Ni ukweli kwamba wako wanawake wengi sana ambao wanahesabu kuwa ni  baraka na jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwaumba wenye sura nzuri na  wenye mvuto. Pamoja na ukweli huu, ni wazi na imethibitika kwamba wako  wanawake ambao wanahesabu kuzaliwa warembo ni mojawapo ya laana au mkosi  kwasababu ya zile hali ambazo wamezipitia hususani katika mahusiano yao  ya kila siku na wanaume.
Mara kwa mara kumekuwepo na tabia ya wanaume kutamani sana kuwa  kwenye mahusiano na wanawake warembo, na hupenda kuwatongoza hao mara  kwa mara ingawa moyoni mwao wanawaangalia warembo hawa kama wasichana wa  kula nao raha tu “good time girls” na wala sio wake wakuoa.
Utakubaliana na mimi labda umewahi kuona mwanaume anakuwa kwenye  mahusiano na binti mzuri sana kisura na kiumbo tena wanakuwa kwenye  mapenzi kwa muda mrefu tu huku huyu binti akijua mbeleni kuna ndoa,  ghafla ukija kusikia huyu kaka anaona unapigwa mshangao kuona wala sio  yule binti mrembo anayeolewa.
Hii imewaacha mabinti wa aina hii katika maumivu makali sana ya moyo,  na wengine wamekata tama na kuamua kujirahisisha ili mraadi maisha  yaende. Wengine wameamua kukaa wakitunzwa na waume za watu kwasababu wao  wamejithibitishia kwamba kuolewa hakupo.Tafiti zinaonyesha kwamba  ukiona mwanaume aliyeamua kukaa muda mrefu na mwanamke mrembo, mara  ningi unakuta ni wale wanaume wenye tabia za kisanii “players” ambao  hata wao huwatumia mabinti hawa na kuwatelekeza hapo baadae.
Inasemekana imani au mtazamo huu hauko tu kwa wanaume bali hata  wanawake wale wenye uzuri au urembo wa kati au wasio warembo kabisa  wanajua na kuamini hivyo na mara nyingine huwarushia vijembe wale  wanawake warembo kuwa “utachezewa tu na utaachwa na wataolewa wengine”.  Na pale inapotokea kwenye mahusiano binti wa kawaida akagundua mpenzi  wake wa kiume ametembea au husiana kinyemela na binti mrembo zaidi  kuliko yeye, utakuta wakikutana kwenye kupashana au hata kwenye ugomvi  wa kuandikiana ujumbe wa maneo, huyu binti wa kawaida humwambia yule  mrembo kwamba “we jifurahishe tu ila usiamini kwamba utaolewa, huyu  mwenzako anakuchezea tu anajuwa nani wa kuoa”. Unadhani imani hii  wameitoa wapi?
Wakati mfumo au mtazamo huu unapoenea au kujirudia zaidi, wanawake  hawa warembo au wazuri wa sura na umbo huamini kwamba wanaume wote  ndivyo walivyo, wanaamini kwamba wanaume wote huwasogelea ili  kujifurahisha kimapenzi tu na baada ya hapo kuwakimbia. Wakati huu wa  kusubiria kumpata mwanaume wa kuoa “Mr. Right” ukizidi wanawake hawa  huchoka na kukata tama, na hivyo wao sasa huamua kukimbizana na kutafuta  mwanaume wa kuwapenda na kutulizana nao.
Tabia hii ya kuwafukuzia wanaume kwa bahati mbaya kuwagharimu sana  wanawake hawa kwasababu wanaume wengi wanamtazamo hasi kwa wanawake wa  jinsi hii. Wanaume wengi wanaamini wao ndio wanatakiwa kuwa wa kwanza  kumtongoza mwanamke na sio mwanamke kuwa wa kwanza kuwatongoza wao, na  mbaya zaidi anapokuwa mwanamke mzuri ndio shida huongezeka, wengine  wakianza kuambiana “huyu lazima atakuwa mgonjwa anataka kuambukiza  wengine”. Hapa unaweza kuelewa ni kwa kiasi gani hali huwa ya kutatiza.
Kwa upande mwingine, wanawake hawa wanaoonekana wazuri wa umbo na  sura, sio halisi kama wanavyoonekana. Kwa mbali ni kweli mwanaume yeyote  atavutiwa nao lakini jinsi unavyowakaribia na kuwafahamu unagundua  mengi yanayohuzunisha na kuogopesha kuishi nao. Unagundua kuwa uzuri  mwingine umeongezewa kutoka madukani zaidi na sio ulio halisi. Mara  nyingine uzuri huu na ile hali ya kuonekana ni wagharama sana  huwaogopesha wanaume wasio na kipato kikubwa na kwahiyo wanaume hawa  wakishapata kabahati ka kufaidi penzi mara moja au mbili wanakimbia tena  kwa kasi wakihofia kukamuliwa kiuchumi, ingawa mara nyingine hofu yao  hii huwa sio ya kweli. Inasemekana baadhi ya wanawake wa aina hii  huwekeza zaidi kwenye kuonekana wazuri na walimbwende ili kuficha au  kufunika baadhi ya mapungufu yao.
Wanaume wengi walioulizwa sababu za kuwatumia na kuwatelekeza  wanawake wa jinsi hii walisema kuwa, kwa kutembea, kuonekana nao au  kufanya nao mapenzi, wanaume hawa hujihisi sifa sana, hususani  wanapoonekana na wanaume wenzao, yani ni kama vile timu ndogo iliyopata  nafasi kucheza katika kombe la dunia. Unajua tena wanaume wanavyopenda  kujionyesha wanapokuwa na wanawake wazuri mbele ya macho ya wanaume  wenzao.
Wamesema kwamba wanapowaza kuishi na wanawake hawa kama mume na mke,  huwa wanazidiwa na hofu ya kuelemewa au kujihisi kutokuwa salama “sense  of insecurity”. Mioyoni mwao wanahisi kwamba kama wanaume wenye hela  wamekuwa wanamfuatilia kwa kasi kubwa hivi mwanamke huyu, vipi  nikishaoana naye?? Si ndiyo kila siku kusuguana na kukorofishana  vishawishi vinapozidi? Je nitaweza kustahimili?
Wanaume wengine walioulizwa walijibu kwamba, wanawake wa jinsi hii ni  wa gharama sana, sio rahisi kuwaweka mjini na kuhakikisha wanaishi  maisha yao ya kawaida kama hauna fedha ya kutosha. Hata wale wanaume  wachache waliokuwa na hao wanawake kwa muda wa maswali haya wameeleza  jinsi wanavyohisi wanatumia fedha nyingi na yamkini zaidi ya  wanavyojiweza.
Wanawake wa aina hii watahitaji mitoko ya nje ya mji, sehemu  zilizojitenga, sehemu za faragha ambazo ni za bei ghali, wanataka zawadi  za gharama, ukitaka kuwapa zawadi za kushtukiza “surprise” basi  ujipange, sio vitu vya kitoto vitakavyomsisimua aweze kukwambia  “waoooooow…this is wonderful” hapo lazima ujipinde mfukoni haswa.
Ukitaka kuwatoa nje kwa ajili ya chakula cha jioni basi lazima kwenda  maeneo wanayoenda watu maarufu, mkitaka kwenda kupumzika kidogo nje ya  nyumbani basi uwaambie wachague wao wapi pa kwenda, na hapo  utakapotajiwa ni pa gharama kubwa sana, na imeelezwa kwamba pamoja na  mambo yote haya ya gharama kubwa bado huko wapenzi hawa wanapoenda  msichana huyu anaishia kuonekana ni mwanafunzi asiyejua tendo la ndoa  kabisa tofauti na hali aliyoionyesha “poor perfomer”, wanaume wengine  wanasema inaonekana kama kupoteza tu pesa, unaishia kutokufurahia penzi  lenyewe.
Na wengine wameenda mbali zaidi kueleza kwamba hata unapotaka kuzaa  na mwanamke wa jinsi hii basi yeye anataka mtoto mmoja au wawili tu  akiogopa asije kuliharibu umbo lake, tofauti na kiu ya mwanaume ya  kupata watoto zaidi ya wawili. Imeelezwa kuwa hata ujuzi wa kupika kwao  ni shida maana kutwa kucha wako “bize” na sura zao, na hata ukikaa nao  sio watu wakufurahisha zaidi ya kutumia tu hela zako “they are boring”.
Pamoja na uchunguzi huu na ukiangalia hali halisi ya maisha yetu ya  kila siku tena katika jamii tofauti utagundua kwamba wanaume kiu yao sio  kuoa wanawake wenye umaarufu, au wenye kujulikana sana, au walio  warembo kupindukia, bali wanaume wanapotaka kutafuta mke wa kuoa  wanaangalia tabia na haiba zilizojificha, wanauliza tabia ya huyo  msichana, wanataka kujua anavyohusiana na watu, wataangalia nyendo zake  kuanzia wakati anasoma.
Ni ngumu kuwakuta wamenaswa na aina ya wanawake ambao wanataka  kuonekana wakati wote, wanataka wajulikane kuwa wao nao wapo kwenye  makundi ya watu, la hasha. Kiu zao ni kuwa na mwanamke ambaye atakuwa  mke anaye leta furaha nyumbani, anaye sikiliza, anaye weza kushauri na  kushaurika, aliyeko tayari kufundishika sio kuwa mwalimu kwenye kila  kitu, anayeweza kuandaa mapishi mazuri yatakayo wafurahisha watoto na  mume wake, sio kila siku kuelekeza kipikwe nini wakati yeye analinda  kucha zake zisiharibike.
Hivi umewahi kujiuliza kwanini watu wengi waliooa wakiwa na  michepuko, hiyo michepuko ni mabinti warembo na walimbwende ila  hawajaolewa, hivi hujajiuliza kwanini hawajaolewa? Na hata wengine  wakiolewa hizo ndoa kila siku tia maji tia maji, wataachika leo na  kuolewa kesho na kuachika kesho kutwa nakuolewa tena mtondogoo.
                 
Unadhani hawa wanaume wanaoenda kwa hao wanawake ni kwamba hawajui  wanachokitaka? utashangaa hata umpe mapenzi gani bado hawezi kukwambia  atakuoa, ingawa yuko tayari akupangishie nyumba au hata akujengee lakini  ulale huko mwenyewe, yeye anaenda kulala na mke wake. Ushauri wangu wa  bure kwa wanawake wa jinsi hii; badilikeni tabia zenu, jitihada  mnazotumia kwenye kucha na sura zenu ziwekeni kwenye kushuhulikia tabia  na haiba zenu, la sivyo mtasubiri sana tu.