TAFUTA HAPA

MAMA MDOGO SEHEMU YA TATU


     Ilipoishia,,,,Alipofika katika ofisi za utawala aliwaeleza walimu hali halisi kuhusu kuugua kwa mama yake. Walimu walimwita Jamal. Baada ya Jamal kumwona baba yake alishtuka kwani haikuwa kawaida yake kwenda kumtembelea shuleni.
 Inapoendelea,,,,“Shikamoo baba!” Aliamkia Jamal
“Marahaba mwanangu!” Aliitika Mzee Said.
“Baba karibu sana shuleni kwetu.” Alisema Jamal huku akimwangalia baba yake kwa furaha ya kutembelewa.
“Asante mwanangu,  je, unaendeleaje na masomo?” Alijibu na kuuliza Mzee Said.
“Vizuri baba, tunajiandaa na mitihani ya kumaliza muhula, je, hawajambo nyumbani?” Alijibu na kuuliza Jamal.
“Hawajambo kiasi ila mama yako anaumwa kidogo na angefurahi sana kama ungekwenda kumwona halafu utarudi kuendelea na maandalizi yako ya mtihani.” Alisema Mzee Said.
“Haiwezekani baba kumbuka hii ni mitihani ya kumaliza Kidato cha Tatu hivyo ninahitaji kuwa na muda wa kutosha kujiandaa.” Alijibu Jamal
Ni kweli lakini kwa sababu mama yako mwenyewe ameomba kukuona huna budi kwenda angalau ukamwone tu leo kisha kesho utarudi kuendelea na hayo matayarisho ya mtihani. Haya nenda ukajiandae nishakuombea ruhusa kwa walimu.” Alishauri baba yake.
Jamali aliondoka kuelekea bwenini kujiandaa huku akiwaza kuna nini mbona baba yake anasisitiza sana.  Alichukua begi lake dogo na kuongozana na baba yake hadi nyumbani. Walipofika tu walimkuta Aisha nje ambaye alimkimbilia Jamal na kumpokea begi kisha kumshika mkono.
“Shikamoo kaka Jamal” Aliamkia Aisha akimwongoza ndani.
“Mama anaumwa hawezi kutoka kitandani analia tu!” Alisema Aisha huku akionyesha wasiwasi mkubwa.
Jamal alimsikiliza mdogo wake lakini hakumjibu chochote aliingia chumbani na kumkuta mamake akiwa amelala kitandani.
“Shikamoo mama!” Aliamkia Jamal.
“Marahaba mwanangu nimefurahi kukuona baba!” Alimwitikia mama yake kwa sauti ya chini sana na ya upole.
 “Unaumwa nini mama yangu?” Aliuliza Jamal huku akimwangalia  Mama yake.
Mama yake alikuwa amebadilika sana rangi ya ngozi yake ilififia na kuonekana mweusi na alikuwa amepungua sana. Jamal akalia kwa uchungu huku akitaka kujua mama yake anaumwa nini.

 “Usilie mwanangu wewe ni kijana mkubwa kwa sasa mimi naumwa sana mwanangu kuna vitu nilikuwa nataka kukwambia, naomba unisikilize kwa umakini.” Aliongea mama yake kwa sauti ya chini sana.
"Nakusikiliza mama ongea tu.” Jamal alisema huku amemshika mkono mama yake.
Wakati huo wote pale chumbani walikuwa wawili tu, baba yake pamoja na mdogo wake walikuwa wamekaa sebuleni na wageni. Ndipo mama yake alipoanza kumwambia Jamal alichomwitia.
“Mwanangu nakuomba usome kwa bidii naamni utamsaidia sana mdogo wako katika masomo yake na pia mali zote zilizopo hapa ni za kwangu kampuni zote mbili na nyumba ambazo zipo kimara Mbezi ambazo zina wapangaji zote ni zangu pamoja na nyumba hii tunayoishi. Mimi nilikutana na baba yako nikiwa tayari nimeshajiendeleza sana  kimaisha na nilimsaidia hadi akapata kazi Wizara ya Kilimo na baadaye tukawa tunashirikiana pamoja katika kazi zangu, nimekwambia hivi ili ujue hizi mali ni zako wewe na mdogo wako naomba msome kwa bidii.” Kabla hajaendelea kuongea Jamal alimkatisha.
“Lakini mama kwa nini unaongea hivyo? Twende hospitali mama utapona tu mama bado tunakuhitaji.” Huku akiwa analia Jamal alimtaka mama yake aende hospitali.
“Mwanangu nakupenda sana wewe pamoja na mdogo wako naamini Mungu atawasaidia mimi siwezi kupona naumwa kansa ya kizazi na imefika katika hatua mbaya sana, naomba usilie ningependa kuona mkifurahi muda huu ambao tuko pamoja.” Alisema mama Jamal huku akiwa anatabasamu na kumfuta machozi mtoto wake na kumshika mkono. Mama yake  alikuwa anapata maumivu makali sana kwa wakati huo.