radhi kwa usumbufu uliojitokeza na utakaojitokeza”
“Bila samahani, Bakari. Zungumza, wewe ni kama ndugu yangu..tumesoma wote na tumekuwa marafiki wa siku nyingi”
“Ahsante, nashukuru sana Aloyce… Rafiki yangu ni ndugu yangu....tena wakati mwingine anaweza kunisaidia kuliko ndugu wa kuzaliwa tumbo moja”.
“Ndio” Nilimweleza Aloyce mwanzo hadi mwisho jinsi tulivyo juana na Angela hadi tukafunga ndoa. Pia nilimfahamisha mambo yote aliyokuwa akinifanyia ndani ya nyumba, niliamua kutoa siri yangu hadharani kusudi Aloyce nae aumie kama yangemwingia akilini. Pia nilihitaji ushauri kutoka kwake. Sikuweza kuvumilia kila nilipoelezea madhila ya Angela machozi yalinitoka.
“Pole sana, Bakari. Naomba unisikilize”
“Nakusikiliza, Aloyce. Pia nakutegemea katika kunitatulia tatizo langu, sijawahi kumwelezea mtu yeyote kilio changu” Nilitulia na kumsikiliza Aloyce kama mtu asikilizae Usia wa mzazi.
“Umesema Nissan Terrano si wewe uliyemnunulia mkeo?”
“Ndio, sijamnunulia mke wangu” Kulia kwangu kulikuwa kwa uchungu, nilishaamini mke wangu alishapata mwanaume aliyempenda na mwenye nazo. Aidhaa, aliniona sifai kuwa mumewe tena na kunichukulia kama Anzali, pengine mateso yote ilikuwa njia ya kutafuta talaka.
“Huna ndugu yako, mnene mwenye kitambi ambaye anafanya kazi serikalini?”
“Hapana, nimezaliwa peke yangu. Aloyce...”
“Usilie rafiki yangu, nitakusaidia. Mimi ni nduguyo.....nataka unyamaze kwanza ndiyo tuweze kuongea”Aloyce alinieleza, nikamsikiliza, nikajikaza kiume na kufuta machozi kwa leso yangu. Nilikuwa sasa nimetulia, machozi hayatoki tena ingawa macho yangu yalikuwa mekundu na mishipa ya usoni ilikuwa imetoka kama mkia wa panya.
“Hivi ni kusema mkeo alikuwa na tabia hiyo, ama baada ya kufunga ndoa”
“Hakuwa na tabia hiyo, baada ya kufunga ndoa na mke wangu, mwenzi mzima tulikuwa kukipendana, alinijali nami nilizidisha mapenzi kwake, sikudanganyi Aloyce...Angela alinipenda sana. Kila nilipokuwa nimechelewa kurudi nyumbani hata nusu saa, alinipigia simu akitaka kujua kulikoni?. Siku zingine alikuwa akija kunichukua na gari lake ambalo nilimnunulia siku ya harusi yetu. Mara kwa mara alimwambia kijakazi wa ndani, asipike chakula, yeye ndiye angenipikia na kuniandalia mezani....pia hakusita kunilisha chakula nami nilimlisha kwa upendo wa dhati, tulikuwa tukienda wote bafuni kuoga lakini ghafla kama uhai na mauti Angela mke wangu alibadilika. Dharau ikaanza kuota akilini kama ukoka. Nilishindwa kuelewa nani aliyembadilisha..lakini nahisi baada ya kumtafutia kazi..ndipo alipoanza dharau”
“Hapana, dharau hakuipata ofisini, hilo namtetea. Mbona hapa ofisini kuna wake za watu karibu sita na wanajiheshimu?. Itakuwa tabia yake” Nilikaa kimya.
“Eeee!! Kuna mwanaume mmoja anayependa kumleta mara nyingi na gari aina ya Land Cruiser VX, ila baada ya nusu saa gari ambayo ni NISSAN TERRANO huletwa na dereva mmoja na kuipaki nje kisha anampigia simu Angela kwamba ameshaleta gari, siku nyingine Angela hajanalo mwenyewe bila mtu. Mara nyingi nimezoea kutaniana sana na Angela, siku alipokuja nae huyo mwanaume hadi ofisini, nilimwuliza ni shemeji nini?...Alidai ni kaka yake....lakini kaka gani ambaye anaonyesha kila dalili ni mpenzi wako ama baba watoto... alinijibu “Acha ushamba Aloyce, kaka yangu kunipiga busu ni ajabu....wabongo bwana”Aliongea akionekana ukasirika ingawa tumekuwa tukitaniana. Naomba uelewe sina nia ya kuivunja ndoa yako lakini unapaswa ufanye uchunguzi wa kina usiende nyumbani kugombana naye kwa sababu miye nimekuambia mkeo analetwa na gari na jamaa mmoja kibonge...chunguza upate uhakika.....pengine ni shemejio, yaani kaka yake na mkeo....umenielewa bwana Boka?”
“Ndio” Nilijibu kwa shida huku nikiuma meno kwa ghadhabu kali moyoni. “Kwanini mke wangu amekuwa guberi, ananiona Bozi, huku akinianzali, na zaidi anakuwa Bazazi, anaufanya moyo wangu uwe na Basua?” niliwaza kwa sekunde chache, sikupata jibu. Jibu nililopata lilikuwa kuinua glasi ya bia mezani, kwa kasi ya umeme nikaielekeza kinywani ambapo niliigugumia yote tumboni kisha nikacheua, na kumtizama Aloyce.
“Kumbe nawe ni kihondi, siyo?”
“Hapana, yote ni kwa ajili ya mke wangu Angela anautesa moyo wangu” Nilimweleza kwa uchungu mwingi, nikaimimina bia na kuinywa kwa kugugumia yote bila kubakiza hata povu.
“Eeee! Kweli Angela amekuchanganya, Boka. Sasa nitajaribu kumchunguza Angela, mwanaume huyo ni nani hasa, je? ni kaka yake ama hawara yake. Usijali Boka, nipo pamoja nawe kuhakikisha mkeo anarudisha upendo kwako....unajua hakuna mtu awezaye kupenda watu wawili, aidhaa mmoja atakuwa anamdanganya na mwingine atakuwa anampenda kutoka moyoni. Don’t worry my Friend, i wili help you”
“Nitashukuru, ndugu Aloyce”. Aloyce alikunywa bia yake taratibu, tukaagana. Nilimwacha Aloyce pale baa kwani aliniambia kuna mchumba wake aliyepeana miadi ya kukutana pale.
“Ok, usijali Boka, yaone ni matatizo madogo, sawa?”
“Sawa, Aloyce” Nilimjibu na kuinuka taratibu nikielekea nilikopaki gari yangu.
Nilirudi nyumbani saa moja usiku, nikagonga mlango. Takribani dakika mbili mlango ulifunguliwa, alikuwa kijakazi wetu wa ndani.
“Shikamoo, Baba”
“Marahabaa, mama amerudi kazini?” Nilimwuliza, nikitizama saa yangu ya mkononi.
“Bado”alinijibu na kuelekea jikoni akiendelea na kazi zake. Sikutaka kumhoji yule binti maneno mengi, nilienda kujibweteka sofani, kichwa changu kikiangalia juu, nilifikiri mambo mengi, niliwakumbuka wazazi wangu ambao walikufa wakiwa chumbani kwao. Sikuwa naamini kijakazi aliyenieleza juu ya vifo vya wazazi wangu, “Kweli wazazi wangu wamekufa na yawezekana kweli Angela ndiye aliyewapa sumu. Alifanya kwa makusudi iliaweze kunitesa miye Boka.....”Nilipofikiri hivyo, mara nikakatishwa fikra na binti aliyekuwa akitusaidia kazi za ndani.
“Baba karibu mezani, ule chakula”
“Hapana, usijali nimekula” Hata hamu ya kula sikuwa nayo, toka nilipokula mchana na zile bia mbili basi, sikutia kitu kingine tumboni.
Nikahisi nifungue Jokofu nichukue bia baridi ambayo ingenifanya nipoteze muda hadi Angela atakaporudi. Nilifanya kama nilivyo waza akilini, nichukua Guiness zangu mbili nikaziweka mezani, nikachukua glasi moja na opener . Nilianza kunywa bia ya kwanza, ilikuwa saa tatu na nusu usiku. Nilipomaliza bia ya kwanza, nilifungua ile iliyobaki nikaanza kuinywa, hii nilikuywa taratibu, nikivuta muda. Saa tatu na nusu iligonga, nikiwa bado mlango wazi namsubiri Angela, mke wangu. Pamoja na subira, bado Angela hakuwa amefika. Muda ulisonga mbele, na kufika saa tano na nusu, nikafungua simu yangu ambayo nilikuwa nimeizima. Nikajaribu kumpigia simu Angela, “Hallo, dear. Nakuja, ndio tumetoka kwenye kikao”
“Sawa, nakusubiri mke wangu” Nilivumilia na kumjibu kwa sauti ya ukarimu kabisa, moyoni nilisikia kama pasi ya moto inauchoma moyo wangu.
“Haikosi alisema akilini mwake, mume ninaye, tena namkalia nitakavyo, naweza kulala hata nje, nikisingizia kazi yangu. Atanibabaisha na nini huyo bweha. Natembea na watu wenye vyeo zaidi yake na wenye hadhi ya kutembea na mimi, sio yeye kikaragosi tu, ama anzali, tena nilifanya kosa kuolewa naye, lakini hakuna tabu ndoa nitaivuruga tu”
Nusu saa baadaye, nilisikia mngurumo wa gari sambamba na breki kali, gari likasimama nje ya jengo langu. Nikaamua kuinuka kwenda dirishani ambako nilichungulia kuona ni gari gani?. Lilikuwa gari lile lile alilonieleza Aloyce, NISSAN TERRANO. Sikuamini kama kweli macho yangu yalikuwa sawasawa, nilijaribu kuyapikicha iliniweze kuona vema. Moyo ulinipasuka sana, walitulia ndani ya gari kama dakika tatu hivi, sikuweza kuwaona kwasababu vioo vya gari lile vilikuwa na tinted, isiyo ni ruhusu kuona mtu aliye ndani. Sasa nilimwona Angela akishuka harakaharaka, nikaondoka dirishani na kurudi sofani, dakika ama sekunde kadhaa nilisikia mlango ukigongwa.
“Karibu..” niliinuka na kumfungulia. Nilijifanya kupikicha macho kama vile, ndio kwanza nimetoka usingizini.
“Vipi dear, za kazi”
“Nzuri”alinijibu bila hofu.
“Pole, na kazi”
“Ahsante, dear. Kazi zetu za utangazaji ni ngumu sana, mara leo kuna vikao...mara uandae vipindi” Akatulia akinitizama usoni. Nahisi alikuwa akinisoma mawazo yangu, na pengingine alinidharau vya kutosha. Haikosi alisema kimoyomoyo, “Sisi wanawake wasio waaminifu niwajanja sana, tunaweza kuwachezesha waume zetu kama mpira, wanaujanja gani?. Naweza kuwapanga katika makundi mengi bila wao kujijua. Hebu ona sasa hivi nimeletwa na mwanaume ambaye nilishinda nae kutwa nzima, nimemdanganya mume wangu amekubali, kweli mume wangu hafanani kamwe na wanaume wenziye pengine ni Barubaru”
“Pole nawe na kazi” Aliinua kichwa.
“Nishapoa, dear” Nilimjibu nikijikaza kuyazuia machozi yasinitoke, ukweli wa mambo nilishaujua. “Umeshakula?” Nilimwuliza.
“Ndio, labda unipatie wisky ya baridi” Nilimtizama kwa sekunde kadhaa. “Angela unakunywa pombe siku hizi, umeanza lini?” Alishituka na kunigeukia.
“Kwani hujui nakunywa pombe?”
“Sijui..ndio kwanza nakuona leo, mara nyingi tulikuwa tukitoka na ulikuwa ukiniambia hutumii kilevi chochote, imekuwaje leo”
“Nimefundishwa na rafiki yangu, Naomi. Nakumbuka siku ya kwanza ilikuwa kwenye sherehe yake ya kuzaliwa, nikajifunza na sasa, nimezoea”
“Una muda gani kutoka ujifunze?”
“Mwezi mmoja”Alinijibu bila kupepesa macho.
“Nice, eee! Angela kwa bahati mbaya jokofu halijawekwa Wisky, labda tutoke kwenda kununua kisha tutarudi”
“Hapana najisikia vipaya, labda ukaniletee”
“Nitamtuma Ramla akakuletee”
“No, kwanza sihitaji tena” Sikutaka kumweleza Angela chochote juu ya kile nilichohadithiwa na Aloyce, nilijua kwa kufanya hivyo ningeharibu upelelezi wangu, nilishaanza kuamini maneno ya Aloyce baada ya kuona NISSAN TERRANO, Ila sikumwona mtu niliyetaka kumjua. Nilimtizama Angela machoni, hakika macho yake yalikuwa kama ametoka usingizini, yaliivaa sawa sawa.
“Dear, mbona macho mekundu umekuwa fundi wa kuchomea nini?”
“Hapana, nahisi usingizi, sijazoe kuchelewa kulala” Alinidanganya huku akibonyeza bonyeza namba za simu yake. Nikiwa bado nashangaa, Angela aliipeleka simu sikio la kushoto, mkono wa kuume ukishika shika nywele zake ndefu taratibu. Nilihisi aliposikia simu inaita ndipo alipoamua kuondoka kama anaenda nje, alifungua mlango wa getini akawa anatoka. Nami sikuona tabu kumfuatilia kiujanja ujanja nikibojea taratibu, bila yeye kuniona.
“Hallo, dear....umefika salama nyumbani?.......nimekuwa na wasiwasi kama umefika salama.....Yaaah, usijali nitakuja.......kesho!!, at what time darling.... saa moja ni mapema sana, tufanye saa tatu usiku...ndio..ndio..Ok, nice dearms.. Ok bye .Mmmmwaaa!!” Jasho zito lilikuwa likinitoka, nilitetemeka kama niliyenyeshewa na mvua kubwa kipindi cha baridi kali. Nilimtizama Angela, moyo ukafunga ngumi..akili ilinituma nimpige vibao hata nane ndio nianze kumwuliza mtu waliyekuwa wanawasiliana naye hadi anampachika busu kwenye simu. Lakini nikajikuta kwa lazima nisiyoifahamu, sijui ni kusema nilimwonea huruma, sikufanya hivyo. Nilisimama muda kidogo na kutikisa kichwa kwa uchungu. Nilishajua alikuwa yule yule aliyemleta na Nissan Terrano. “Eee lazima atakuwa mpenziwe, lazima” Niliwaza kichwa kikigonga kuonyesha kiasi gani niliumia moyoni.
“Angela, ni..ni..nana ni uuunawasiliana naye?” Nilimwuliza mwili mzima ukitetemeka kwa ghadhabu kali.
“Haikuhusu, Non of your Bussiness”
“Etiii!!!” Niling’aka nikiwa nimeukunja uso huku nikimfuata.
“Rudia maneno yako, sijakuelewa”
“I Sayed, mind your Bussiness” Niliinua mkono ambao uliviringa ngumi, nikamtizama. Nikahisi kama kuna kitu kinanionya, “Bakari usimpige mkeo, sio haki kabisa. Kama amekukosea jaribu kutumia njia nyingine ya kuhuisha uhusiano mwema, ukimpiga unaweza ukamwuua ukapata dhambi na pia ukaozea jela” Nilimtizama kwa dhadhabu kali, mwili mzima ukitetemeka. Zaidi ya dakika tano nilibaki kiniwaza jambo gani ama adhabu gani ningempatia mwanamke huyu.
“Hivi..Angela unadiriki kuniambia maneno hayo....Kumbuka ahadi ulizokuwa ukiniahidi...Angela uliniahidi hutoutesa moyo wangu. Uliniahidi upo radhi nikifa tuzikwe shimo moja nami....”
“Nani wa hivyo!!!, Nyooo!!” Hapo nilijua Angela alibadilika, alinijibu kwa kejeli akiviringa vidole mfano wa mashangingi yakisutana umbea.
“Wewe, kwani nani mwingine?”
“Mimi Angela nizikwe shimo moja na wewe!!!, umekosea Boka. Hata kama ningekupenda kiasi gani nisingewezi kuzikwa na wewe hata sekunde mbili, labda fulani....”
“Labda nani?”
“Wewe” Nilijua wazi alichotaka kusema, haikosi alitaka kusema labda yule aliyekuwa anaongea naye kwenye simu muda si punde. Alinijibu kwa dharau, niliumia sana moyoni. Kila siku Angela alikuwa akiniumiza na kuniteneka kidonda angali kibichi.
“Hebu niambie Angela, umenioa ama nimekuoa?”
“Kwani wee unaonaje?”Aliniuliza badala kunijibu.
“Nimekuuliza swali, napenda unijibu”
“Umenioa”Alinijibu, akibetua midomo yake utadhani imeteguka.
“Kama kweli nimekuoa, nihaki wewe kama mke wangu unijie nyumbani saa sita kasoro, kazi gani inakufanya unijie nyumbani kwangu usiku. Halafu umebadilika sana, si sawa na mwanzoni mwa mapenzi yetu. Unyumba hutaki kunipa...kila siku visingizio kedekede, kama hunitaki naomba uwe bayani kuliko kuutesa moyo wangu. Hebu tizama mwili wangu unavyokonda kwa ajili yako. Nimekusea nini hadi kunipa adhabu hii kali.....Angela hata nikipiga simu ofisini kwenu sasa hivi watanipa muda ulioondoka kazini, lazima utakuwa ulienda mahali. Huyo uliyekuwa ukiongea naye ni nani?. Niambie nimjue”
“Ni dereva teksi”
“Dereva teksi, yupi?”
“Huyo aliyenileta”
“Sawa, dereva teksi ndiye unamwita Dear...Darling?. Halafu mnapeana miadi!!” Angela alinyamaza kama dakika mbili, tatu hivi.
“Basi, punguza hasira dear” Angela alinifuata akanikumbatia na kunibusu. Nikajikuta nikilainika angali moyo bado ulikuwa ukisononeka.
“Naomba unisamehe, dear” Angela alisema, mikono yake ikitalii kifuani mwangu. Nilijikuta nimetulia kama mamba aliyejianika juani muda mfupi toka atoke majini.Niliamua kumsamehe, ikiwa ni njia ya kumfanya ajione mjanja, nilitaka kuchunguza mtu anayemfanya mke wangu anione Bwege.
“Nimeshakusamehe, ile cheni ya dhahabu uliyosema utanunua iko wapi?”
“Nimeibiwa”
“Wapi?” Nilimwuliza.
“Mjini, niliegesha gari langu maeneo ya Kariakoo kwenye Sonara moja, wakati nashuka garini, vibaka wakanipora pochi yangu”
“Oooo! Pole sana, twende ndani tukajipumzishe” Nilimsihi Angela.Tuliingia chumbani, siku hiyo hakuwa na ubishi wa kwenda ndani kama siku zingine. Kitanda chetu kikubwa kabisa, sita kwa sita kilikuwa kinatusubiri kituhifadfhi hadi asubuhi.
Nilivuta pumzi kwa nguvu na kuziacha zishuke taratibu, nilikuwa mtu wa kwanza kujitupa kitandani. Nilifikiri Angela naye angefanya kama nilivyofanya lakini haikuwa hivyo aliketi kwenye sofa la watu wawili pale chumbani.
“Karibu kitandani, mke wangu” Nilimsihi kwa sauti ya unyenyekevu.
“Baadaye, endelea kulala. Naenda bafuni kuoga” Chumbani kwetu kulikuwa na bafu ndani kwa ndani.
“Basi subiri tuoge wote, mke wangu” Nilimweleza nikiinuka kitandani.
“Hapana, naoga mwenyewe”
“Kwanini mke wangu siku hizi hutaki kuoga na mimi, nisubiri tuoge wote”
“Sitaki, kama unataka nenda kaoge mwenyewe, miye nitaoga baadaye” Alisema akijifunga taulo. Sikutaka kugombana na mke wangu, ilhali nampenda bado, niliamua kumwacha achague apendavyo. Nilihisi endapo ningemkorofisha uwezekano mkubwa wa kutokwenda kitandani ungekwepo. Nikakata shauri kurudi kitandani. Alioga akarejea chumbani, alijisafisha vema. Kisha akavaa suruali yake ya jinzi ambayo ilimbana vema mwili wake hasa mapaja na kiuno. Kuvaa kwenyewe ulimchukua dakika tano, ndipo alipofanikiwa kuitia mwilini.
“Dear, mbona unavaa jinzi ya kubana, kumbuka nataka kuwa na mtoto. Je nitampata kwa njia hiyo?” Nilimweleza Angela kwa upole, nikijaribu kumtomasa mwili wake.
“Usinshike, unataka mtoto wakati kunitunza miye mkeo unashindwa!!”
“Hiyo kashifa, mke wangu. Kuna kitu gani Angela ulichoniomba nikashidwa kununulia, kama ni gari nimekununulia, hereni na cheni za dhahabu nimekupatia pesa ya kununulia. Duka la nguo la mamilioni nimekufungulia, akiba benki ya milioni tano nimekufungulia......nini hasa ulichokosa kwangu?. Chakula kizuri unakula, nini nilichoshidwa kukutimizia”
“Cheni hujanitimizia maana pesa zote niliporwa na vibaka”
“Ndio umenieleza sasa hivi, nikipata hela nitakununulia”
“Waona sasa, huna pesa za kunitimizia”
“Hela ninazo lakini zina mipangilio mingine” Angela alicharuka kweli kweli alitaka nimpatie hela za cheni. Nikakata shauri kufungua kabati langu nililokuwa nimeweka akiba ya nyumbani. Nilimpatia shilingi laki mbili na nusu kama nilivyompa awali.
“Twende basi tukajipumzishe, dear” Nilimsihi nikimshika shika mgongoni.
“Dear nina shida”
“Shida gani?”
“Nitajisikia furaha endapo utanipa pesa nikakupa mapenzi”
“Etttiii!!!”
“Unashangaa nini?”aliniuliza kwa kejeli.
“Dear, nashangaa sana. Tena lazima nishangae. Hivi kweli tutafika?... nilikupa pesa ya cheni, umepoteza, nimekupa nyingine halafu unataka pesa ndipo ulale na mimi. Hapana siamini Angela, itanichukua muda kidogo kuamini maneno yako”.
“Hata kama itakuchukua muda lakini elewa kwamba pesa zako ndizo zilizokuwa zimenileta hadi nikaolewa na wewe, sina muda wa kuwa nawe tena” Maskini, nilijionea huruma mwenyewe. Bila kujizuia, machozi mazito yalinitoka. Jambo lililonifanya niumie moyo wangu, nilifanya sherehe kubwa sana siku nilipofunga ndoa, niliutambulisha ulimwengu kwamba nilipata mwanamke msomi na mwenye mapenzi ya kweli, nilitaka niwe mfano kwa kumsomesha mchumba hadi kufunga nae ndoa, ingawa sasa ndoa yangu ilibadilika kuwa chungu kama shubiri. Yale maneno ya wazazi wangu waliokuwa wakinionya yalijidhatiti akilini, nilijuta nikajua majuto ni mjukuu. Wazazi walinikataza nisimuoe Angela, nikatumia njia niliyojua kwamba wangeridhika na kunipa ruksa ya kufunga ndoa na Angela. Sasa kilio changu nimekuwa changu mwenyewe, kumbe wazazi wanaona mbali sana.
Nitaendelea kukupa uhondo huu wiki ijayo