TAFUTA HAPA

MAMA MDOGO SEHAMU YA TANO


ILIPOISHIA....“Usijali kuhusu hilo mpenzi, kwani mimi nilichoamua hakuna anayeweza kunipinga. Wewe ndiye utakuwa mama mwenye nyumba kuanzia sasa. Hapa ni kwako sawa mamaaa?” Alisema Mzee said kwa kujiamini huku akicheka.
INAPOENDELEA...Mzee Said aliamua kumtembeza Sophia pale nyumbani na kumwonyesha mazingira yote. Tangia siku ile Sophia aliishi na Mzee Said kama mke na mume na aliponogewa na mapenzi ya mke mpya aliamua kufunga ndoa harakaharaka bomani tena kisiri bila watu wengine kujua.
********
Siku moja Jamal aliomba ruhusa kwa mwalimu ili aende Hospitali kutokana na kusumbuliwa na homa.  Baada ya kuruhusiwa aliamua kwenda nyumbani ili akamtaarifu baba yake juu ya kuumwa kwake na kisha ampeleke hospitali. Ilikuwa ni siku ya Jumamosi, Jamal alijua lazima atamkuta baba yake nyumbani. Alipofika na kuingia getini, aliona gari la baba yake likiwa limepaki. Jamal alifurahi sana kwani alikuwa na uhakika kuwa baba yake yupo.
“Afadhali nimemkuta baba.” Aliwaza Jamal na kugonga mlango.
Baada ya kugonga mara kadhaa na kukosa majibu aliamua kuingia ndani na kuanza kuita.
“Baba! Baba!” Aliita Jamal lakini hakupata jibu.
Wakati huo baba yake alikuwa chumbani amepumzika na Sophia. Baadaye Mzee Said alisikia sauti ya Jamal ikiita kutoka sebuleni, alitoka haraka kuelekea sebuleni na kumkuta Jamal.

“Hujambo Jamal! Vipi mbona uko hapa shule imefunga?” Alisalimia na kuuliza Mzee Jamal.
“Sijambo baba shikamoo! Shule hatujafunga ila nimekuja hospitali nasumbuliwa na homa.” Alijibu Jamal. Kisha baba yake alimsogelea na kumshika mkono.
“Pole sana mwanangu, sasa umekwenda hospitali?” Aliuliza Mzee Said.
“Hapana baba ndo nimekuja ili unipeleke hospitali.” Alisema Jamal.
“Sawa hebu nijiandae ili twende.” Alishauri Mzee Said.
Wakiwa wanaendelea na mazungumzo mara Sophia alitoka chumbani.
“Vipi darling {mpenzi} kuna mgeni?.” Aliuliza Sophia huku akimwangalia Jamal.
“Baba kwani huyu ni nani?” Aliuliza Jamal huku akimwangalia Sophia kwa uso wa mshangao.
“Ahaa, imekuwa vizuri sana mwanangu umekuja ili uweze kumfahamu mama yako mdogo.” Alijibu Mzee Said huku akigeuka kumwangalia Sophia, ambaye muda wote alikuwa akitabasamu.
“Mama yangu mdogo?  Kivipi baba?” Alihoji Jamal.
 “Ndiyo mwanangu huyu ndiye atakuwa mama yenu mdogo kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali hapa nyumbani ikiwa ni pamoja na kuwatunza ninyi.” Alieleza Mzee Said.
Jamal alinyamaza kimya kwa muda huku akimkodolea macho yule binti bila kusema kitu.
”Hivi huyu Baba ana matatizo gani? Huyu msichana si sawa tu na binti yake? Haya ni mambo ya ajabu sana. Kamwe siwezi hata siku moja kumheshimu mwanamke wa umri kama huu kuwa mama yangu.” Aliwaza Jamal.
“Mwanangu sasa nadhani mtafahamiana vizuri na mama yako kadiri siku zinavyozidi kwenda.” Alitamka Mzee Said.
“Mama yangu! Huyu hawezi kuwa mama yangu hata siku moja. Mama yangu hawezi kurithiwa na mtu yeyote yule, halafu Baba, mbona huyu msichana hata hamlingani anaonekana ni msichana mdogo sana huoni anaweza kuwa hata mtoto wako?” Alihoji Jamal  huku akionekana kuwa na hasira sana. Nini kinaendelea